NA MWALIMU MEIJO LAIZER
NI wazi kuwa, nyongeza ya mshahara ya watumishi wa umma imegusa maisha ya watanzania wote, kwani ni takribani miaka saba sasa watumishi wameishi katika maisha magumu na ya kizalendo zaidi.
Pamoja na kuishi katika mazingira hayo, uwajibikaji wao umeendelea kuwa mkubwa kwa ujenzi wa nchi yao.
Miaka yote hii watumishi hawa wamekubali kufanya kazi ya utumishi wa umma bila kufanya maandamano na bila kugomea majukumu yao ya kiiutumishi.
Nyongeza ya mshahara kwa watumishi wa umma nchini Tanzania imekua gumzo kila kona ya Afrika Mashariki na Afrika ya kati, nchini Kenya nyongeza ya mshahara ni 12%, nchi zingine zipo chini ya 23.3% iliyoongezwa na Serikali ya Tanzania kwa watumishi wake hongera rais.
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan imefanya maamuzi magumu na yenye tija kwa watumishi wa umma na kwa watanzania wanaotegemea kile wanachokipata watumishi wa umma katika ujira wao, hii ni kwa sababu watumishi wa umma wanatumika kama daraja kufikisha fedha kwa watu wasio na ajira rasmi kwa kufanya manunuzi ya bidhaa mbalimbali jambo linalosababisha mzunguko wa fedha kirahisi.
Ni ukweli usiyofichika kuwa mishahara ya watumishi haishi kwenye mikono yao tu, bali inawezekana kufika katika maeneo yafuatayo.
Mosi, inachangia pato la taifa kupitia makato ya kodi kwa maendeleo ya nchi yetu. Pili, kupitia kodi inasaidia kuchangia maendeleo katika ujenzi wa shule, vituo vya afya, barabara vijijini na kadhalika.
Tatu, inasaidia kushiriki katika masuala ya kijamii kama vile harusi/ndoa, katika huduma ya Afya kwa wenye mahitaji maalum kama tunavyofahamu kwamba, kupitia bima ya afya mtumishi anayo haki ya kuweka wategemezi ili kupata huduma za matibabu maana yake kadili mshahara unavyopanda ndivyo asilimia za makato zinavyoongezeka na kuongeza kiwango cha huduma pia.
Nne, mishahara hii inatumika pia katika kuendeleza huduma za kiroho kwani wengine wanashiriki katika ujenzi wa misikiti na makanisa. 23.3% hii inafanya mzunguko wa fedha ndani ya nchi kuwa mkubwa na kuweza kuimarisha uchumi wa nchi kuwa imara zaidi.
Ongezeko hili litaongeza ajira mtaani kwani nidhahiri kuwa watumishi wa umma wanajishughulisha na shughuli mbalimbali za maendeleo katika biashara, kilimo na shughuli za ujenzi.
Kutokana na ongezeko hili katika mishahara, ni dhahiri kuwa watumishi wa umma wana deni kubwa kwa Mh.Rais, serikali yake pamoja na umma wa watanzania kwa ujumla, ili kutimiza malengo ya matamanio ya serikali ya awamu ya sita.
Hivyo ni vema kila mmoja wetu aweze kutimiza wajibu wake katika kufanya kazi kwa vitendo, ubunifu, uzalendo, ufanisi mkubwa na wa hali ya juu ili kujenga taifa imara zaidi katika kuimarisha uchumi wa taifa letu.
Sote kama watumishi wa umma ni jambo jema kutafsiri zaidi maono ya Mh.Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kufanya kazi usiku na mchana ili nchi iweze kusonga mbele kwa kuwa na uchumi endelevu.
Kuhudumia wananchi vizuri na kwa wakati katika maeneo yetu ya utoaji wa huduma za kijamii katika maeneo ya Hospitali zetu, kuanzia ngazi ya chini hadi ya kitaifa hasa kwa kutumia lugha nzuri kuachana na lugha za kejeli, chuki na udhalilishaji wa kijinsia.
Katika taifa lolote watumishi wa umma ni daraja kubwa kati ya Serikali na wananchi, hasa katika masuala ya kuleta maendeleo kwa wananchi.
Watumishi ni watafsiri wa sera za maendeleo katika nchi na zaidi ndio wasimamizi na watekelizaji wa ilani ya chama kinachoongoza jambo ambalo sote tuna wajibu wa kufanya kazi kwa ujasiri na utii mkubwa kwa masilahi mapana ya taifa letu.
Kama alivyowahi kusema Mzee Ally Hassan Mwinyi, Rais wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwamba “Kila zama na kitabu chake”.
Rais Samia ameandika kitabu chake kwani watumishi wa umma kila kona ya nchi wamejawa na furaha na matumaini makubwa kwa ongezeko la mshahara wa 23.3%. Wote wanasema mama kaupiga mwingi, wengine wanasema mama ana upendo wa dhati kwa watanzania, na kwamba ni mlezi namba moja kwa taifa lake.
Sote kama watumishi wa umma, tuna kila sababu ya kutumikia nchi yetu kwa moyo wote katika kuwajibika kikamilifu. Tukatae dhuluma, uonevu, rushwa na ufisadi katika maeneo ya kazi kwaajili ya masilahi mapana ya maendeleo ya Taifa letu la Tanzania. Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania.
Imeripotiwa Na:-
Mwl. Meijo laizer
MNEC Mstaafu
Wilaya ya Siha
Mkoani Kilimanjaro
0755898037