NA DIRAMAKINI
MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC),Dkt.Sophia Kongela amesema, ni shauku yao kuona miradi mbalimbali inayotekelezwa na shirika hilo ikiwemo ya ujenzi wa nyumba jijini Dodoma inakamilika kabla ya muda ili kutoa nafasi katika utekelezaji wa miradi mingine nchini.

"Sisi tunashukuru kama bodi tumepata nafasi ya kuja kutembelea miradi yetu, tumeona kuna mwendelezo mzuri, kwa sababu ilivyoanza tuliona na tumeona tuko makini nini kinaendelea.
"Tumekuwa tukipata feedback (mrejesho),tumetoka chini ambako huwa kunasumbua,na kwa sasa hakuna kitu cha kutusubirisha, kuna maendeleo tunaomba muendelee kupambana na sapoti yetu mnayo shirika zima linawaangalia ninyi,"amefafanua Dkt.Kongela.

Dkt.Kongela ameongeza kuwa, kukamilika kwa miradi hiyo kunatoa fursa kwa miradi mingine iliyopo jijini Dar es Salaam, hivyo akawataka kutekeleza kwa kasi kuhakikisha kwamba inafanyika kwa haraka.

"Tufanye kazi kwa bidii mnasapoti yetu tunawatakia kazi njema na kila la heri tupambane ninyi bado ni vijana mnaweza,endeleeni hivyo hivyo tumalize mapema iwezekanavyo hata (DG) ameliona hilo angalau tumalize miezi sita kabla, utaleta tija kubwa kwa taifa,"amesema Dkt.Kongela.
Pia amesema, ili kasi ya ujenzi iwe kubwa wanahamasisha vifaa vya ujenzi viwe eneo la kazi na si muda wa kazi ndiyo mchakato wa manunuzi unaanza kwani kwa kufanya hivyo kutachangia kasi ya ujenzi kupungua.
Uhandisi na Ujenzi
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uhandisi na Ujenzi wa NHC, Haikamen Mlekio amesema, wanatekeleza mradi huo katika maeneo ya Chamwino na Iyumbu jijini Dodoma.

"Hapa tuliposimama tunajenga nyumba 303 kwa maana majengo haya yako 300 na majengo ya huduma yako matatu, tuna Nursery, Club house pamoja na duka na katika hizi nyumba tulizokaa hapa katika hizi nyumba 1000 hizi 300 ziko za aina tatu,"amesema Bw.Mlekio.
Amefafanua kuwa, "Nyumba ziko 150 za mita za mraba 120 square mita na square mita ziko 100 na square mita 75 ziko 50 na jumla zinakuwa 300. Lakini kule tulikotoka mwanzoni kuna nyumba za aina tatu vilevile kuna nyumba zenye square mita 115, kuna nyumba zenye square mita 85, kuna nyumba zenye square mita 79, lakini ukiziangalia kwa nje ni kama ndogo, ni nyumba ambazo tunasemaga ni toroka uje, chumba kimoja kinajitegemea kwa nje kule Chamwino kuna maghorofa yako apartment 100, tatu apartment 60 za vyumba vitatu na apartment 40 vyumba 2 na jengo moja la huduma nalo ni duka," amesema.
"Huu mradi wa nyumba 300 upande ule au mradi ule wa nyuma kabla ya huu huwa tulikuwa shirika linagharamia gharama za kuleta umeme na maji toka Hayati Magufuli alipotoa lile agizo kule Mtwara kwenye mradi wetu wa Raha Leo wakati anafungua pale aliagiza kwamba watoa huduma watuletee huduma za umeme na maji,"amesema.
"Hilo Mwenyekiti lilifanyika kwenye ile Awamu ya kwanza sisi tulilipia tu gharama za kuunganisha mita hivyo hizo nguzo zote na transfoma,"amesema.