NA DIRAMAKINI
SIKU moja
baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia
Suluhu Hassan kuridhia nyongeza ya mishahara ikiwemo kima cha chini kwa
watumishi wa umma kwa asilimia 23.3, wafanyabiashara na waendesha
bodaboda jijini Dar es Salaam wamepongeza hatua hiyo.

Hayo wameyasema kwa nyakati tofauti leo Mei 15,2022
wakati wakizungumza na DIRAMAKINI ambapo wamesema, hatua ya Rais Samia
kuridhia nyongeza ya mishahara kwa asilimia 23.3 kwa watumishi wa umma
inaonesha ni kiongozi mahiri anayethamini
Sambamba na kuheshimu juhudi zao
thabiti wanazozifanya katika kuchochea maendeleo, hatua ambayo pia
itaimarisha mzunguko wa shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazofanywa na
wananchi wa makundi mbalimbali.

"Hatua
ya Rais ni ya kupongezwa sana, jambo alililofanya ni zuri mno, sisi
tunategemea wafanyakazi wa Serikali, Serikali inapotoa mishahara kwa
wafanyakazi mzunguko wa fedha unaongezeka na biashara
zinachangamka,"amesema Charles.
Naye Abukabar Seif Shaban ambaye
ni mwendesha bodaboda katika Kituo cha Ubungo Mawasiliano amesema kuwa,
Rais amefanya jambo ambalo linapaswa kupongezwa kwani wafanyakazi wana
mchango mkubwa katika kuwezesha mzunguko wa fedha na hivyo kitendo cha
Rais Samia kuwaongezea mishahara kunawezesha neema kwa wananchi.
"Mfanyakazi
anaposhika fedha anakuwa na shughuli zake mbalimbali anazofanya,kwa
sababu hiyo anaweza kuhitaji bodaboda kutokana na ongezeko alilonalo.
Lakini mshahara ukiwa mdogo angeona gharama zimezidi kuwa kubwa na
asingechukua bodaboda angeweza kupanda daladala au angetembea kwa miguu,
hatua ya Rais ni nzuri sana,"amesema Shaban.