NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amepongeza juhudi zinazochukuliwa na uongozi wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA), katika kuhakikisha nchi wanachama zinashirikiana ipasavyo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza mgeni wake Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Barani Afrika.Mhe.Wamkele Mene (kulia kwa Rais) akiwa na ujumbe wake walipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu. (Picha na IKULU).
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Mei 20,2022 Ikulu jijini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA), Bwana Wamkele Mene.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi alisema kuwa, ana matumaini makubwa kwamba juhudi hizo zinazochukuliwa kwa makusudi zitasaidia kwa kiasi kikubwa kufikia lengo lililokusudiwa na nchi wanachama wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) katika kuimarisha uchumi na kuleta maendeleo endelevu.
Rais Dkt.Mwinyi alieleza jinsi alivyofurahishwa kwa kupata taarifa kwamba Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA), imetoa mazingatio maalum kwa nchi za visiwa ikiwemo Zanzibar.
Alisema kuwa, amefurahishwa na mafanikio yanayoendelea kupatikana katika Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA), ambapo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mwanachama.
Aidha, alisema kwamba atahakikisha Zanzibar inashirikiana na nchi wanachama wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) katika mipango yake ya kuimarisha Sera ya uchumi wa buluu ambayo ndio dira ya uchumi wa Zanzibar hivi sasa na tayari imepewa kipaumbele na nchi wanachama wa Mkataba huo.
Rais Dkt. Mwinyi alimuhakikishia Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA), Wamkele Mene kwamba Serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zitahakikisha wafanyabiashara na wawekezaji pamoja na wananchi wote kwa jumla wanatumia fursa za masoko na uwekezaji zilizoko katika Mkataba huo.
Sambamba na hayo, Rais Dkt. Mwinyi alisema kuwa atahakikisha wafanyabiashara na wajasiriamali waliopo nchini wanapewa elimu ya kutosha ili kuweza kutumia fursa zilizoko katika soko la nchi wanachama wa (AfCFTA).
Nae Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA), Bwana Wamkele Mene alimueleza Rais Dk. Mwinyi jinsi alivyofarijika kupata fursa ya kuja Zanzibar kwa mara ya pili.
Katika maelezo yake, Katibu Mtendaji huyo alieleza miongoni mwa malengo ya ujio wake ni pamoja na kuja kutoa elimu ya uwelewa na malengo ya Mkataba wa (AfCFTA) kwa Kamati ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar ambapo mafunzo hayo yanatarajiwa kufanyika siku ya Jumaapili ya Mei 22, 2022 hapa Zanzibar katika Hoteli ya Sea Cliff.
Aidha, kiongozi huyo alieleza kwamba uelewa pamoja na malengo hayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuwawezesha wananchi kufahamu vyema mipango na malengo ya Mikataba ya Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA), kwa nchi wanachama wake.
Katibu Mtendaji huyo wa Sekretarieti ya (AfCFTA), aliipongeza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi zinazoendelea kuchukuliwa katika kuimarisha utekelezaji wa Mikataba iliyopo tangu kujiunga kwake.
Alitumia fursa hiyo kueleza jinsi fursa zilizopo kwa nchi ndogo ndogo zikiwemo za visiwa ambazo zitafaidika moja kwa moja katika mikataba hiyo ikiwemo Zanzibar ambayo tayari imeshaonesha mikakati yake katika kuimarisha sera ya uchumi wa buluu.
Sambamba na hayo, kiongozi huyo alitumia fursa hiyo kumueleza Rais Dkt. Mwinyi shughuli na mikakati iliyowekwa na Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA), kwa nchi wanachama wake pamoja na mafanikio yaliyokwisha patikana.