Mashamba ya Tanzania Plantations Ltd yakabidhiwa wilaya za Arusha, Arumeru

NA MUNIR SHEMWETA-WANMM

SERIKALI imekabidhiwa mashamba yaliyokuwa yakimilikiwa na Kampuni ya Tanzania Plantations Ltd yenye ukubwa wa ekari 6,176.5 katika wilaya za Arusha na Arumeru mkoani Arusha na hivyo kumaliza mgogoro wa muda mrefu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Allan Kijazo (kulia ) akisaini hati ya makubaliano ya makabidhaino ya shamba kati ya serikali na Kampuni ya Tanzania Plantations Ltd wilayani Arumeru mkoani Arusha tarehe 29 Aprili, 2022.

Mgogoro kati ya Kampuni ya Tanzania Plantations Ltd na Serikali uliibuka mwaka 1999 baada ya kampuni hiyo kupinga ubatilisho wa mashamba yake uliofanywa na serikali kutokana na kampuni hiyo kushindwa kutimiza masharti ya umiliki jambo lililoifanya kufungua kesi Mahakama Kuu Kanda ya Arusha mwaka 2015.

Hata hivyo, katika kutafuta suluhu nje ya Mahakama Serikali kupitia Wakili Mkuu wa Serikali Mei 15, 2019 aliwasilisha ombi la kufanya majadiliano na mdai kwa lengo la kumaliza shauri nje ya mahakama ambapo Mahakama iliridhia pande mbili za shauri kumaliza suala hilo nje ya mahakama.

Makabidhiano ya mashamba hayo yaliyokuwa yakijulikana kama Karangai na Lucy Estate yanahitimisha mgogoro kati ya Serikali na Kampuni ya Tanzania Plantations Ltd sambamba na ule wa wananchi uliotokana na wananchi kuuziwa baadhi ya maeneo kwenye mashamba yaliyobatilishwa.

Katika makubaliano ya kutafuta suluhu nje ya mahakama, Serikali ilikubali kulipa shilingi bilioni 5.7 kwa ajili ya fidia ya mashamba Na 304 na 305 Nduruma yenye ukubwa wa ekari 6,133 na shamba la ekari 43.5 ambalo halikubatilishwa lakini ilionekana ni busara likachukuliwa na serikali. Pia serikali ililipa fidia ya mkonge na mtambo wa kuchakata mkonge uliokuwa ukifanya kazi.

Makabidhiano ya mashamba hayo yalifanyika Aprili 29, 2022 katika Kata ya Bwawani wilayani Arumeru mkoani Arusha baina ya Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dkt. Allan Kijazi na Mkurugenzi wa Tanzania Plantation Ltd, Bw. Ladhia Prabhudas Pradip mbele ya Waziri wa Ardhi, Dkt.Angeline Mabula.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Allan Kijazo (kulia) na Mkurugenzi wa Kampuni ya Tanzania Plantations Ltd wakionesha hati ya makubaliano ya makabidhiano ya mashamba ya Kampuni ya Tanzania Plantantions na Serikali wilayani Arumeru mkoani Arusha tarehe 29 Aprili, 2022.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mashamba hayo, Waziri wa Ardhi Dkt. Angeline Mabula alisema, Mheshimiwa Rais aliridhia makubaliano yafanyike na kutoa fedha kwa ajili ya fidia kumaliza mgogori huo uliodumu kwa muda mrefu.

"Tunamshukuru sana mhe Rais Samia Suluhu Hassan kwa sababu masuala haya yanahitaji hekima na busara na aliliona hili kuwa kuna uhitaji wa kuwa na mazungumzo na Tanzania Plantation Ltd, lakini pia akiangalia mustakabali wa watu waliokuwa eneo, tunamalizaje hili na kuelekeza makubaliano yafanyike na akatoa fedha na tayari mmiliki alishalipwa,"alisema Dkt.Mabula.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Angeline Mabula akikuzungumza wakati wa makabidhiano ya mashamba ya Tanzania Plantations Litd na Serikali wilayani Arumeru mkoani Arusha tarehe 29 Aprili 2022.

Kwa mujibu wa Dkt.Mabula, Serikali ya Mama Samia haiwezi kuwatelekeza wananchi waliokuwa wakiishi katika mashamba hayo na kubainisha kuwa itaweka utaratibu mzuri ili wananchi hao waweze kufaidika na matunda amabayo serikali imepanga.
Mmoja wa wananchi wa Kata ya Bwawani wilayani Arumeru mkoa wa Arusha akitoa ombi kwa serikali kuwafikiria kuwapatia maeneo wananchi wa eneo hilo wakati wa makabidhaino ya shamba kati ya serikali na Kampuni ya Tanzania Plantations Ltd wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Sehemu ya wananchi wa kata ya Bwawani wilaya ya Arumeru mkoa wa Arusha wakimsikiliza Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (hayupo pichani) wakati wa makabidhaino ya shamba kati ya serikali na Kampuni ya Tanzania Plantations Ltd wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikuzungumza na Mkurugenzi wa Kampuni ya Tanzania Plantations Ltd Bw. Ladhia Prabhudas Pradip mara baada ya kikao cha makabidhiano ya mashamba ya Tanzania Plantations Litd na Serikali wilayani Arumeru mkoani Arusha. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI).

Ametoa agizo kwa halmashauri ambazo ni mamlaka za upangaji nchini kuendelea kufanya tathmini kwa yale mashamba ambayo wamiliki wake wameshindwa kuyaendeleza au kuyatelekeza hatua za kuyatwaa uanze kufanyika mara moja.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Allan Kijazi alisema, wizara yake kwa kushirikiana na wizara na taasisi nyingine imeanza kuchukua hatua zitakazoiwezesha serikali kufanya maamuzi kuhusu matumizi ya mashamba hayo ikiwemo uvunaji wa mkonge kwa kuzingatia baadhi ya mahitaji ya wananchi.

"Serikali imeweka pia utaratibu wa ulinzi wa mashamba sambamba na mamlaka ya mkoa kusimamia mali kipindi hiki ambacho mpango wa matumizi ya ardhi unaandaliwa na niwatake wananchi kutoa ushirikiano,"alisema Dkt.Kijazi.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Tanzania Plantations Ltd Bw. Ladhia Prabhudas Pradip akikuzungumza wakati wa makabidhiano ya mashamba ya kampuni yake na Serikali wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Mkuu wa mkoa wa Arusha John Mongela akikuzungumza wakati wa makabidhiano ya mashamba ya Tanzania Plantations Litd na Serikali wilayani Arumeru mkoani Arusha.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela aliwatahadharisha wananchi wa eneo hilo kuwa eneo hilo sasa ni mali ya Serikali na wanachotakiwa ni kusubiri utaratibu wa matumizi ya mashamba hayo utakapowekwa.

"Asitokee mwananchi kufanya eneo hili kuwa shamba la bibi na mara kadhaa vinara namba moja katika kuanzisha migogoro ni viongozi hivyo niwatake viongozi wa vijiji na vitongoji msiwe madalali na tusije tukalaumiana, wajibu wa viongozi ni kusimamia wananchi na mali zao na kutaka wasianzishe migogoro,"alisema.

Naye Kamishna wa Ardhi nchini, Nathaniel Methew Nhonge alisema, baada ya makabidhiano ya shamba yaliyofanyika sasa ni lazina eneo hilo liandaliwe mpango wa matumizi ya ardhi kwa ajili ya manufaa ya nchi na kusisitiza kuwa zile changamoto zitakazojitokeza zitafanyiwa kazi na kutafutiwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news