NA IMMACUALATE MAKILIKA-MAELEZO
WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe.Nape Nnauye amewataka Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Serikali kuhuisha taarifa za Serikali kwenye tovuti za Serikali na mitando ya kijamii ili wananchi waweze kupata taarifa na kujua kinachoendelea kuhusu Serikali yao.
Waziri wa Habari ,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye akizungumza na Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini wakati akifungua kikao kazi cha 17 cha Maafisa hao kinachofanyika Jijini Tanga leo tarehe 9 Mei 2022.
Akizungumza leo jijini Tanga wakati akifungua Kikao cha 17 cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Serikali, Waziri Nape amesema kuwa Maafisa Habari wa Serikali ni daraja linalorahisisha mawasiliano kati ya Serikali na wananchi, hivyo ni muhimu kutimiza wajibu wao kwa kuwa na taarifa sahihi za Serikali na kwa wakati katika tovuti za Wizara au Taasisi zao.
“Natoa siku 14 kuanzia Mei 14 mwezi huu kila tovuti ya Serikali na mitandao ya kijamii iwe na taarifa za Serikali zinazoendana na wakati kuhusu utekelezaji wa Sera au miradi mbalimbali ya Serikali, Afisa atakayeshindwa kutekeleza hili tutaachana nae,”amesema Mheshimiwa Nape.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima akizungumza katika kikao kazi cha 17 cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kinachofanyika Jijini Tanga leo tarehe 9 Mei 2022.
Katika hatua nyingine, Waziri Nape ameahidi kutatua changamoto ya uhaba wa Maafisa Habari katika ngazi ya Wizara na Halmashauri ili kuhakikisha Serikali ina wataalamu wa kuisemea katika ngazi hizo.
“Nawaahidi hili liko ndani ya uwezo wangu la kusaidia kupata Maafisa habari katika mikoa ya Lindi, Manyara, Mbeya na Tabora na mikoa ya Dodoma, Kigoma na Geita mbayo Maafisa Habari wake wamekuwa Wasaidizi wa Wakuu wa Mikoa,"amesema.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa Kikao Kazi hicho kitandaa mkakati na kujifunza namna ambavyo dunia itahabarika kupitia Tanzania na kufikisha ujumbe wa maendeleo na namna ya watu kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Mwisho
Tags
Habari
Kikao na Waziri
Maofisa Habari wa Serikali
Sekta ya Habari na Mawasiliano
Tovuti za Serikali