RC KUNENGE AWAANGUKIA WAFANYABIASHARA WA MAZAO YA MISITU (MKAA) KULIPA TOZO ZILIZOPO,ASEMA SERIKALI YA AWAMU YA SITA INASHUGHULIKIA CHANGAMOTO ZAO

NA ROTARY HAULE

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amewaomba wafanyabiashara wa mazao ya misitu waliopo maeneo mbalimbali ndani ya mkoa huo (Mkaa) kuendelea kulipa tozo zilizopo kwa kuwa zimewekwa kisheria.
Kunenge ametoa kauli hiyo leo ofisini kwake katika mkutano wake na waandishi wa habari pamoja na timu ya uongozi wa Wakala za Huduma ya Misitu Kanda ya Mashariki (TFS).

Amesema, kumekuwa na changamoto kutoka kwa wafanyabiashara wa mkaa na upande wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) lakini changamoto hizo zimepitishwa na zimepelekwa kwa Waziri husika ili kuzipitia.

"Niwaombe wafanyabiashara waendelee kutumia tozo zilizopo mpaka Waziri wa Maliasili na Utalii atakavyoamua vinginevyo kwa kuwa masuala ya kisheria yanakwenda kiutaratibu,"amesema Kunenge.

Aidha, Kunenge amesema tozo zinazotumika hivi sasa zipo kwa mujibu wa sheria na ziliwekwa kupitia GN namba 59-28-01 ya mwaka 2022 na kwamba mabadiliko yake yatafanyika kwa muongozo wa sheria.

Kunenge amesema,  kwa mujibu wa sheria hiyo viwango vinaelekeza kilo moja ya mkaa inapaswa kulipiwa Sh.250 sawa na Sh.37500 kwa gunia la kilo 100 mpaka 150.

Amesema,tozo hizo zimekuwa sehemu ya kuongeza pato la Mkoa na Taifa ambapo kwa kiasi kikubwa husaidia katika kuchangia katika miradi mbalimbali ya maendeleo.

Amesema,Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan ni sikivu na malalamiko hayo yatafanyiwa kazi ili kuwapa nafasi ya wafanyabiashara kujikwamua kiuchumi.

Amesema,Rais Samia yupo kwa ajili ya kutetea maslahi ya wananchi wake na hata katika tozo hizo anaimani litafanyiwa kazi na hivyo kuondoa malalamiko na changamoto ndogo ndogo za wafanyabiashara.

"Mimi nina imani kubwa sana na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa hiyo tuvute subira na tuendelee kutumia tozo zilizopo wakati Serikali inafanya marekebisho ya kisheria ya tozo hizo,"ameongeza Kunenge

Katika hatua nyingine Kunenge amewaomba wananchi kutumia njia mbadala ya nishati ya gesi kwa kuwa ni rahisi na inasaidia katika uhifadhi wa mazingira.

Hata hivyo,Kunenge amewaomba wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali yao katika kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika maeneo yao ili kuweza kufikia malengo ya kimaendeleo katika Taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news