'Dream Team Explorers' kutoka Oman yaunga mkono juhudi za Rais Dkt.Mwinyi katika kuutangaza utalii

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameupongeza utayari wa Dream Team Explorers kutoka Oman kwa kuamua kuutangaza utalii wa Zanzibar.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Ikulu Zanzibar wakati alipokutana na ujumbe wa “Dream Team Explorers” kutoka Oman ambao umetumia usafiri wa gari kutoka nchini humo hadi Tanzania ukipita nchi kadhaa za Afrika na zile za Bara la Asia kwa lengo la kuutangaza utalii.

Katika mazungumzo hayo Rais Dk. Mwinyi aliukaribisha ujumbe huo hapa nchini na kueleza kwamba Zanzibar iko tayari kuwapokea watalii kutoka Oman hasa ikizingatia uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya pande mbili hizo.

Alisema kuwa, kwa vile Zanzibar inategemea sana utalii katika uchumi wake na kwa sehemu kubwa utalii uliopo ni utalii wa fukwe ambapo fursa nyingi zinapotea kwani upo utalii wa kufanya nje ya fukwe za bahari.

Hivyo, Rais Dkt. Mwinyi aliupongeza ujumbe wa timu hiyo kwa kuja na utalii wa aina hiyo ambao unaweza kufanyika na kuwa sehemu nyengine ya utalii nje ya utalii wa fukwe ambao umezoeleka hapa Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa Vijana wa “Dream Team Explorers” kutoka Nchini Oman ukingozwa na Ndg. Nassel Al-Salmi, walipofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar. (Picha na Ikulu).

Rais Dkt. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuushukuru ujumbe huo kwa utayari wao wa kufanya kazi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuongeza watalii kutoka Oman na kuahidi kushirikiana nao.

Alisema kuwa watu wengi wa Oman wanaokuja Zanzibar huja kwa ajili ya kuwatembelea ndugu na jamaa zao hivyo, hali hiyo ikibadilishwa na kuwa katika sehemu ya utalii makundi kadhaa kama hayo yatakuja kufanya utalii hapa nchini.

Aidha, alisema kuwa kwa wale wanaofanya kazi katika maeneo ya majangwa ambao hupata likizo mara kwa mara uwamuzi wa kuja kuitembelea Zanzibar utasaidia kwa kiasi kikubwa kuuimarisha utalii na kuufanya uwe ndani ya mwaka mzima kutokana na utalii wa Zanzibar kuwa wa miongo.

Rais Dk. Mwinyi alieleza imani yake kubwa kwamba baada ya timu hiyo kuja hapa nchini itasaidia kuutangaza utalii wa Zanzibar katika nchi ya Oman.

Rais Dk. Mwinyi alitoa shukurani kwa timu hiyo na kuahidi ushirikiano wa hali ya juu pamoja na kuwaondoshea changamoto iwapo zitatokea na kueleza kwamba Kamisheni ya Utalii nayo kwa upande wake itashirikiana vyema na timu hiyo katika kuutangaza utalii wa Zanzibar.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa hatua hiyo ya watu kutoka Oman na kuja kufanya Utalii Zanzibar kwa wale wenye ndugu na wale wasio na ndugu ni jambo la busara kwani litaongeza kasi ya kuutangaza utalii wa Zanzibar nchini Oman.

Mapema akitoa maelezo kiongozi wa “Dream Team Explorers” kutoka Oman Nasser Al Salmi alimueleza Rais Dk. Mwinyi jinsi ujumbe huo ulivyofarajika kwa kupata fursa ya kuonana na hatimae kuzungumza nae licha ya kuzungumza nae kwa mara ya kwanza kwa njia ya mtandao.

Nasser Al Salmi alieleza kwamba ujumbe huo tayari umeshazuru Tanzania Bara miaka ya nyuma na kuweza kutembelea mikoa kadhaa pamoja na sehemu za kitalii huku akitumia fursa hiyo kueleza kazi kubwa inayofanywa na timu hiyo ikiwa ni kutembelea maeneo ya utalii na kuyatangaza duniani.

Hivyo, alieleza kwamba kwa mwaka huu timu hiyo imeamua kufika Zanzibar baada ya kupita nchi kadhaa zikiwemo nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu, Saudi Arabia, Sudan, Ethiopia, Kenya, Uganda, Rwanda, Tanzania Bara hadi Zanzibar.

Kiongozi huyo wa “Dream Team Exlorers” kutoka Oman alimueleza Rais Dk. Mwinyi hatua watakazozichukua katika kuutangaza utalii wa Zanzibar hasa kwa wale Waomani wanaofanya kazi katika maeneo ya majangwa kwenye Kampuni za mafuta ambao huwa wanapata likizo za mara kwa mara kuja kuitembelea Zanzibar badala ya kutembelea maeneo mengine.

Alisisitiza kwamba hivi sasa kumezoeleka kwa Waomani walio wengi wanaokuja Zanzibar huja kwa ndugu na jamaa zao tu hivyo, mikakati maalum wataiweka katika kuhakikisha mbali ya kutembelea familia zao pia, wanafanya utalii.

Sambamba na hayo, kiongozi huyo aliwatoa hofu wale wote wanaotaka kuja kuitembelea Zanzibar na kueleza kwamba ni eneo salama lenye amani na utulivu mkubwa pamoja na vivutio kadhaa vya kitalii vilivyopo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news