NA FRESHA KINASA
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mheshimiwa Innocent Bashungwa amesema fedha zinazotolewa na Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo maeneo mbalimbali nchini hazipaswi kukaa kwenye akaunti za halmashauri bila kufanyiwa kazi na badala yake zitumike kutekeleza miradi iliyokusudiwa kwa manufaa ya wananchi kwa wakati.
Mheshimiwa Bashungwa ameyasema hayo leo Mei 7, 2022 wakati akikagua mradi wa ujenzi wa makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na Ujenzi wa Hospitali ya Halshauri ya Wilaya ya Musoma katika kata ya Suguti Wilaya ya Musoma Mkoa wa Mara.
Amesema, fedha zinazotolewa zinalenga kutekeleza miradi ili kuwanufaisha Wananchi wapate huduma bora na hivyo hazipaswi kuendelea kukaa kwenye akaunti au kukawia kutekeleza mradi husika kwani kunachelewesha wananchi kupata huduma kwa wakati.
Akiwa katika eneo la ujenzi wa makao makuu ya Halmashauri hiyo ambapo ujenzi wake ulianza mwaka 2019, Waziri Bashungwa ameomba kasi iongezeke katika ujenzi wa makao makuu kwani fedha zaidi ya Shilingi Bilioni 2 zimekwishatolewa na serikali. Hivyo lazima ujenzi huo uendelee kwa haraka.
Huku akimtaka Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Hapi kuzitumia kamati zilizotumika kaharakisha ujenzi wa vyumba vya UVIKO-19 zisaidie kuharakisha mradi huo.
Akiwa katika ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ambapo amekagua ujenzi huo ambao majengo yake yamefikia asilimia 81 na fedha zaidi ya Bil. 3 zimetolewa kwa ajili ya mradi huo, Waziri Bashungwa ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Mara kufanya uchunguzi wa kina kujua gharama halisi za mradi huo kwani kuna harufu ya ubadhirifu wa fedha za mradi huo.
"Nimuagize Katibu Mkuu (TAMISEMI) na yeye alete timu yake kutoka juu haraka iwezekanavyo kusudi ije kuchunguza ujenzi wa mradi wa Hospitali kubaini waliohusika na ufujaji wa fedha za mradi huo ili wachukuliwe hatua kali za kisheria. mheshimiwa Mkuu wa Mkoa nakuongezea nguvu katika uchunguzi wa mradi huo." amesema Waziri Bashungwa.
Akizungumza katika mkutano na Wananchi wa Kata ya Suguti Waziri Bashungwa amewahakikishia Wananchi hao na Watanzania kwa ujimla kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Hassan itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo inayogusa maisha ya Wananchi maeneo mbalimbali hivyo wazidi kumuombea Rais na kumuunga mkono kufanikisha dhamira yake njema.
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Hapi,amesema amekwisha chukua hatua kadhaa ikiwemo kumsimamisha aliyekuwa Afisa Manunuzi wa Halmashauri hiyo kufuatia kushindwa kutimiza wajibu wake kwa ufanisi.
Mheshimiwa Hapi amesema kuwa, atahakikisha anasimamia kwa ufanisi maelekezo ya Waziri Bashungwa Katika kuhakikisha miradi hiyo na miradi mingine ya Maendeleo Mkoani Mara inatekelezeka kwa haraka na kwa ufanisi.
Awali Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Mheshimiwa Prof. Sospeter Muhongo amesema kuwa, miradi hiyo kuchelewa kutekelezeka ndani ya jimbo hilo kunatokana na Viongozi kutowajibika kikamilifu na kushindwa kutambua kwamba wanawajibu wa kuwatumikia wananchi.
Aidha, Prof. Muhongo amesema kuwa katika ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Musoma wapo baadhi ya Viongozi wamehusika kufanya ubadhirifu kutumia fedha hizo kwa manufaa yao hivyo hatua ya TAKUKURU kupewa jukumu la kuchunguza mradi huo na Waziri Bashungwa kuagiza katibu Mkuu alete timu kuongeza nguvu kufanya uchunguzi ni jambo la faraja.
"Wapo watu walikamatwa zaidi ya mara tatu na wengine wakiwa wameiba vigae, lakini hakuna hatua walizochukuliwa. Tunahitaji kuona thamani ya fedha iliyotolewa na Serikali ikileta tija kwani mradi huu baadhi ya watu wamekula fedha hivyo ni muhimu waliohusika wachukuliwe hatua za kisheria," amesema Prof. Muhongo.