NA MWANDISHI MAALUM
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi maafisa sita wa Jiji la Arusha akiwemo Mkurugenzi wa Jiji hilo, Dkt. John Pima kwa makosa ya matumizi mabaya ya fedha za Jiji na tuhuma za kughushi nyaraka.
Watumishi wengine waliosimamishwa kazi ni Mweka Hazina wa Jiji, Bi. Mariam Shaban Mshana; Bw. Innocent Maduhu (Mchumi), Bw. Alex Daniel Tlehama (Ofisi ya Mchumi,; Bw. Nuru Gana Saqwar (Ofisi ya Mchumi) na Bw. Joel Selemani Mtango, Afisa Manunuzi ambaye alihamishiwa Halmashauri ya Wilaya ya Longido.
Ametoa agizo hilo leo Mei 24, 2022, wakati akizungumza na viongozi na watumishi wa Jiji la Arusha na Halmashauri ya Wilaya ya Arusha kwenye ukumbi wa AICC jijini humo.
Amesema amefikia uamuzi huo kwa kuwa hawezi kuvumilia kuona fedha za umma zikitumika kinyume na taratibu. “ Mdhibit na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG ingia kazini mara moja, tafuta nyaraka zote na wakati huo watumishi hawa watakaa pembeni kupisha uchunguzi hadi kazi hiyo itakapokamilika,” amesema na kumuagiza Kamanda wa TAKUKURU wa Mkoa afuatilie masuala hayo hadi ijulikane ni akina nani waliohusika.
Alisema Mkurugenzi anatuhumiwa kwa kutosimamia ipasavyo utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo na watumishi, matumizi mabaya ya vifaa vya ujenzi wa miradi kutumika kwa ujenzi binafsi ambapo nondo, matofali, misumari, mbao, gypsum boards, saruji, mchanga, kokoto na bati vyenye thamani ya sh. milioni 44 viliagizwa kupitia kampuni ya Cherry General Supplies and Services na kupelekwa kwenye nyumba binafsi iliyoko Olkereyan, eneo la Njiro chini ya Usimamizi wa Bw. Joel Selemani Mtango.
“Tarehe 28 Machi, 2022 Mkurugenzi ulimwagiza Mweka Hazina aingize shilingi milioni 103 kwenye akaunti binafsi ya Innocent Maduhu iliyoko NMB zikiwa ni masurufu kwa ajili ya shughuli za kiwanda cha matofali. Ni kwa nini fedha ya kazi hii imeingizwa kwenye akaunti ya mtumishi binafsi badala ya akaunti za Kata?”alihoji Waziri Mkuu.
“Tarehe 14 Aprili, 2020 uliagiza sh. milioni 65 ziingizwe kwenye akaunti ya Alex Daniel ya benki ya NMB zikiwa ni malipo kwa ajili ya matenegenezo ya barabara za kata na mitaa. Tarehe hiyohiyo, sh. milioni 65 ziliingizwa kwa Bw. Nuru Ginana zikiwa ni malipo ya kununua vifurushi vya moramu. Hapa jumla ni shilingi milioni 233 ambazo hazikutumika kwa lengo lililokusudiwa,” amesema.
Mkurugenzi huyo pia anatuhumiwa kuhamisha watumishi 50 kati ya Januari na Mei mwaka huu. “Umefanya uhamisho wa watumishi usiokuwa halisia. Kuanzia Januari hadi Mei 2022, watumishi wapatao 45 wa kada mbalimbali wamehamishwa na wengine watano wamehamishwa mwezi huu wa tano kwa maombi yako.”
Amesema Mkurugenzi na timu yake, walimwomba mwenye kampuni ya Cherry General Supplies awape risiti ya sh. milioni 103 hali iliyosababisha adaiwe sh. milioni 15 na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) fedha ambazo hakuwa nazo na akatishiwa kushtakiwa.
Waziri Mkuu ambaye alikuwa mkoani Arusha kwa ziara ya siku moja na kukagua masoko ya Mbauda, Kilombero na Machame alibaini kuwa mabati yaliyotumika kwenye ujenzi wa vibanda vya wamachinga ni ya geji 30 wakati kanuni zinataka majengo yote ya Serikali yatumie mabati ya geji 28.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema timu nyingine za uchunguzi zilizokuwa zikifanya kazi kwenye suala hilo ziache mara moja na kuiacha timu maalumu ya uchunguzi ya CAG ifanye kazi yake. Timu hizo ni za PPRA na TAMISEMI.