NA DIRAMAKINI
KATI ya mwaka 2001 hadi 2005 Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Diramakini Business Limited na Mhariri wa DIRAMAKINI, Bw.Godfrey Nnko alibahatika kuishi na kushirikiana na jamii ya wafugaji (Wamasai) huko Makiba katika Halmashauri ya Arumeru mkoani Arusha.
Kuishi huko, kushiriki shughuli za ufugaji, vyakula vyao kulimuwezesha kujifunza kwa kiasi kuhusu mila na desturi za jamii hiyo ambayo Mungu amewajalia roho ya huruma, upendo na umoja.
Aliweza kujifunza mambo mbalimbali, kubwa likiwa ni pamoja na sababu za mkuki kusimikwa nje ya mlango na mara nyingi mkono wa kuume.
Wengi wetu tumekuwa tukiaminishana au kujazana uongo kuwa, mkuki ule ukikuta umesimikwa nje hususani mwanaume wa boma husika anapaswa kutambua kuwa, ndani kuna mwanaume anayesaidia chakula cha usiku.
Dhana hiyo imekuwa ikienezwa siku baada ya siku, wengi wamekuwa wakiamini hivyo, lakini wenye mila zao wanatambua maana yake.
Ukweli ni kwamba, mkuki kusimikwa nje,kwanza kabisa ifahamike mkuki hutumiwa na vijana wa Kimasai wajulikanao kwa jina la Morani kwa ajili ya ulinzi.
Hao Morani ni walinzi wa mali kwa maana ya mifugo ya jamii yao, hivyo kitendo cha kusimika mkuki nje haina maana ya kumzuia mwenye nyumba kuingia ndani bali maana yake ni kwamba lolote linaweza kutokea mfano mifugo kuvamiwa na wanyama wakali.
Hivyo zoezi la ubebaji silaha kwa maana ya mkuki ni jepesi maana ipo sehemu ya wazi na inayoonekana. Kwa msingi huo ukikuta mkuki umesimikwa nje ondoa fikira potofu, kwani hata wewe unaweza kuutumia iwapo utabaini kuna wanyama au hali ya hatari dhidi ya mali za jamii.