KATIBU MKUU WA WIZARA YA MADINI AFUNGA JUKWAA LA KWANZA LA UTEKELEZAJI WA USHIRIKISHWAJI WA WATANZANIA KATIKA SEKTA YA MADINI JIJINI MWANZA

NA MWANDISHI WETU

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Madini, Adolf Ndunguru tarehe 22 Mei, 2022 amefunga Jukwaa la Kwanza la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania Katika Sekta ya Madini lililoanza tangu tarehe 20 Mei 2022 jijini Mwanza.
Jukwaa hilo lililoambatana na maonesho lilishirikisha wadau wa madini wakiwa ni pamoja na wachimbaji wa madini, watoa huduma kwenye shughuli za uchimbaji wa madini, mabenki, na watendaji kutoka Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Madini.

Akizungumza kwenye ufungaji wa jukwaa hilo Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adolf Ndunguru amesema kuwa Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini imeandaa jukwaa kwa lengo la kuhakikisha watanzania wanabaini fursa zilizopo na kushiriki kikamilifu kwenye Sekta ya Madini.

Amesema kuwa Wizara ya Madini itaendelea kuhakikisha watanzania wananufaika na Sekta ya Madini kupitia ushirikishwaji wa watanzania katika sekta ya madini pamoja na kutatua changamoto mbalimbali.

Aidha, amewataka wadau wa madini kushiriki katika zoezi la sensa linalotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu ili kuiwezesha Serikali kuweka mipango mbalimbali ya maendeleo.

Wakati huohuo,Ndunguru ametoa tuzo na vyeti kwa wadhamini wa Jukwaa hilo wakiwa ni pamoja na Equity Bank (Tanzania) Limited, CMS (Tanzania) Limited, Twiga Minerals Corporation Limited na BR Drilling Limited.

Wengine ni pamoja na Tansec Limited, Boart Longyear (Tanzania) Limited, Geita Gold Mining Limited, Williamson Diamonds Limited, Tembo Nickel Corporation Limited, BG Umoja Services Limited, Epsom Limited, African Assay Laboratories, Tanga Cement Limited, Shanta Mining Co. Limited na SGA Guards Tanzania Limited.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Kamishna wa Tume ya Madini, Janet Reuben Lekashingo sambamba na kushukuru kwa ushirikiano mkubwa unaotolewa na Wizara ya Madini kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini amewataka wananchi kuchangamkia fursa zilizopo kwenye Sekta ya Madini.

Naye Kamishna wa Madini, Dkt. Abdulrahman Mwanga amesema kuwa jukwaa limewapa mwanga wadau wengi wa madini kuhusu dhana nzima ya ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini.

Aidha amesema kuwa jukwaa hilo limetumika kama njia mojawapo ya kujadili namna ya kuzitatua changamoto mbalimbali zinazoikumba Sekta ya Madini hususan kwenye eneo la ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Kanali Dennis Mwila akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel ameipongeza Tume ya Madini kwa kuandaa jukwaa la kizalendo lenye lengo la kuhakikisha watanzania wanafahamu namna wanavyoweza kushiriki kwenye Sekta ya madini kupitia utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini.

Aidha, amewataka washiriki wa jukwaa hilo kuwa wazalendo kwenye utekelezaji wa shughuli zao na kupata fursa zaidi kwenye migodi ya madini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news