NA DIRAMAKINI
MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Njombe, Scolastika Kevela amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kupandisha mishahara ya wafanyakazi nchini na hivyo kumaliza kilio chao cha muda mrefu.
Bi.Kevela ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Udalali ya Yono Auction Mart, ametoa kauli hiyo mara baada ya taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu kusema kuwa, Rais Samia ameridhia mapendekezo ya mishahara ikiwemo kima cha chini kwa watumishi wa umma kwa asilimia 23.3.
Hatua hiyo ya Rais Samia ni utekelezaji wa ahadi aliyokuwa ameitoa wakati wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi Duniani ambapo pamoja na mambo mengine, aliahidi kuongeza kima cha mishahara kwa wafanyakazi jambo ambalo lilikuwa kilio chao kwa muda mrefu.
"Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa hili anastahili pongezi nyingi sana, amedhirisha wazi wazi kuwa yeye ni mama mwenye malezi mazuri na ujali kwa wanae, madai ya nyongeza ya mishahara ilikuwa kilio cha miaka mingi hapa nchini, kwetu sisi UWT Mkoa wa Njombe tunasema hana baya," amesema Mama Kevela.
Amesisitiza kuwa siyo jambo la kawaida kwa kiongozi aliyekaa madarakani Kwa kipindi cha mwaka mmoja na siku 56 kutekeleza takwa la ongezeko la kima cha mishahara wakati akiwa pia akiwa anaendeleza miradi mbalimbali mikubwa ikiwemo ya kimkakati.
Aidha, kupitia taarifa hiyo iliyotolewa na Ikulu, nyongeza hiyo ya mishahara imefanyika kwa kuzingatia Pato la Taifa (GDP), mapato ya ndani yanayotarajiwa kukusanywa mwaka 2022/2023 na Hali ya uchumi wa ndani na nje ya nchi.
Kutokana na hatua hiyo, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imepanga kutumia kiasi cha Sh Trilioni 9.7 kwa ajili ya kugharamia malipo ya mishahara ya watumishi wote katika Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Taasisi na Wakala za Serikali.
Hivyo kwa hatua hiyo bajeti ya Serikali ya Mwaka 2022/2023 ina ongezeko la Sh Trilioni 1.59 sawa na asilimia 19.51 ikilinganishwa na bajeti ya Mwaka 2021/2022
Aidha akizungumzia hilo, Mwenyekiti huyo wa UWT Mkoa wa Njombe alisema hatua hiyo ya Rais Samia ni utekelezaji kwa vitendo wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho pia Lila wakati kinampongeza kwa umakini wake katika kuitekeleza hiyo kikamilifu na kwamba siri kubwa ya mafanikio Kwa chama hicho.
Alisisitiza kwa kusema kuwa Chama Cha Mapinduzi siku zote kimekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha maslahi ya wananchi wake yanasimamiwa na kulindwa hatua iliyomfanya Rais Samia kuwa kiongozi bora kila kukicha