NA DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka watetezi wa haki za binadamu kufanya kazi za uhanaharakati zenye tija na kuibua changamoto na sio kupambana na Serikali.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wadau mbalimbali (hawapo pichani) kwenyemMaadhimisho ya miaka 10 ya Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) katika hafla iliyofanyika ukumbi wa PSSSF jijini Dar es Salaam tarehe 13 Mei 2022.
Rais Samia ameyasema hayo wakati akizindua ripoti ya miaka kumi ya mtandao wa watetezi wa haki za binadamu THRDC akisema kuwa, wasifanye kazi kwa kupambana na serikali ila wanachopaswa kufanya ni kuikosoa serikali kwenye mapungufu ili iyafanyie kazi.
Amesema, hakuna atakayejenga hii nchi bali ni kila mtu ambaye ni mtanzania mwenyewe kwa ushirikiano wa pamoja kati ya serikali na wadau wake wakiwemo THRDC huku akiwakaribisha kuzngumza na serikali muda wote bila woga wowote.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo kutoka kwa Mwenyekiti wa THRDC Jaji Mstaafu Joaquine De Mello kutokana na mchango wake wa kulinda na kusimamia haki za binadamu na utawala wa Sheria katika kipindi cha mwaka mmoja tangu aingie madarakani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akinyanyua Tuzo aliyopewa na Kituo cha THRDC kutokana na mchango wake wa kutetea Haki za Binadamu na utawala wa Sheria katika Maadhimisho hayo ya miaka 10 ya Kituo Jijini Dar es Salaam tarehe 13 Mei 2022.
“Tufanye kazi kwa pamoja tusiwe wagomvi kila kitu tuwekane wazi ninyi huko kila kitu mmekikumbatia wenye hata waziri hapa hana leteni tusome tuone nini mnacho huko na sisi tujue”.
Pia amewataka watetezi wa haki za binadamu kuaminiana serikali kwa kila mmoja kuzungumza huku akiwapongeza kwa hatua waliyoifikia kwa miaka kumi na kila mmoja andelee kufanya kazi kwa nafasi yake.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akikata utepe kuzindua Ripoti ya miaka 10 ya Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania THRDC mara baada ya hotuba yake tarehe 13 Mei, 2022.
Hata hivyo, Rais Samia amewahakikishia kuwapatia maeneo ya kujenga ofisi zao THRDC kama walivyoomba kwenye ripoti yao huku akiendelea kusisitiza ushirikiano wa kufanya kazi pamoja.