PANYA ROAD MWASIKIA? Zinazofuata nguvu, hakuna cha msalie

NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)

WAKATI Serikali kupitia Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ikiendelea na msako maalum dhidi ya vijana ambao wanajihusisha na vitendo vya uhalifu jijini Dar es Salaam ambao wamejipa jina la 'Panya Road', juhudi za pamoja miongoni mwa wanajamii zinahitajika ili kuwafichua wote wanaojihusisha na uhalifu huo, lengo likiwa ni kutokomeza kabisa tabia hizo na jamii iendelee kubaki salama.

Kila mmoja wetu anatambua wazi kuwa, kundi hilo ambalo lilibuka miaka kadhaa jijini Dar es Salaam ambapo vyombo vya ulinzi na usalama vilifanikiwa kulidhibiti, lakini kwa siku za karibuni limeibuka tena, limekuwa likitekeleza uhalifu wowote bila hofu.

Uhalifu huo umekuwa ukisababisha maumivu makubwa katika jamii, kwani mbali na kujeruhi watu pia huwa wanapora,wanaiba na kukaba watu katika maeneo mbalimbali.

Bw. Lwaga Mwambande (KiMPAB) ambaye ni mshairi wa kisasa ameendelea kutumia kalamu yake kuwapa elimu vijana hao ambao wanaishi miongoni mwa jamii zetu, huku akiwashauri kuachana na matendo hayo ambayo licha ya kuhatarisha usalama wao kutokana na mkono mkubwa wa Serikali na nguvu ya umma pia wanapeleka vilio kwa familia zao, hatua kwa hatua jifunze jambo kupitia shairi hapa chini;
 
1:Mwakalia kuti kavu, Panya Road msikie?
Mmeshapewa makavu, majumbani mtulie,
Vitendo vyenu vya nguvu, bora kwenu viishie,
Kwanini mfe mapema, au jela muishie?

2:Mwakalia kuti kavu, Panya Road tuwambie,
Kwa hizo tabia mbovu, mtuibieibie,
Zinazofuata nguvu, hakuna cha msalie,
Kwanini mfe mapema, au jela muishie?

3:Mwapata mali kwa nguvu, kwa visu mtuvamie,
Tena na macho makavu, na nyumba mtuvunjie,
Mwafanya tuwe na wivu, nanyi tuwafanyizie,
Kwanini mfe mapema, au jela muishie?

4:Mwatufanya wapumbavu, mali yetu mjilie,
Kufanya kazi wavivu, njiani mtuvizie,
Mbwaimbwai kavukavu, hadi nanyi mzimie,
Kwanini mfe mapema, au jela muishie?

5:Maisha ya ulegevu, ndiyo ya kwenu nyie,
Ingawa mnazo nguvu, za kwenda mtulimie,
Ni matumizi ya nguvu, eti mtufanyizie,
Kwanini mfe mapema, au jela muishie?

6:Mmeshapata makavu, ni bora muyasikie,
Huo wa kwenu utovu, wa nidhamu uishie,
Hivi zinategwa nyavu, nyote humo muingie,
Kwanini mfe mapema, au jela muishie?

7:Vijana mnazo nguvu, taifa litumikie,
Endapo siyo wavivu, kazi mbele jifanyie,
Hamtatoka kavu, shida zenu zisalie,
Kwanini mfe mapema, au jela muishie?

8:Uhalifu ni uchovu, jela isiwanukie,
Uchapakazi werevu, hadhi yenu isalie,
Tumechoka sasa nguvu, ikija iwaingie,
Kwanini mfe mapema, au jela muishie?

9:Vidonda hata makovu, kwanini mtupatie?
Wa kwetu uvumilivu, sasa bora uishie,
Tutumie zetu nguvu, mbaroni na tuwatie,
Kwanini mfe mapema, au jela muishie?

10:Vijana mnazo nguvu, mwovu asiwazidie,
Siwe kama sumu kuvu, mazao iharibie,
Wala mistake nguvu, hizo tuwaumizie,
Kwanini mfe mapema, au jela muishie?

Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news