NA FRESHA KINASA
JAMII imeshauriwa kujenga utaratibu wa kuwasaidia watoto wa kike kupata mahitaji yao ikiwemo kuwatengenezea mazingira wezeshi kusudi waweze kufikia malengo yao.

Kauli hiyo imetolewa Mei 28, 2022 na Emmanuel Goodluck ambaye ni Afisa Mwelimishaji Jamii kutoka Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia lenge makao makuu yake Mugumu wilayani Serengeti mkoani Mara wakati akizungimza na DIRAMAKINI.
Goodluck amesema,watoto wa kike wana nafasi kubwa ya kufanya mambo mengi ambayo yana tija katika jamii ikiwemo uzalishaji mali, kutoa malezi bora pamoja na kuchochea mabadiliko chanya katika jamii.Hivyo jamii ina wajibu wa kuhakikisha inawajali, kuwathamini na kuwapatia mahitani muhimu na kuwatia moyo wakati wote bila kuwakatisha tamaa.

Ameongeza kuwa, hivi sasa ni jambo la kushukuru na kupongeza kutokana na Rais Samia Hassan tangu aingie madarakani mchango wa viongozi mbalimbali wanawake wanaohudumu nafasi mbalimbali za uongozi serikalini unazidi kuonekana na tena wakifanya vizuri katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo na hivyo ameomba watoto wa kike waendelee kuwezeshwa kwa nguvu zote na usawa uwepo baina ya watoto wa kiume na wa kike hususani katika elimu na fursa mbalimbali.

"Rais Samia aliandaliwa vyema na kikamilifu na ndio maana hivi sasa tunaona matunda mazuri ya uongozi wake katika Taifa letu. Na pia akiwainua wanawake na kuwapa heshima nao pia wanadhihirisha uwezo wao tunawaona wakipiga kazi kwa uhakika lazima jamii tuendelee kuwaandaa zaidi na zaidi kimaadili na kielimu kusudi waje kuonesha uwezo wao katika kuliletea taifa maendeleo,"amesema Goodluck.

Sambamba na kuunda klabu za wanafunzi wapinga ukatili wa kijinsia ili kuweka mazingiara mazuri kwa Watoto wa kike kufika mbali zaidi akaomba juhudi za kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia pia zifanywe na kila mmoja ikiwemo kuwafichua wanaofanya vitendo hivyo mbele ya vyombo vya sheria kwa hatua kali.
Amesema, Shirika hilo pia linaendelea kutoa hifadhi kwa wasichana wanaokimbia vitendo vya ukatili wa Kijinsia ikiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni katika Kituo Cha Hope Mugumu Nyumba Salama na Nyumba Salama Butiama ambapo pia linawaendeleza kielimu na wengine katika vyuo vya ufundi kusudi wapate maarifa na ujuzi utakaowasaidia kujikwamua kiuchumi.