*Mazao ya trilioni 1.52/- yauzwa kupitia vyama vya ushirika
NA MWANDISHI MAALUM
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema usimamizi mzuri wa sera za kiuchumi na fedha sambamba na kujenga mahusiano mazuri kati ya walipa kodi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kumechangia kuimarika kwa makusanyo ya kodi.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Aprili 13, 2022 wakati akisoma hotuba ya kuhitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake pamoja na Mfuko wa Bunge, jijini Dodoma. Bunge limepitisha kwa kauli moja bajeti hiyo.
“Kwa mfano, Desemba 2021, TRA ilikusanya shilingi trilioni 2.51 sawa na ufanisi wa asilimia 109 wa lengo la kukusanya shilingi trilioni 2.29 katika kipindi hicho. Kuvunjwa kwa rekodi hiyo ya makusanyo ya kodi ni kielelezo tosha cha kazi nzuri anayoifanya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan,”amesema.
Waziri Mkuu amesema kuwa takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) zinaonesha kuwa katika kipindi cha Machi, 2021 hadi Februari, 2022, Serikali imeweza kuvutia na kusajili jumla ya miradi ya uwekezaji 294. “Miradi hiyo inatarajiwa kuwekeza mtaji wa thamani ya dola za Marekani bilioni 8.13 na kutoa ajira kwa watu wasiopungua 62,000.”
Amesema kuwa Afrika inamtazama Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa miongoni mwa viongozi waliochangia kuliweka bara hili katika ramani nzuri ya dunia kutokana na namna alivyofanikiwa kushughulikia suala la UVIKO-19.
Ameongeza kuwa mkopo nafuu wa sh. trilioni 1.3 kutoka IMF umeiwezesha Serikali kupeleka sh. bilioni 100.58 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya za sekondari 214. “Taratibu za kuanza ujenzi huo, zinaendelea kwenye kata za majimbo yote nchini.”
“Tumepeleka shilingi bilioni 30 kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari mpya za wasichana kwenye mikoa 10 ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kujenga shule moja ya sekondari ya wasichana kwa kila mkoa wa Tanzania Bara.”
Amesema kupitia mpango huo, Serikali ya awamu ya sita imetoa sh. bilioni 204.4 kwa ajili ya utekelezaji wa afua mbalimbali za afya. Afua hizo zinajumuisha kuimarisha huduma za dharura, huduma za wagonjwa mahututi, wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu na huduma za maabara.
“Kwa upande wa vifaa na vifaa tiba, Serikali imenunua mashine za CT Scan 29, MRI nne, magari 253 ya kubebea wagonjwa, magari 250 kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za afya ngazi ya wizara, mikoa na halmashauri zote nchini, magari nane ya damu salama na magari 30 ya kusambaza chanjo”.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema sekta ya ushirika nchini imeanza kuonesha mafanikio makubwa ikiwemo kuimarisha uuzaji wa mazao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani, kusimamia urejeshaji wa mali za vyama vya ushirika, kufufua viwanda vidogo na vikubwa na kujenga imani ya wakulima katika ushirika.
Akizungumzia kuimarika kwa uuzaji wa mazao kupitia Mfumo wa Stakabadhi Ghalani, Waziri Mkuu amesema hatua hiyo imewezesha kuimarika kwa bei katika baadhi ya mazao. “Hivi karibuni tumeona bei ya kakao ikiongezeka maradufu kutoka shilingi 2,500 hadi 5,000 kwa kilo moja baada ya kutumia mfumo wa ushirika na stakabadhi ghalani.
Aidha, kupitia uhamasishaji wa masoko na uwekezaji katika vyama vya ushirika, mazao ya aina 10 yenye uzani wa tani 575,296 zenye thamani ya shilingi trilioni 1.52 yaliuzwa kupitia ushirika kwa kipindi cha Julai 2021 hadi Februari 2022.”
Amesema ushirika umeendelea kuwa sehemu ya kipaumbele kwa Serikali ya awamu ya sita katika kuhakikisha unakuwa na tija kwa wakulima, wafugaji na wavuvi na kutaja mafanikio mengine kuwa ni kusimamia urejeshaji wa mali za vyama vya ushirika zikiwemo mashamba, viwanja, majengo, maghala na nyinginezo zenye thamani ya sh. bilioni 68.
“Hatua zinazochukuliwa katika kuimarisha utendaji wa vyama vya ushirika zimeanza kuonesha mafanikio makubwa kama vile kuanzisha na kufufua viwanda vidogo na vikubwa 452. Viwanda hivyo ni pamoja na viwanda vya kahawa, alizeti na pamba vikiwemo vya kuchambua pamba vilivyopo Kahama na Chato.”
Hatua hizo, Waziri Mkuu amesema, zimesaidia kujenga imani ya wakulima katika sekta ya ushirika ikilinganishwa na hapo awali. “Kutokana na imani iliyojengeka, idadi ya vyama vya ushirika vyenye usajili vimeongezeka na kufikia 9,741 mwaka 2022 ikilinganishwa na vyama 9,185 mwaka 2020, sawa na ongezeko la vyama 556. Pia idadi ya wanachama imeongezeka na kufikia 914,948 kutoka mwaka 2021 hadi mwaka 2022.”
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema ili ushirika uendelee kuimarika, bado kuna changamoto ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi ikiwemo kukosekana kwa elimu ya ushirika kwa wadau muhimu na utitiri wa tozo unaofanya bei anayolipwa mkulima kuwa ndogo.