NA MWANDISHI-WyEST
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda (Mb) amesema Chuo cha Ufundi Dodoma kinachojengwa eneo la Nala jijini Dodoma kinatarajia kukamilika mwezi Desemba 2022 na kuanza kudahili wanafunzi mwaka 2023.
Waziri Mkenda amesema hayo jijini Dodoma alipofanya ziara kukagua maendeleo ya ujenzi wa Chuo hicho ambacho amesema kukamilika kwa Chuo hicho kutafanya idadi ya Vyuo vya Ufundi hapa nchini kuwa vinne vikiwemo vya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST).
Amesema, chuo hicho kinajengwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza itagharimu Sh bilioni 17.9 na ujenzi ukikamilika kitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,500.
Waziri Mkenda amesema katika mageuzi ya elimu yanayofanyika hapa nchini kwa sasa Vyuo vya Ufundi vina nafasi kubwa ya kusaidia kupeleka nchi kwenye mageuzi hayo kwa kuwa mitaala mipya itakapoanza kutumika itajikita kwenye Ufundi na Ujuzi.
“Ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwamba mapitio ya Sera na Mitaala yatakapokamilika na elimu kutolewa kwa mitaala mipya kuhakikisha kunaongezeka mambo ya ufundi na ujuzi ili wahitimu waweze kujiajiri na kuajiriwa hivyo kukamilika kwa vyuo vya ufundi kutasaidia sio tu kutoa mafundi lakini pia watu watakaokwenda kufundisha ufundi,” amesema Prof. Mkenda.
Prof Mkenda ameongeza kuwa Wizara kwa sasa inaanza hatua za kutafuta watumishi ikiwemo wakufunzi kutoka ndani na nje ya nchi kwa ajili ya chuo hicho.
Kwa upande wake Mkurugenzi anayesimamia Elimu ya Ufundi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Noel Mbonde amesema Chuo hicho kitakapokamilika kitaanza kutoa fani za kipaumbele tatu ambazo ni nishati, vifaa tiba na ujenzi.
Msimamizi wa Mradi kutoka BICCO, mhandisi Aliki Nziku amemwambia Waziri Mkenda kuwa utekelezaji wa Mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Dodoma awamu ya kwanza kwa sasa umefikia asilimia 50 na ulianza Juni 2021 na unatarajia kukamilika Desemba 2022.