IPRT yaja na mafunzo kuhusu mawasiliano ya kimkakati nchini

NA DIRAMAKINI

TASISI mpya ya Mahusiano na Mawasiliano ya Umma nchini Tanzania (IPRT) imetangaza hatua yake ya kutoa mafunzo kuhusu mawasiliano ya kimkakati (strategic communication and leadership) mahususi kwa watendaji wakuu, maofisa mawasiliano, maofisa utumishi pamoja na maafisa mbalimbali katika mashirika.
Mratibu wa mafunzo kutoka Taasisi ya Mahusiano na Mawasiliano ya Umma nchini Tanzania (IPRT) Bw Evarist Ngalimuwili akizungumza na waandishi wa habari pamoja na wageni waalikwa wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa mpango wa kutoa mafunzo kuhusu mawasiliano ya kimkakati mahususi kwa watendaji wakuu, maofisa mawasiliano pamoja na maafisa mbalimbali katika mashirika unaoratibiwa na taasisi hiyo kwa kushirikiana na taasisi nyingine za elimu ya juu kutoka ndani na nje ya nchi. Wengine ni pamoja na Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited, Bakari Machumu (Kulia) na Katibu Mtendaji wa Chemba ya Madini Tanzania (TCM) Mhandisi Benjamin Mchwampaka (Kushoto).

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa taasisi hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam mapema leo na kuhudhuriwa na wadau kutoka taasisi mbalimbali pamoja na vyombo vya habari, Mratibu wa mafunzo kutoka IPRT, Bw. Evarist Ngalimuwili alisema wazo la kuanzishwa kozi hiyo linachagizwa zaidi na uwepo wa changamoto katika eneo la mahusiano na mawasiliano ya umma kimkakati miongoni mwa taasisi mbalimbali hapa nchini.

Kwa mujibu wa Bw Ngalimuwili, katika kufanikisha mpango huo, taasisi hiyo imejipanga kushirikiana na taasisi mbalimbali zinazotambulika kwa weledi katika ufundishaji wa masuala hayo zikiwepo za ndani na nje ya nchi, sambamba na kutumia wahariri wabobevu kwenye masuala ya mawasiliano na mahusiano ya umma katika utoaji wa kozi hizo.

“Mpango huu utahisisha ushirikiano baina yetu na Chuo Kikuu cha Daystar cha nchini Kenya ambao ni wabobevu katika masuala haya na kwa kuanzia tunatarajia kuanza na kozi mahususi kwa watendaji wakuu wa mashirika na taasisi mbalimbali, maofisa mawasiliano na mahusiano ya umma, maofisa utumishi pamoja na maafisa mbalimbali katika mashirika hayo kisha baadae tutahusisha wanahabari kutoka makampuni ya habari, wakiwemo wanafunzi kutoka vyuo vikuu,’alisema Bw. Ngalimuwili.

Alizitaja kozi ambazo zitatolewa kuwa ni pamoja na programu za mawasiliano ya kimkakati kwa taasisi na mashirika kama vile Mawasiliano ya Biashara, mawasiliano wakati wa mgogoro (Crisis Communication), Usimamizi wa Chapa, Mawasiliano fanisi, Mawasiliano binafsi, mawasiliano ya kitaasisi sambamba na kozi nyingine zinazolenga kujenga ujuzi bora kwa wadau wa mawasiliano.

Aidha, ili kuhakikisha taarifa zinazohusu sekta mbalimbali za kitaaluma zinaripotiwa kwa weledi na utashi mkubwa, Bw Ngalimuwili alisema taasisi hiyo pia imeandaa mafunzo mahususi kwa wanahabari yakilenga kuwajengea uwezo katika kutoa taarifa zinazohusu nyanja hizo ikiwemo uchambuzi wa taarifa za fedha na taarifa za mahakama.

Nyingine ni habari za michezo na uchambuzi, taarifa zinazohusu sekta ya madini, mafuta na gesi, kilimo na mifugo, benki na bima, afya, ripoti za mazingira na Uchumi wa Bluu unaohusisha bahari, maziwa, mito, uvuvi, usafiri wa baharini na utalii.

"Lengo ni kuwajengea uwezo zaidi waandishi wa habari hapa nchini ili kuhakikisha habari zinazotolewa katika sekta mbalimbali zinaandaliwa kwa weledi wa hali ya juu na kwa usahihi” alisema huku akiongeza kuwa amefurahishwa kusikia mafunzo hayo ya msingi yataendeshwa kwa kushirikisha wataalamu na wakufunzi kutoka sekta husika.

Katika hatua nyingine inayolenga kuwezesha upatikanaji wa taarifa sahihi na za kuaminika katika maeneo ya Mahusiano na Mawasiliano ya Umma, Mawasiliano ya Kibiashara na Masoko pamoja na Uongozi na Utawala, Bw Ngalimuwili alisema taasisi hiyo pia imejipanga kutambulisha chapisho maalum linalotambulika kama Reputation Today litakalo kuwa pia na agenda kuu ya kuthibitisha weledi katika eneo la mawasiliano.
Katibu Mtendaji wa Chemba ya Madini Tanzania (TCM) Mhandisi Benjamin Mchwampaka (Kushoto) akizungumza na waandishi wa habari pamoja na wageni waalikwa wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa mpango wa kutoa mafunzo kuhusu mawasiliano ya kimkakati mahususi kwa watendaji wakuu, maofisa mawasiliano pamoja na maafisa mbalimbali katika mashirika unaoratibiwa na Taasisi ya Mahusiano na Mawasiliano ya Umma nchini Tanzania (IPRT) kwa kushirikiana na taasisi nyingine za elimu ya juu kutoka ndani na nje ya nchi. Wengine ni pamoja na Mratibu wa mafunzo hayo kutoka IPRT Bw Evarist Ngalimuwili (katikati) na Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited, Bakari Machumu (Kulia).

Akizungumzia hatua hiyo Katibu Mtendaji wa Chemba ya Madini Tanzania (TCM) Mhandisi Benjamin Mchwampaka alisema ujio wa mkakati huo umekuja katika kipindi ambacho taifa linahitaji kuwa na waandishi wabobevu katika maeneo mbalimbali ya kimkakati ikiwemo eneo la madini ili taarifa zinazotolewa ziwe na tija kwa wananchi.

“Tukiwa kama wadau wa sekta ya madini tumeguswa sana na ujio wa mafunzo haya si tu kwa ajili ya mawasiliano yetu sisi kama taasisi bali pia tunahitaji kuona waandishi wakipata mafunzo haya muhimu. Sekta ya madini inahusisha uwekezaji mkubwa hivyo hata aina ya uandaaji wa taarifa zake unahitaji umakini na weledi mkubwa. Uwepo wa waandishi waliofundishwa vema kuripoti habari za madini utatusaidia sana kama taifa,’’alisema.
Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited, Bakari Machumu (Kulia) akizungumza na waandishi wa habari pamoja na wageni waalikwa wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa mpango wa kutoa mafunzo kuhusu mawasiliano ya kimkakati mahususi kwa watendaji wakuu, maofisa mawasiliano pamoja na maafisa mbalimbali katika mashirika unaoratibiwa na Taasisi ya Mahusiano na Mawasiliano ya Umma nchini Tanzania (IPRT) kwa kushirikiana na taasisi nyingine za elimu ya juu kutoka ndani na nje ya nchi. Wengine ni pamoja na Mratibu wa mafunzo hayo kutoka IPRT Bw Evarist Ngalimuwili (katikati) na Katibu Mtendaji wa Chemba ya Madini Tanzania (TCM) Mhandisi Benjamin Mchwampaka (Kushoto).

Akizungumzia hatua hiyo, Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited, Bakari Machumu alisema ni muhimu kwa wanahabari wote kuendelea kujifunza ili kujijenga taaluma kwa maisha yao yote ya kuhudumu sekta hiyo sambamba na kubuni mbinu mpya za kuendesha mambo katika tasnia hiyo inayokwenda kwa kasi huku ikipokea mabadiliko mapya kila siku.

"Mambo mengi yanabadilika katika tasnia yetu hivyo kuna haja ya kujifunza na kupanua uwezo wetu na kuwa na uelewa mpana kila wakati," Bw.Machumu alisema.

Alisema mpango huo utakuwa sehemu muhimu katika kukuza na kuendeleza sekta ya mawasiliano nchini na juhudi za kudumisha tasnia hiyo;

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news