NA GODFREY NNKO
OFISI ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imefanya uchambuzi wa tathmini ya utendaji kazi kwa Wakuu wa Kitengo cha Fedha kwa kutumia tathmini iliyowasilishwa na Makatibu Tawala wa Mikoa sambamba na tathmini iliyofanywa na OR -TAMISEMI.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Mei 5,2022 na Bi.Nteghenjwa Hosseah ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Rais TAMISEMI
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tathmini hii imefanyika kwa kutumia vigezo vya ukusanyaji wa mapato ya ndani,upelekaji wa fedha za miradi ya maendeleo na matumizi ya fedha hizo kwenye miradi inayogusa wananchi.
Pia utoaji na usimamizi wa mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na watu wenye Ulemavu pamoja na ukusanyaji wa marejesho na matumizi ya fedha za marejesho.
Hivyo, kutokana na tathmini hiyo na ili kuboresha utendaji kazi katika kitengo hicho muhimu cha fedha, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mhe. Innocent Bashungwa amewabadilishia majukumu Wakuu wa kitengo hicho 16 na Wakuu wa Kitengo/Maafisa Waandamizi 109 wamehamishiwa katika vituo vipya vya kazi kati ya hao 16 wanakwenda kujaza nafasi zilizoachwa wazi.
Aidha,Wakuu wa Kitengo hicho ambao wamebadilishiwa majukumu, 72 wamebakizwa katika vituo vyao vya awali na 3 wamebakizwa katika vituo vyao vya awali na kupewa muda wa miezi 6 ya matazamio ili waweze kuboresha utendaji kazo wao.
Uhamisho uliofanyika umezingatia Barua yenye Kumb. Na.C/CB. 271/431/01/62 ya tarehe 8 Juni, 2006 ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora aliyokasimu madaraka kwa Katibu Mkuu OR – TAMISEMI.
Tathmini hii itaendelea kufanyika katika Idara na Vitengo vingine katika Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini ili kuboresha utendaji kazi wa Mamlaka hizo katika kuwahudumia wananchi.
Orodha ya watumishi wa Kitengo cha Fedha waliobadilishiwa majukumu, waliohamishwa kwenye vituo vipya na watumishi wa kitengo hiki ambao wanaendelea kuwepo kwenye vituo vyao vya awali ni kama ifuatavyo;