NA DIRAMAKINI
CHAMA cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kinatarajia kufanya Uchaguzi Mkuu katika nafasi ya Rais, Makamu wa Rais na Mweka Hazina.
Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Mei 27, mwaka huu jijini Arusha, ambapo tayari kampeni za wagombea urais zimeanza tangu Aprili 15, mwaka huu na zinatarajiwa kuhitimishwa Mei 26, mwaka huu siku ambayo pia utafanyika uchaguzi katika nafasi nyingine ikiwemo ya viongozi wa kanda.

Uchaguzi huo ni kwa mujibu wa katiba ya chama hicho ambao hufanyika kila baada ya mwaka mmoja.
Miongoni mwa wagombea wa nafasi ya urais ni Profesa Edward Hoseah ambaye anawania nafasi hiyo kwa awamu ya pili.

"Katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wangu TLS imeweza kushauri zile sheria kandamizi kuondolewa au kurekebishwa ili kuimarisha misingi ya utoaji haki nchini kwa maslahi mapana ya wananchi na ustawi wa Taifa letu;


"Uongozi wa TLS kwa kushirikiana na Serikali tumeweza kupunguza gharama za bima ya Afya kwa Mawakili kutoka Milioni 1 hadi laki Tano;


"TLS imekuwa ikitoa msaada wa kisheria bure kwa Wananchi ambao hawana pesa ya kupata huduma ya kisheria, ili kuwawezesha wananchi kupata haki na stahili zao,"amefafanua kwa kina Prof.Hoseah.