NA GODFREY NNKO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameahidi kuimarisha maslahi ya wafanyakazi nchini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdor Mpango, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Hussein Kattanga, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson, Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya wakiimba wimbo wa mshikamano (solidarity).(Picha na Ikulu).
Ahadi hiyo ameitoa leo Mei 1, 2022 katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi) ambayo Kitaifa yamefanyika katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Pia amesema alishatoa ahadi mwaka jana, ambapo ameagiza kufanyika majadiliano ya kuimarisha maslahi ya wafanyakazi yanayoendelea kati ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) na Serikali ili kujua kiwango cha maslahi yatakayohitajika.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia Wafanyakazi kutoka Sehemu mbalimbali nchini katika Sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi ambapo Kitaifa zimefanyika katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
"Ndugu zangu, jambo letu lipo si kwa kiwango kilichosemwa na TUCTA (Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi) kwa sababu mnajua hali ya uchumi wetu, na hali ya uchumi wa Dunia, hali si nzuri sana na uchumi wetu ulishuka chini sana, yale tuliyofanya mwaka huu, mambo mbalimbali ikiwemo kupunguza kodi, tutaendelea kuyafanya,"amesema Mheshimiwa Rais Samia.
Wafanyakazi kutoka taasisi mbalimbali za Serikali wakiwa katika Sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi ambapo Kitaifa zimefanyika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Samia ameagiza maafisa rasilimali watu na mifuko ya hifadhi ya jamii kushughulikia haki na stahiki za watumishi wanaotarajia kustaafu ndani ya miezi sita ili mtumishi anapofika muda wa kustaafu mafao yake yawe tayari.
Mheshimiwa Rais Samia akizungumzia kuhusu kiwango cha kikotoo amesema, kimekuwa na mvutano, lakini Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) limetaka wakutane.
“Sasa Serikali itakwenda kukaa katika utatu wetu ama sisi na TUCTA kuangalia jinsi tutakavyoenda kufanya. Lakini wazo mlilokuja nalo sio baya. Ombi langu kwenu TUCTA mtoe ushirikiano wa kutosha ili kwa mwaka huu ukimalizika lifanikiwe,”amesema Rais Samia.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa mara baada ya kuwasili katika uwanja wa Jamhuri kwa ajili ya kushiriki Sherehe za siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi ambapo Kitaifa zimefanyika jijini Dodoma.
Rais Samia amesema hakuna mshahara wala mafao yanayotosha lakini angalau kikotoo kiwe kwa kiwango cha kuridhisha.
TUCTA
Awali Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) lilimkumbusha Rais Samia ahadi yake ya kuboresha mishahara kwa wafanyakazi na kupendekeza kima cha chini cha mshahara kwa sekta zote kiwe shilingi milioni 1,010,000.
Katibu Mkuu wa TUCTA, Bw.Henry Mkunda akizungumza katika maadhimisho hayo amesema,“Tunakumbuka ahadi yako ya kuboresha mishahara katika mwaka huu wa 2022, hivyo TUCTA tunapendekeza kiwango cha kumwezesha mfanyakazi kuishi kiwe walau shilingi milioni 1,010,000 kwa mwezi baada ya hizi tafiti kufanyika. Tutashukuru sana Mama kama utaliona hilo,”amesema.
Bw.Mkunda amesema, sababu iliyowasukuma kuandaa kauli mbiu ya Mei Mosi ya 'Mishahara na Maslahi kwa Wafanyakazi ndio Kilio chetu, Kazi iendelee' ni wafanyakazi kuwa raslimali na nyenzo ya kuinua uchumi katika nchi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi zawadi ya Shilingi milioni 13 Afisa Msaidizi wa Mtendaji Mkuu akiwakilisha Chama cha Tughe Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika Sherehe za siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi ambapo Kitaifa zimefanyika katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Amesema pamoja na ukweli huo, wafanyakazi hawajaongezwa mishahara kwa takribani miaka tisa kwa sekta binafsi na miaka sita kwa sekta ya umma hali ambayo imesababisha kupungua kwa ari ya kufanya kazi, hivyo kupunguza ufanisi na uwajibikaji na tija mahali pa kazi.
Bw.Mkunda amesema tafiti zinaonyesha kuwa mishahara na maslahi humwezesha mfanyakazi kufanya kazi kwa ubora na ufanisi na weledi.
Pia amesema ni wazi gharama za maisha zimezidi kupanda na ili hali stahiki na ujira wa wafanyakazi zimeendelea kuwa duni.
Amesema kwa hivi sasa mshahara wa kima cha chini kwa sekta binafsi ni sh.40,000 na sh. 60,00 kwa mfanyakazi wa majumbani wakati kwa wafanyakazi wa mashambani na viwandani ni sh.100,000 viwango vilivyotangazwa mwaka 2013 katika Gazeti la Serikali.
Katibu huyo wa TUCTA amesema, kwa upande wa umma, kima cha chini cha mishahara ni sh.300,000 kilichotangazwa mwaka 2015.
Amesema, kufuatia hilo TUCTA ilifanya utafiti mwaka 2006 na kuwasilisha mapendekezo serikalini mapendekezo kuwa kima cha chini cha mshahara kinachomwezesha mfanyakazi kumudu mahitaji muhimu kwa wakati huo sh.315,000.
Bw.Mkunda amesema, utafiti mwingine ulifanyika mwaka 2014 na kubaini kuwa malipo ya mshahara ya sh.720,000 kwa mwezi yangemwezesha mfanyakazi wa kima cha chini kumudu gharama za maisha.
Pia amesema, pamoja na mapendekezo hayo viwango hivyo havijakubaliwa na Serikali na kwamba kutokubaliwa kwa mapendekezo hayo kumeathiri wafanyakazi na familia zao kutokana kupanda kwa gharama za maisha na kuwafanya kuishi maisha ya chini ya mstari wa umasikini.
Amesema, pamoja na UVIKO-19 na vita vya Urusi na Ukraine bado wafanyakazi wanaomba kuweka kiwango kitaifa cha kima cha chini cha mshahara ili kuwezesha wafanyakazi kuishi maisha bora.
Wafanyakazi kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali wakiwa katika Sherehe za siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi ambapo Kitaifa zimefanyika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Rais Samia akizungumzia kuhusu watumishi waliofanya kazi kwa muda mrefu na kisha kufukuzwa kazi kwa sababu ya vyeti vya kughushi bila kulipwa malipo yoyote amesema, ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kushughulikia stahiki zao zinazotokana na makato ya mishahara yao na kuwalipa.
“Waangalie walitoa kiasi gani lakini nasisitiza kile asilimia tano (walichochangia kutoka katika mishahara yao) na kuacha ile ya asilimia 10 ya mwajiri,” amesema.
Pia amesema ameziagiza Wizara ya Fedha na Mipango, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma kuangalia kiasi gani kitagharimu kuwalipa wafanyakazi waliofanya kazi kwa muda mrefu, lakini wakabakisha mwaka mmoja ama miwili kustaafu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiagana na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama mara baada ya kushiriki katika Sherehe za siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi ambapo Kitaifa zimefanyika katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
“Na wenyewe waangalie ni kiasi gani kitatugharamu kama tutawapa mafao yao baada ya kufanya kazi kwa muda mrefu. Tunayafanyia maamuzi baada ya kuona ni gharama kiasi gani Serikali itaingia,”amesema Rais Samia.