Rais Dkt.Mwinyi:Profesa Abdulrazak Gurnah umeipa Zanzibar heshima kubwa Kimataifa, hongera sana

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amempongeza, Profesa Abdulrazak Gurnah, Mshindi wa Tuzo ya Nobel ya Fasihi ya mwaka 2021 kwa kuipa heshima kubwa Zanzibar katika anga za Kimataifa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiagana na mgeni wake Mshindi wa Tuzo ya Nobel ya Fasihi (2021), Prof.Abdulrazak Gurnah baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar leo. (Picha na Ikulu.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo wakati alipofanya mazungumzo na Profesa Abdulrazak Gurnah, Mshindi wa Tuzo ya Nobel ya Fasihi ya mwaka 2021 ambaye alifika Ikulu Zanzibar, kufuatia mwaliko wa Rais Dkt. Mwinyi.

Katika maelezo yake, Rais Dkt. Mwinyi alimueleza mshindi huyo wa Tuzo ya Nobel ya Fasihi ya mwaka 2021 kwamba Zanzibar inajivunia na kuona fahari kutoa mtu aliyefanikiwa kwa kupata tuzo hiyo ambayo ni kubwa duniani.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amempongeza Profesa Gurnah kwa utayari wake wa kufanya kazi na kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mambo mbali mbali ya kimaendeleo ikiwemo maonesho ya vitabu.

Rais Dkt. Mwinyi pia ametumia fursa hiyo kumkaribisha nyumbani Mshindi huyo wa Tuzo ya Nobel ya Fasihi ya mwaka 2021 na kumpongeza kwa mafanikio hayo aliyoyapata ambayo yameitangaza Zanzibar.

Pamoja na hayo, Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kufanya kazi na mtu yeyote mwenye azma ya kuitangaza Zanzibar.

Rais Dkt. Mwinyi pia, alieleza kwamba kwa vile Zanzibar ni nchi ya Kitalii na kwa vile nchi nyingi hivi sasa zimekuwa zikiyatumia matamasha katika kujitangaza hivyo, ipo fursa ya kujifunza kutokana na matamasha hayo na kueleza kwamba tamasha la vitabu ambalo Mshindi huyo ameahidi kuliunga mkono, litasaidia zaidi kuitangaza Zanzibar.

Mapema Profesa Abdulrazak Gurnah, Mshindi wa Tuzo ya Nobel ya Fasihi ya mwaka 2021alimpongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa kumpa mwaliko huo wa kuja kumuona ambapo mwaliko huo aliutoa Rais Dkt. Mwinyi siku aliyompongeza Mshindi huyo kwa kumpigia simu mara tu baada ya kutangazwa kupewa Tuzo hiyo.

Hivyo, katika mazungumzo hayo, Profesa Abdulrazak Gurnah, Mshindi wa Tuzo ya Nobel ya Fasihi 2021 alimuhakikishia Rais Dkt. Mwinyi utayari wake wa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mambo mbalimbali ya kimaendeleo.

Alitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa ukaribisho alioupata kutoka kwa Serikali, ndugu, jamaa na marafiki pamoja na makaribisho aliyoyapata kutoka kwa uongozi ZATO na FESTAC Africa 2022, Tamasha la Sanaa na Utamaduni wa Muafrika linalofanyika hapa Zanzibar katika Hoteli ya Verde iliyopo Mtoni.

Aidha, Profesa Abdulrazak Gurnah, Mshindi wa Tuzo ya Nobel ya Fasihi ya mwaka 2021 alieleza nia yake kwa Rais Dk. Mwinyi ya kushirikiana na watu wengine hapa nchini katika Tuzo mbali mbali ambazo zitakuwa zikitolewa kila baada ya muda ikiwa ni pamoja na kushirikiana na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).

Nao uongozi wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, ulieleza kufarajika kwa ujio wa Mshindi huyo pamoja na ahadi zake mbali mbali alizoahidi katika kuutangaza utalii wa Zanzibar ikwia ni pamoja na kuyatumia makumbushi ya Zanzibar kwa ajili ya kuweka vitu na nakala zake mbali mbali.

Profesa Abdulrazak Gurnah, Mshindi wa Tuzo ya Nobel ya Fasihi ya mwaka 2021 alizaliwa mnamo mwaka 1948 na kukulia Zanzibar na hatimae kuelekea Uingereza akiwa kijana kwa ajili ya masomo mwishoni mwa miaka ya 1960, Mwandishi huyu wa Tunzo hiyo ya Nobel ya Fasihi alikuwa Profesa wa Kiingereza katika Fasihi kwenye Chuo Kikuu cha Kent huko Ceterburry nchini Uingereza hadi alivyostaafu hivi karibuni.

Mnamo Alhamisi ya tarehe 07 Oktoba mwaka 2021 kituo kinachotoa tuzo kilimtangaza Profesa Abdulrazak Gurnah kuwa mshindi wa Tuzo ya Nobel ya Fasihi na kumpongeza kwa kuangazia suala la ukoloni na athari zake katika utunzi wake.

Tuzo hiyo inayotolewa na kituo hicho cha Sweden ina thamani ya corona milioni kumi za taifa hilo sawa na dola za Kimarekani milioni 1.4.

Mwandishi huyu wa riwaya, kazi yake ya kwanza aliandika akiwa na umri wa miaka 21 huko nchini Uingereza ambapo ndiye mwandishi wa kwanza Mtanzania kushinda Tuzo ya Nobel ya Fasihi na wa pili barani Afrika baada ya mwandishi wa vitabu Wole Soyinka kutoa nchini Nigeria.

Tunzo za Nobel ambazo zimetunzwa tangu mwaka 1901, zinatambua ufanisi katika fasihi sayansi, amani na uchumi ambapo washindi wa awali wamekuwa wakiwashirikisha waandishi wa Riyawa kama vile Emest Hemingway, Gabriel Garcia Marquez na Toni Morrison, washairi kama vile Pablo Neruda, Joseph Brodsky na Rabindranath Tagore na waandishi wa michezo ya kuigiza akiwemo Harold Pinter na Eugene O’Neill.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news