"Na kuna wakati,Rais wa Uganda, Yoweri Museveni alisema Tanzania ndio bima yao pale inapotokea shida katika mataifa yao,"amesema.
Naye Mshairi wa kisasa, Bw.Lwaga Mwambande kupitia kalamu yake anaendelea kukujuza mambo mengi mazuri yamhusuyo Hayati Baba wa Taifa kwa njia ya mashairi, ikiwa sehemu ya kwanza ya shairi hili ulijifunza jambo,SOMA HAPA
Endelea shemu ya pili hapa chini, Tanzania ni Bima Tosha;
1:Wasomi watukumbusha, Nyerere wa Tanzania,
Alivyotuimarisha, na kujenga Tanzania,
Wengi alishirikisha, si kwamba twawasagia,
Kumbukizi ya Mwalimu, hiyo ya vizazi vyote.
2:Amani tunadumisha, hapa kwetu Tanzania,
Inatutofautisha, nchi zatuzungukia,
Vurugu wavurumisha, hali twasikitikia,
Kumbukizi ya Mwalimu, hiyo ya vizazi vyote.
2:Museveni hakubisha, aonavyo Tanzania,
Kwamba ni bima yatosha, choko zinapoingia,
Hapa wajisalimisha, amani ya Tanzania,
Kumbukizi ya Mwalimu, hiyo ya vizazi vyote.
Vita kuwafurumusha, majirani Tanzania,
Kuyaokoa maisha, usalama Tanzania,
Kumbukizi ya Mwalimu, hiyo ya vizazi vyote.
4:Kile alifurahisha, Nyerere wa Tanzania,
Litaka kutufikisha, kuwa huru Tanzania,
Kusiwe wa kututisha, uchumi wa Tanzania,
Kumbukizi ya Mwalimu, hiyo ya vizazi vyote.
5:Kujitegemea bisha, kama siyo nzuri nia,
Ambayo ngesababisha, hakuna kuingilia,
Vile tunavyozalisha, ndivyo tungevitumia,
Kumbukizi ya Mwalimu, hiyo ya vizazi vyote.
6:Kwa kweli alikiwasha, Azimio kuingia,
Mali alitaifisha, ziwe zetu Tanzania,
Japo hakutufikisha, yake tuliona nia,
Kumbukizi ya Mwalimu, hiyo ya vizazi vyote.
7:Miiko alianzisha, viongozi Tanzania,
Wasije jimilikisha, mali za Watanzania,
Hizo pia lifundisha, kotekote Tanzania,
Kumbukizi ya Mwalimu, hiyo ya vizazi vyote.
8:Wala rushwa liwarusha, mbali wende jifilia,
Alisema imetosha, kuongoza kaishia,
Somo alitufundisha, cheo si kung’ang’ania,
Kumbukizi ya Mwalimu, hiyo ya vizazi vyote.
9:Wengi alitusomesha, shule kote Tanzania,
Bila ada kufupisha, kile ninakuambia,
Tungeshindwa jisomesha, tubaki twalialia,
Kumbukizi ya Mwalimu, hiyo ya vizazi vyote.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602