NA STEVEN NYAMITI-WM
NAIBU Waziri wa Madini, Dkt.Steven Kiruswa ameshuhudia utiaji saini mkataba kati ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Kampuni ya ABSA ambapo tani 60,000 zitauzwa kwa mwezi kwa wawekezaji hao.
Hafla hiyo ya utiaji saini mkataba kati ya STAMICO na mwekezaji wa makaa ya mawe Kampuni ya ABSA imefanyika leo Mei 10, 2022 jijini Dodoma. |
Dkt.Kiruswa amesema, STAMICO itakusanya mapato wastani wa shilingi bilioni 4.16 kwa mwezi sawa na wastani wa shilingi bilioni 50 kwa mwaka katika uwekezaji huo.
Pia, STAMICO itatoa ajira za moja kwa moja 600 na fursa nyingine za ajira kwa Watanzania katika mradi huo.
Amempongeza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt.Venance Mwasse na Menejimenti yake yote kwa maamuzi ya kukubaliana na Kampuni ya ABSA katika kufanya biashara nchini.
"Ni matumaini yangu kuwa makubaliano haya yaliyosainiwa yatakuwa na manufaa kwa pande zote mbili,"amesema Dkt.Kiruswa.
Akizunguzia mafanikio ya STAMICO, Dkt.Kiruswa amesema, katika kipindi cha Julai, 2021 hadi Machi 2022, katika mradi wa Kabulo, tani 17,324 za makaa ya mawe zilichimbwa ambapo tani 12,792 zenye thamani ya shilingi 1.2 ziliuzwa na kulipa serikalini shilingi 174,191,290.87 ikiwa ni mrabaha na ada ya ukaguzi.
Dkt. Kiruswa amempongeza Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelelea kuifungua nchi ili wawekezaji waweze kuja kuwekeza Tanzania."Niwahakikishie wawekezaji wetu wa makaa ya mawe kuwa Tanzania ni nchi salama, inayojali wawekezaji na inayozingatia sheria mbalimbali za nchi na kimataifa. Wizara itahakikisha pia inafuatilia mwenendo mzima wa mkataba huu ili kupata matokeo chanya kwa Shirika na Kampuni ya ABSA," amesema.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Venance Mwasse amesema, tukio hilo ni matokeo ya mkakati wa kuanza uchimbaji mkubwa wa makaa ya mawe.
Amesema, maandalizi yamekamilika katika ukarabati wa miundombinu ya barabara, daraja na mgodi wa chini ambapo uchimbaji umeanza.
Dkt.Mwasse amesema, STAMICO imesaini mkataba mkubwa wakihistoria ndani ambapo STAMICO itauza tani 60,000 kwa mwezi za makaa ya mawe.
"Mkataba huu ni wa kipindi cha miaka mitano, thamani ya mkataba huu ni dola za Marekani milioni 108 na zaidi, sawa na shilingi bilioni 250 za kitanzania kwa miaka mitano,"amesema Dkt.Mwasse.
Kwa upande wake Rais wa Kampuni ya ABSA, Bw.Gerges Schmickrath ameishukuru wizara kupitia STAMICO kwa kuaminiwa kuwekeza katika mradi wa makaa ya mawe. Amesema,mradi huo utakuwa na manufaa kwa watanzania kwa kuongeza pato la Taifa.
Hafla ya utiaji saini mkataba wa makaa ya mawe ya Mkoa wa Songwe katika mgodi wa Kabulo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Wizara ya Madini na Taasisi ya STAMICO.