NA HAPPINESS SHAYO-WMU
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amewaasa wananchi kuacha kudai kuruhusiwa kufanya shughuli za kibinadamu katika msitu wa Nusu Maili ambao ni tegemeo kubwa la ikolojia ya Mlima Kilimanjaro.
Ameyasema hayo hivi karibuni katika ziara ya Mawaziri wa Kisekta mkoani Kilimanjaro katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.
“Niwashauri wananchi tusiendelee kudai kumegewa nusu maili kwa kuwa kwa kufanya hivyo tutasababisha theluji iliyo katika Mlima Kilimanjaro kuyeyuya na hatimaye mlima utakwisha,”Mhe.Masanja amesisitiza.
Amewataka viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro kuwaelimisha wananchi juu ya sifa ya mlima huo ambao unatarajiwa kuongeza idadi ya watalii hasa kipindi hiki cha uhamasishaji wa Royal Tour.
Aidha, amesema eneo la Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA) awali lilikuwa chini ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na baadae kupandishwa hadhi kuwa hifadhi kitu ambacho kinaondoa sifa ya kuruhusu shughuli za kibinadamu.
Mhe. Masanja amewataka viongozi kushirikiana katika kurudisha uoto wa asili kwenye maeneo yaliyoharibiwa na pia kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kutovamia maeneo ya Hifadhi.