Kamati ya Bunge yaiomba Serikali kuwekeza fedha za kutosha kuendeleza bunifu

NA MWANDISHI WETU

MAKAMU Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge na Huduma za Maendeleo ya Jamii, Mhe. Aloyce Kamamba ameiomba Serikali kuwekeza fedha za kutosha katika kuendeleza bunifu zinazozalishwa nchini ili ziweze kujibu changamoto zilizopo kwenye jamii.
Mhe. Kamamba amesema hayo Jijini Dodoma alipotembelea maonesho ya Wiki ya Ubunifu ambayo Kitaifa yamefanyika katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma kuanzia Mei 16 - 20, 2022.

Amesema, kwa kuwekeza fedha hizo pamoja na kwamba zitatumika kuendeleza bunifu zilizoiva pia zitasaidia kuibua wabunifu wachanga kuanzia ngazi za vijiji, shule za Msingi pamoja na zile za Sekondari.
“Sisi kama Kamati ya Bunge tunafarijika kuona vijana wa Kitanzania, wabunifu kutoka sehemu mbalimbali wamepitia katika mchakato wa kushindanisha bunifu zao na hatimaye kushiriki mashindano kitaifa. Kwa kweli tunaishukuru na kuipongeza Wizara ya Elimu kwa kuandaa na kufanikisha maonesho haya ambayo yanaibua vijana wengi wenye uwezo,” amesema Mhe. Kamamba.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojiaa Mhe. Omari Kipanga (Mb) amesema mashindano ya mwaka huu yamekuwa na mwitikio mkubwa wa wabunifu na kwamba mpaka sasa bunifu 26 zimeendelezwa na Serikali huku nyingine zaidi ya 200 zikiwa zinaatamiwa.
“Mnaweza kuona dira, nia na dhamira ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuhakikisha pamoja na mambo mengine vijana wanafundishwa ujuzi zaidi kuliko nadharia; eneo la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu sasa ndilo pia litatufikisha katika azma hiyo,” amesema Mhe. Kipanga.
Ametumia fursa hiyo kushukuru wabunifu kwa kujitokeza kwa wingi, wafadhili, wananchi pamoja na vyombo vya habari kwa kutangaza vyema Wiki ya Ubunifu kwa mwaka 2022 pamoja na bunifu zao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news