NA FRESHA KINASA
SHIRIKA la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia lenye makao makuu yake Mugumu Wilaya ya Serengeti mkoani Mara limeratibu na kuwezesha (ufadhili) mafunzo maalumu kwa watu wa kuaminika 30 wanaotoa hifadhi kwa watoto wanaoishi mazingira magumu, yatima na waliotelekezwa kutoka Wilaya ya Serengeti, Bunda na Butiama ili waweze kufanya kazi hiyo kwa ufanisi.
Mafunzo hayo, yanafanyika Mjini Bunda kuanzia Mei 23, 2022 hadi Mei 25, 2022 ambapo wanafundishwa mambo mbalimbali ikiwemo elimu ya Ukatili wa Kijinsia, namna bora ya kutoa hifadhi kwa watoto, kukabili changamoto za watoto, haki na wajibu wa mtu wa kuaminika anapoishi na mtoto sambamba na kuweka mikakati ya pamoja ya ulinzi wa mtoto na malezi ndani ya miezi sita ambayo wanaruhusiwa kuishi nao.
Afisa Mwelimishaji Jamii Kutoka Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT), Emmanuel Goodluck amesema kuwa, kupitia mpango huo wa kuwapa elimu watu wa kuaminika watasaidia kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya vitendo vya ukatili wa Kijinsia, kutoa hifadhi bora kwa weledi.

Ameongeza kuwa, shirika hilo limejizatiti kuendeleza mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kushirikiana na serikali ikiwemo kuyajengea uwezo makundi mbalimbali Katika Jamii yasaidie Kupambana na vitendo vya ukatili wa Kijinsia sambamba na kutoa elimu kwa jamii katika mikutano ya hadhara, shule na makongamano. Huku akisisistiza Jamii kuwathamini Watoto wa kike kwa kuwawekea mazingira wezeshi yankufikia ndoto zao na kuwasomesha.


Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mara Elizabeth Mahinya amesema kuwa makao ya Watoto yamekuwa yakizidiwa hivyo kupitia watu wa kuaminika yatapunguza mzigo mkubwa. huku akisema Mkoa wa Mara matukio ya Ukatili wa Kijinsia bado yanaendelea ikiwemo kubwaka kwa Watoto, kupingwa kwa watoto, kulawitiwa.
Amesema Watu wa kuaminika ni daraja la kusaidia kumaliza ukatili wa Kijinsia na vitendo vingine vya ukatili wa Kijinsia ambavyo hufanyika Katika jamiii.

Aidha amesema, Mtu wa Kuaminika anazo haki ikiwemo kupata taarifa kamili za mtoto anayemhudumia, historia ya mtoto, historia ya elimu ya mtoto, kuwa na usiri, kushirikiana na Maafisa Ustawi wa Jamii kwa karibu, kutoa malezi kwa Watoto wanaowahudumia. Huku wajibu wao ikiwa ni kumuandaa mtoto vizuri kurudi kwa Wazazi wake, kutoa mrejesho kwa afisa Ustawi juu ya Maendeleo ya mtoto, kumlea mtoto kama Mwingine unayeishi naye, kutoa taarifa kwa Afisa Ustawi jamii pindi mtoto anapofariki.
Nao baadhi ya Washiriki wa mafunzo hayo, wamelipongeza Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania kupitia Mkurugenzi wake Rhobi Samwelly kwa kuwapa mafunzo hayo na wameomba lizidi kuungwa mkono na kupewa ushirikiano wa dhati lifanikishe kutekeleza majukumu yake.