Dawa za kulevya zilivyoacha kilio kwa Mtumishi wa Umma Shirika la Posta-4

NA GODFREY NNKO

YOHANA Komba ambaye alikuwa mtumishi wa umma kupitia Shirika la Posta kabla ya kufukuzwa mwishoni mwa mwaka 2012 kutokana na uvutaji wa heroine uliopitiliza ambao ulimshawishi kujiingiza kwenye vitendo vya wizi ili kupata fedha za kununulia dawa hizo anasema kuwa, baada ya kufukuzwa walienda kufanya mchakato mwingine wa maisha ingawa safari ilikuwa ngumu.

"Tuliondoka mpaka hotelini, lakini tulipofika hotelini mzee akachukua chumba chake na mimi chumba changu, sikuwa na hela nikamuomba mzee anisaidie elfu 20,000, akanipa nikaenda kununua unga nikatumia na mwingine nikaweka wa akiba kwa sababu kesho yake tulipaswa kusafiri kwenda Dodoma ambapo nilikuwa niutumie safarini. Niliporudi kutoka kununua unga, mzee alishangaa sana kurudi kwangu, akasema alijua nimekimbia nikamwambia sikukimbia nilikwenda tu sehemu.

"Tulisafiri salama hadi kufika Dodoma nyumbani na cheki (hundi) alikuwa nayo mzee (baba yake) yeye tayari na nimeshafukuzwa kazi sina jinsi, ambapo siku moja majira ya usiku tukiwa tumekaa mezani tunakula, mzee aliniambia kwamba,mwanangu Yohana...alikuja kunichukua Tabora akiwa na bastola, kwa sababu alikuwa ameshapata taarifa zangu kwamba nipo na majambazi na tabia yangu ni mbaya, alikuja na bastola alidhani angenikuta na majambazi. Endelea sehemu ya nne...
"Kwa hiyo alikuwa na image (picha) tofauti na mimi, lakini alisema ameshangaa kuona hata siku aliponipa elfu 20,000 naenda sehemu nilirudi akasema mbona haupo kama nilivyosimuliwa awali kuhusu mwenendo wako,"amesema.

Anasema, kwa baadaye mchakato wa kwenda kutoa fedha zake benki kulingana na kiasi ambacho kilikuwa kimeandikwa kwenye cheki ulifanyika, ambapo fedha hiyo ilitolewa benki na ikawekwa katika akaunti ya baba yake ikiwa ni shilingi milioni 14.

Pia alikuwa amejiunga kwenye Chama cha Wafanyakazi wa Mawasiliano (TEUTA) ambapo walikuwa kuna fedha wanakatwa na Chama chao cha Kuweka na Kukopa ambacho kilikuwa kinaitwa KK Saccoss kikiwa na makao yake makuu Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam (Posta na Simu Savings and Credit Cooperative Society Limited).

Bw.Yohana Komba anasema, katika hicho chama alikuwa amechangia kama shilingi milioni nne na kwa vile alikuwa amefukuzwa kazi alibidi arudishiwe fedha hiyo kwa kupewa cheki ya milioni nne.

"Baada ya kupewa hizo milioni nne, baba alizichukua na kwenda kuninunulia kiwanja huku zingine zikibaki katika akuanti ya baba,"anasema.
Aendelea na Heroine

Bw.Yohana Komba anafafanua kuwa, aliendelea kutumia dawa za kulevya akiwa nyumbani Dodoma. "Nimerudi nyumbani, nimefukuzwa kazi, lakini dawa za kulevya bado ninatumia tena kwa kiwango kikubwa".

Anasema,taarifa zake za kutumia dawa za kulevya zilikuwa zimeenea kila mahali na baba yake alishauriwa ampeleke Kituo cha Methadene katika Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutumia dawa hizo.

Safari ya Kliniki

"Kweli mwaka 2013 mwishoni nilielekea Dar es Salaam, nikaanza kuhudhuria Kliniki ya Methadone katika Hospitali ya Mwananyamala kuanzia mwaka 2014 hadi 2017.

"Nimetoka kuvuta unga, nimehamia kwenye Methadone,nilikuwa ninakunywa kila siku, haijalishi iwe Jumatatu, Jumapili au sikukukuu,lazima niende hospitali kumeza Methadone,lakini nikajiona bado nipo kwenye utegemezi, ingawa utegemezi ule ninaupata bila hela,nikajiona nipo kwenye uraibu bado, hivyo nilikuwa ninatoka pale kumeza Methadone, ninarudi nyumbani, nikifika nyumbani ninaanza kunywa tena pombe, nikawa ninajiona mazingira ni kama yale yale,hakuna mabadiliko na watu ninaokutana nao ni wale wale.

Miaka mitatu Kliniki

"Kwa hiyo, ikaenda hadi miaka mitatu, angalau nimeanza kurejea katika hali ya kawaida baada ya kunywa Methadone kila siku,na kiwango changu cha uraibu kilikata kutoka asilimia 130, kwenda 30 na kufikia asilimia tano, ingawa bado hiyo asilimia tano ni kubwa kwa mraibu, nikafika kwa daktari akaniuliza ninaendeleaje na unajisikiaje...nikasema nipo sawa.

"Ingawa baada ya kupunguza hadi asilimia tano ambayo ni kama kitone, kiwango ambacho ni kidogo, lakini pale nilipokuwa ninakosa Methadone ninapata maumivu, kwa hiyo nilipopata safari ya kusafiri kwenda Nairobi, nilirudi pale Kituo cha Methadone Hospitali ya Mwananyamala kutoa taarifa kuwa ninasafiri, nao waliridhishwa na hali yangu, nikapewa ruhusa.Kwani hali yangu ilikuwa imeimarika.

"Kwa sababu ukiwa umekunywa Methadone kwa muda mrefu, kuna kiwango ambacho wanakuangalia na kufahamu, huyu mtu ana uwezo mzuri wa kuendelea na majukumu yake mitaani,"anasema.

Ajiondoa Kliniki

Bw.Yohana Komba anasema, ilipofika mwaka 2017 mwishoni alisafiri kwa wiki kadhaa kwenda Nairobi nchini Kenya kumpelekea mdogo wake gari ambalo alilinunua.

Akiwa Nairobi anasema, alijikuta akijihusisha na unywaji wa pombe (bia) aliporudi nchini, mwaka 2019 kwenda mwaka 2020 alitoa taarifa katika Kituo cha Methadone kuwa anaondoka, kwani afya yake imeimarika na ameachana na utumiaji wa dawa za kulevya na aliruhusiwa kwenda kuendelea na majukumu mengine ambapo walipotaka kumtangaza kama shuhuda aliyeachana na uraibu aliwagomea.

Ni pombe, heroine

Anasema kuwa, mwaka 2020 alikunywa pombe kwa mwaka mzima. "Siku moja baada ya kunywa pombe niijaribu kutumia unga (heroine) tena, ambapo baada ya kufanya hivyo nilirudia hali hiyo ya uraibu tena hali yangu ikawa mbaya zaidi ya awali wakati sasa nikiishi Dar es Salaam, ingawa nilikuwa nikienda mara kwa mara Dodoma kuwasalimia wazazi wangu na sikuendelea na pombe tena bali nilirudi kwenye matumizi ya dawa za kulevya kwa kasi kubwa mno.

"Nilipokuwa naongea na mama kwenye simu alikuwa akinibaini sauti kwamba nimetumia dawa za kulevya, si unajua mzazi ni mzazi tu, japo nilikuwa nakataa, wakati mwingine nikienda ananiambia mbona afya yako imedhoofika shida nini, ninamwambia ni changamoto za hapa na pale, si unajua nipo peke yangu, muda huo nipo Dar es Saam kwangu, nafanya mambo yangu, lakini ninapiga simu nyumbani kuomba matumizi na wanisaidie fedha,"anasema.

Fedha na dawa

"Mimi shilingi laki moja kumaliza kwenye unga ni siku moja tu, ukinipa milioni ndani ya wiki moja au mbili imeisha kama nina elfu 20,000 ninatumia kidogo kidogo, kama nina laki tatu (300,000) ninajifungia ndani ni kuvuta unga tu sitoki kabisa, sasa wakati naendelea endelea hivyo nikawa nawasiliana na rafiki yangu Twaha akasema yuko Bomang'ombe Moshi, akasema anatoa toa huduma ya kusaidia waraibu huko, tukaendelea kuwasiliana wasiliana akaniambia anataka kufungua nyumba ya kutoa huduma huko.

"Tukazidi kuwasiliana akaniambia anataka kufungua nyumba nikamwambia endelea na mapambano, anajua mimi nimesisimama kutumia dawa hizo kwa sababu alikuwa akinifahamu vyema kipindi cha nyuma kwamba natumia. Alipomaliza kufungua nyumba siku moja tukawasiliana, nikamwabia ndugu yangu, nakuja kukutembelea akasema karibu sana, nikasafiri hadi Dodoma nikakaa kidogo baadaye, nikaenda Moshi akanielekeza nikafika kwake kwa sababu nimetokea nyumbani nilikuwa nakula vizuri, kwa hiyo nilikuwa na afya kidogo imeimarika,"anasema.

Afika Moshi

"Rafiki yangu (Twaha Amani) kabla sijamwambia yeye akabaini ninatumia baada ya kuniona tu, kwani ana uzoefu wa kutosha nikakiri, nikamwambia natumia nimekuja kupata usaidizi, akanipa usaidizi mpaka sasa nipo kwake nina miezi miwili sasa tangu nimefika situmii kilevi chochote japo hisia huwa zinakuja, lakini najizuia kutokana na misingi tunayoifahamu na kufundishwa hapa,"anasema.

Wito kwa vijana

Aidha, Bw.Yohana Komba ametoa wito kwa vijana na jamii ya Watanzania, kuliona tatizo la dawa za kulevya ni kubwa na kulichukulia uzito wa namna yake katika kuweza kulitokomeza kwani lina athari kubwa katika nguvu kazi ya Taifa.

Bw.Komba anasema, anatamani siku moja Mungu amvushe katika hali anayopitia ambayo imezima kabisa ndoto zake huku ikimpotezea kazi ambayo alipaswa kutumia taaluma yake kulisaidia Taifa kusonga mbele.

"Dawa za kulevya, ni janga hatari sana, vijana wenzangu msikubali kushawishika kwa namna yoyote kujiingiza katika huo ushetani kwa kuuza au kuvuta, kwangu dawa za kulevya zimezima ndoto za maisha yangu, ninachumuomba Mungu ni yeye kunisaidia ili niondoke katika hali niliyo nayo kwa sasa, na kuanza upya safari ya maisha yangu,"anasema Bw.Komba.

Ajipeleka Sober

Bw.Yohana Komba ndani ya mwaka huu baada ya kuona hali ya maisha yake na afya inazidi kuyumba alijipeleka mwenyewe katika nyumba ya upataji nafuu ya Surrender for Freedom Teatment Center Njia Panda (Himo) Sober House mkoani Kilimanjaro.

Hii ni nyumba ambayo inamilikiwa na rafiki yake ambaye walikutana naye huko Tabora wakati wakivuta wote dawa za kulevya, Bw.Twaha Amani ambaye naye alifukuzwa kazi na kuondolewa cheo cha uaskari wa Jeshi la Polisi kutokana na utumiaji uliopitiliza wa dawa za kulevya uliochangia kujiingiza katika vitendo vya uhalifu na kuzorotesha utendaji kazi.

Twaha Amani

Mkufunzi na Mkurugenzi wa Surrender for Freedom Teatment Center Njia Panda (Himo) Sober House mkoani Kilimanjaro,Bw.Twaha Amani anasema,kituo chake ambacho kilianza hivi karibuni wakati kikiendelea na taratibu nyingine za kiserikali kimefanikiwa kuwaunganisha vijana zaidi ya 20 ambao walikuwa wanatumia dawa za kulevya na hali zao zinaendelea vizuri.

Anasema, Bw.Yohana Komba ni miongoni mwa watu ambao wanapata usaidizi wa upataji nafuu kituoni hapo huku akisisitiza kuwa,uraibu huwafanya watu wajiingize katika matatizo makubwa ikiwemo tabia mbaya na wakati mwingine huwafanya washindwe kumudu matumizi yao ya vilewesho.

Anaendelea kueleza kuwa,uraibu ndio unajumuisha tabia mbaya na mienendo isiyofaa, hivyo akifika katika kituo hicho mtu hubadilishwa tabia yake, mwenendo, fikra, hisia ili arudi katika hali nzuri kama awali kabla hajajiingiza katika matumizi ya vilewesho hivyo.

"Watu wengi wanadhani tatizo ni kilewesho, kumbe tatizo sio kilewesho bali ni 'addiction', kwa hiyo tunatibu uraibu kwa kubadili tabia, mwenendo, fikra na hisia kwani ukidhibitiwa mtu atakuwa na tabia nzuri, mwenendo mzuri.

"Mimi nina miaka sita tangu nimeacha kutumia dawa za kulevya,sio kwamba hisia za kutumia hazinijii, zinanijia lakini huwa ninazishinda kwa kudhibiti hisia.

"Kulingana na elimu niliyopata na masomo ambayo nilishafundishwa kukabiliana na hali hii lazima nizingatie pia taratibu zote, kwa vile hii ni shule ya upataji nafuu ili mtu atoke huko lazima ajizatiti kama shule nyingine, anayefaulu ni yule anayezingatia wengine tunawapokea wakiwa na pingu, wengine kwa hiari yao, lakini anayekuja na pingu anapopona hufurahi sana,"amesema Bw.Twaha.

Ombi

Aidha, Bw.Twaha ameiomba Serikali kuendelea kuijengea uwezo Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) ili iweze kuyafikia maeneo yote kuanzia nchi kavu, baharini, angani iweze kudhibiti dawa hizo zisiweze kuingia hapa nchini.

"Tukifanikisha kuyadhibiti haya madawa (dawa) yasiingia kabisa nchini, tutakuwa tumefanikisha ushindi mkubwa wa vita ngumu na hatari, na hayo yanaweza kufanikiwa kwa sisi wananchi pia kuunganisha nguvu ya pamoja, tushirikiane na Serikali kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini ili wazungu (wauzaji), watumiaji waweze kukomeshwa, hii vita ni rahisi iwapo tutashirikiana wakati wote,"anasema Bw.Twaha.

Pia ameiomba DCEA kuangalia namna ambavyo itazifikia nyumba zote za upataji nafuu ambazo ni changa kama hiyo anayoiendesha ili kuangalia namna ya kuwashauri waweze kufikia kundi kubwa zaidi la waraibu nchini.

"Na ninaamini Serikali imedhamiria kuziwezesha hizi nyumba kama ambavyo wataona mwongozo unaruhusu.Ni ombi langu tena kuwa, jamii iendelee kuunga mkono juhudi za Serikali za kuunga mkono mapambano ya dawa za kulevya ili jamii ya Watanzania iwe salama zaidi,"amesema Bw.Twaha.

Mwananyamala

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, Dkt. Zavery Benela amesema kuwa, Kliniki ya MAT Mwananyamala inahudumia wateja zaidi ya 1,350 kila siku ambao wanafika kunywa dawa.

Amesema, juhudi mbalimbali zimekuwa zikifanyika ikiwemo kuwaelimisha vijana wote wanaopatiwa huduma ili baada ya kupona waweze kushiriki zaidi katika shughuli za uzalishaji mali kwa manufaa yao, jamii na Taifa.

"Tumekuwa tukiwaelimisha vijana wote wanaopatiwa huduma hapa ili baada ya kupona waweze kushiriki zaidi katika shughuli za uzalishaji mali kwa manufaa yao, jamii na Taifa,"anasema Dkt.Benela.

Ustawi wa Jamii

Naye Afisa Ustawi wa Jamii anayesimamia kliniki hiyo, Hafsa Rashid Mtwange anasema kuwa, miongoni mwa vyanzo vikuu vinavyochangia vijana wengi kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya ni pamoja na makundi, hali ya maisha na ndoa.

Amesema, mara nyingi kila anapokutana na watumiaji wa dawa hizo ambao huwa wanafika katika kliniki hiyo kwa ajili ya kutafuta uponyaji wamekuwa wakizitaja sababu hizo.

"Peer groups (makundi), hii ni moja wapo ya sababu kubwa ambayo vijana wengi wanaofika hapa wamekuwa wakitaja kuwa ndiyo chanzo cha wao kujikuta wanatumia dawa za kulevya, wengine wamekuwa wakisema, hali ngumu ya maisha nayo imechangia wao kujikuta kujiingiza katika utumiaji wa dawa za kulevya na migogoro ya ndoa,"amesema Bi.Mtwange.

DCEA

Kamishina wa Kinga na Tiba wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Dkt. Peter Mfisi amesema kuwa, wameendelea kufikia kundi kubwa la waraibu wa dawa za kulevya nchini kwa kuhakikisha wanapata tiba saidizi kupitia vituo mbalimbali.

Dkt.Mfisi anasema kuwa, hadi Desemba mwaka jana zaidi ya waraibu 10,600 walikuwa wamehudumiwa kupitia vituo vya tiba saidizi kwa waraibu, vikubwa kwa vidogo vilivopo hapa nchini.

Amesema, kwa sasa wana vituo 15 ambapo kuna vinne vidogo huku 11 vikiwa vikubwa kwa ajili ya kutoa tiba saidizi kwa waraibu kwa kutumia dawa.

"Vituo hivi husimamiwa na Serikali na huhudumia waathirika wa dawa ya kulevya aina ya afyuni kama vile heroin na baadhi ya dawa tiba zenye asili ya kulevya.

"Waathirika wanaotibiwa kwenye vituo hivi hutibiwa kwa kutumia dawa mfano Methadone. Waathirika wanatakiwa kuhudhuria matibabu kila siku mpaka watakapomaliza matibabu. "Huduma ya MAT hutolewa bure chini ya uangalizi wa wataalamu,"amesema Dkt.Mfisi.

Amevitaja vituo hivyo kuwa ni Kliniki ya MAT Muhimbili iliyopo Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam,
Kliniki ya MAT Mwananyamala iliyopo Hospitali ya Mkoa ya Rufaa Mwananyamala jijini Dar es Salaam, Kliniki ya MAT Temeke iliyopo Hospitali ya Mkoa ya Rufaa Temeke jijini Dar es Salaam

Nyingine, Dkt.Mfisi anasema ni Kliniki ya MAT Mbeya iliyopo Hospitali ya Rufaa ya Kanda jijini Mbeya,Kliniki ya MAT Mwanza iliyopo Hospitali ya Mkoa ya Rufaa ya Sekou Toure jijini Mwanza, Kliniki ya MAT Itega iliyopo Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe jijini Dodoma

Pia amesema kuna, Kliniki ya MAT Bagamoyo iliyopo Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, Kliniki ya MAT Tanga iliyopo Hospitali ya Mkoa ya Rufaa ya Bombo jijini Tanga, Kliniki ya MAT Tumbi iliyopo Hospitali ya Rufaa yaMkoa ya Tumbi, Kibaha mkoani Pwani

Aidha, Dkt.Mfisi amesema kuwa, kuna Kliniki ya MAT Arusha iliyopo Hospitali ya Mkoa ya Rufaa yaMkoa, Mount Meru- Arusha jijini Arusha, Kliniki ya MAT Tunduma iliyopo Kituo cha Afya cha Tunduma mkoani Songwe, Kliniki ya MAT Segerea katika Kituo cha Afya cha Segerea jijini Dar es Salaam.

Dkt.Mfisi ametaja nyingine ni Kliniki ya MAT Tegeta iliyopo Kituo cha Afya cha Tegeta jijini Dar es Salaam, Kliniki ya MAT Mbagala iliyopo Zahanati ya Round Table-Mbagala jijini Dar es Salaam, Kliniki ya MAT Kigamboni iliyopo Hospitali ya Vijibweni-Kigamboni jijini Dar es Salaam

Amesema kuna faida nyingi za tiba ya methadone ikiwemo kundoa utegemezi wa dawa za kulevya aina ya heroine,kupunguza hatari ya mtegemezi kuwa katika hali ya kupata maambukizi ya HIV, homa ya ini na kifua kikuu.

Pia amesema, inaimarisha mwili na kumfanya mgonjwa kurudi katika hali yake ya kawaida na inaboresha mfumo wa mwili na kupunguza hatari za matumizi yasiyo sahihi ya dawa kwa kuzidisha kiwango ikiwemo kupunguza vifo vya ghafla.

Mtaalamu

Dkt.Miriam Kabanywanyi kutoka katika Kliniki ya MAT Mwananyamala anasema kuwa, wamekuwa na jukumu kubwa la kuwajenga kisaikolojia waraibu hao wa dawa za kulevya, kwani kila anayefika kituoni hapo ana changamoto zake kubwa ikiwa ni kuathirika kisaikolojia.

"Hivyo, tunatumia muda mwingi kuwajengea uwezo kwa kuwaandaa kisaikolojia ili waweze kuyakubali mazingira ya kupatiwa tiba na baada ya 'kugraduate' (kuhitimu) waweze kuwa watu mwema katika jamii na kushiriki kikamilifu katika maendeleo yao na jamii kwa ujumla,"amesema.

Wizara inasemaje

Hivi karibuni aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ambaye kwa sasa ni Waziri wa Maliasili na Utalii aliwataka waraibu wa dawa za kulevya kuendelea kutumia kliniki za MAT zilizopo katika maeneo mbalimbali nchini kupata dawa ili waweze kurejea katika hali ya kawaida kwa ajili ya kushiriki katika shughuli mbalimbali za ujenzi wa Taifa.

Mheshimiwa Waziri Balozi Dkt. Chana aliyasema hayo Machi 15, 2022 alipofanya ziara katika kituo cha kutolea huduma ya Methadone (MAT Clinic) kilichopo katika Hospitali ya Mkoa ya Rufaa Mwananyamala.

Alisema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa, vijana wote wakiwemo waraibu wanaopona wananufaika kupitia fursa mbalimbali ikiwemo kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotokana na mapato ya ndani ya halmashauri.

"Hata wale wenye changamoto, waraibu wanayo haki ya kujiunga katika vikundi wakapata fursa hii, na mikopo hii inatolewa pasipokuwa na riba ya aina yoyote. Hizi ni jitihada za Serikali yetu za kuwasaidia wanawake na vijana, hivyo fursa hizi zinatolewa katika vikundi, ni muhimu sana vijana wakajiunga katika vikundi, kwani umoja ni nguvu. Kikundi ndiyo dhamana ya kurudisha fedha hizo ili wengine wapate” amesema Dkt. Chana.

Pia alitoa wito kwa maofisa wa ustawi wa jamii kuwaunganisha waraibu na maafisa wanaoratibu utoaji wa mikopo kwa vijana na wanawake ili waweze kunufaika kupitia mikopo hiyo kwa ajili ya kwenda kuzalisha.

Nitapataje huduma

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA),zipo njia nyingi zilizothibitishwa kisayansi zinazoweza kutumika kuwatibu waathirika wa dawa za kulevya. Hapa nchini Tanzania njia zinazotumika zaidi ni tatu ambazo ni kupata matibabu kwenye vituo vya Methadone.

"Tiba hii hutolewa kwa waathirika wa dawa ya kulevya aina ya Heroin. Njia nyingine ni kupata matibabu kwenye nyumba maalumu za upataji nafuu (Sober House). Hii ni kwa waathirika wa dawa zote za kulevya na pombe.

"Pia njia nyingine ni kupata matibabu katika idara za magonjwa ya afya ya akili za hospitaliza rufaa za mikoa yote. Hii ni kwa waathirika wa dawa zote za kulevya pamoja na pombe,"anasema Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka DCEA, Bi.Florence Khambi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

2 Comments

  1. Kiukweli ubarikiwe sana Kwa makala nzuri sana inafundisha kweli

    ReplyDelete
    Replies
    1. MHARIRI DIRAMAKINIMay 2, 2022 at 8:43 PM

      Asante sana ndugu.
      Mhariri Diramakini

      Delete
Previous Post Next Post

International news