Mganga Mkuu wa Serikali:Tudumishe ushirikiano katika kutokomeza UVIKO-19 nchini

NA DIRAMAKINI

MGANGA Mkuu wa Serikali, Dkt.Aifello Sichwale ametoa rai kudumishwa kwa juhudi za pamoja baina ya Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali katika kukabiliana na janga la UVIKO-19 nchini Tanzania.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mkutano huo ulioandaliwa na Shirika la My
Legacy na kufanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Jumanne Mei 17 hadi Ijumaa Mei 20,2022, Dkt. Sichwale amesema, licha ya ukweli kwamba watu wengi wamechoka kusikia kuhusu UVIKO-19, bado janga hilo lipo.

Amewataka Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari ili kupunguza kuenea kwa maambukizi ya UVIKO-19 mbali na kwamba jamii imeikubali na kuizoea hali hiyo mpya.
Dkt. Sichwale amesisitiza juu ya umuhimu wa ushirikiano wa wadau na kutumia mbinu za kiujumla badala ya kutegemea uwezo wa kiserikali na uongozi wa kisiasa pekee katika kukabiliana na janga la UVIKO-19.

"Lazima tukumbuke kuwa UVIKO-19 ni janga la kibinadamu ambalo linahitaji mshikamano wa sekta zote katika jamii. [Hata hivyo] Kulinda na kukuza ustawi wa afya ya binadamu haliwezi kuwa suala la Wizara ya Afya pekee. Inahitaji mshikamano wa jamii nzima kwani afya ikiwa hatarini, kila kitu huwa hatarini. Lakini afya ikilindwa na kukuzwa, watu binafsi, familia, jamii, uchumi, na mataifa yanaweza kusitawi,”alisema Dkt.Sichwale.

Sambamba na wito huo, Mganga Mkuu wa Serikali ilipongeza juhudi za wadau mbalimbali ikiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali kama vile My Legacy na Amref Tanzania ambao waliandaa hafla hiyo kwa kuunga mkono serikali katika kukomesha kuenea kwa janga UVIKO-19.

"Mashirika yasiyo ya kiserikali, sekta binafsi, na mtu mmoja mmoja wana jukumu la kutekeleza mikakati ya kupunguza idadi ya watu wanaopata ugonjwa wa UVIKO-19, vifo, na athari za kijamii na kiuchumi. Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa washirika kufanya kazi. Pia itaratibu juhudi za wadau kutoka sekta mbalimbali zikiwemo asasi za kiraia ambazo ni mshirika muhimu wa serikali,”aliongeza Dkt. Sichwale.
Bi. Fortunata Temu (katikati), Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la My Legacy akizungumza na washiriki wakati wa ufunguzi wa mkutano huo.

Bi. Fortunata Temu, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya My Legacy ambao ndiyo waandaaji wakuu wa mkutano huo amesema kwamba hatua hii imelenga kusaidia juhudi za serikali zinazofanywa na Wizara ya Afya katika mapambano ya kuzuia kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya korona nchini.

“Kwa siku za hivi karibuni, watu wengi wamejisahau kufuata hatua za kudhibiti na kujilinda na maambukizi ya UVIKO-19. Katika akili zetu tunapaswa kuelewa kuwa ugonjwa huu haujaisha na hivyo tunapaswa kuendelea kuishi nao ila kwa kuchukua tahadhari zote. Ugonjwa wa UVIKO-19 bado upo licha za juhudi mbalimbali za kukabiliana nao kuchukuliwa. My Legacy na washirika wetu kama AMREF Tanzania na Global Fund tumeamua kushirikiana ili kuunga mkono juhudi za serikali na wadau wengine kuhakikisha kuwa kila raia nchini anakuwa salama dhidi ya maambukizi ya virusi vya korona,” Bi. Fortunata Temu alinukuliwa.
Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt.Aifello Sichwale.

Jumla ya washiriki 100 kutoka makundi mbalimbali, wajumbe 50 kutoka kwenye Asasi za Kiraia, wajumbe 5 kutoka kwenye vyombo vya maamuzi na wajumbe 25 wakiwa ni watu wenye ushawishi ndani na nje ya mkoa wa Dar es salaam walijengewa uwezo kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu janga la UVIKO-19 ikijumuisha uelewa juu ya ugonjwa huo, mbinu za kukabiliana nao, na namna ya kupunguza athari zitokanazo na janga hilo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Serikali iliyotolewa na Wizara ya Afya, tangu mwezi Machi 2020, Tanzania ilipokumbwa na janga la UVIKO-19 mpaka mwezi Mei 2022, Tanzania imesajili jumla ya visa 33,916 vya korona huku vifo vikiwa 803. Pia, jumla ya watu 4,110,884 wamepata chanjo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news