NA DIRAMAKINI
MKUU wa Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani, Sara Msafiri amesema kufuatia moto uliotokea kwenye Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkuza na kuteketeza bweni la wanafunzi wa shule hiyo wilaya kwa kushirikiana na wadau watahakikisha ndoto za wanafunzi hao hazitapotea kwa kutoa misaada ya hali na mali na kurejesha hali ya kawaida shuleni hapo.
Msafiri ameyasema hayo alipotembelea shule hiyo kukagua bweni lililoungua na kutoa msaada wa vitabu kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne.
Amesema kuwa, kutokana na moto huo kuteketeza bweni hilo ambalo lilikuwa na uwezo wa kulaza wanafunzi 76 ambao moto ulipowaka walikuwa wakijisomea madarasani.
"Wilaya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali tutahakikisha kila kitu kinarudi kuanzia miundombinu vifaa vyote pamoja na ukarabati wa miundombinu yote inarejeshwa ili wanafunzi waweze kurudia katika hali yao ya kawaida,"amesema Msafiri.
Aidha, amesema kuwa licha ya changamoto hiyo iliyowapata wanafunzi hao jukumu lao ni kusoma na kufaulu lakini masuala mengine wadau watahakikisha mahitaji yote yanapatikana.
"Nimetoa vitabu hivi ili kuhakikisha hamyumbi katika suala la masomo kwani nyie kama wasichana mnapaswa kusoma kwa bidii ili tupate viongozi mbalimbali mfuate nyayo za Rais wetu Samia Suluhu Hassan,"amesema Msafiri.
Ameongeza kuwa, anawapongeza wadau mbalimbali waliojitokeza kuisaidia shule hiyo baada ya kupata changamoto hiyo ya moto na kuwataka wadau zaidi wajitokeze kuisaidia ili irudie katika hali yake ya kawaida.
"Nashauri nyakati za usiku kuwe na utaratibu wa baadhi ya wanafunzi kusomea bweni wakati wengine wa wakiwa wanasomea madarasani ili iwe rahisi kugundua endapo moto utatokea ili kudhibiti,"amesema Msafiri.
Naye Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, John Sanga alisema kuwa kutokana na moto huo kutokea hakuna mwanafunzi aliyepata madhara zaidi ya hilo bweni kuungua na vifaa vya wanafunzi.
Sanga alisema kuwa, wameandaa safari za kimafunzo ikiwemo kwenda Makumbusho ya Taifa na sehemu nyingine kwa wanafunzi hao ili kuwarejesha katika hali ya kawaida ili kuwaondolea msongo wa mawazo.
Pia amesema wamewaandaa walimu wa Saikolojia ili kuwaondolea hali hiyo ya mawazo na wanawashukuru wadau kwa kutoa misaada ya hali na mali.
Naye Diwani wa Kata ya Mkuza, Focus Bundala alisema kuwa wanashukuru mkuu wa wilaya kutoa vitabu hivyo zaidi ya 100 vya aina tofauti tofauti.
Bundala alisema kwa mtu atakayeguswa anaweza kuendelea kutoa misaada mbalimbali ili iweze kusaidia wanafunzi hao.
Mwanafunzi Elista Thomas alisema wanawashukuru wadau kwa kuwapatia misaada mbalimbali tangu walipopata changamoto hiyo ya moto wanaahidi kusoma kwa bidii na kufanya vizuri kwenye mitihani yao.
Bweni hilo liliungua Mei 15,mwaka huu majira ya saa moja usiku wakati wanafunzi wanaolala kwenye bweni hilo wakiwa wanajisomea madarasani ambapo ina wanafunzi 190.