ROYAL TOUR FAGILIA:Nchi kututangazia, watu wapate hamasa,Muda wa kujiandaa, kuvuna ujio wao

NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)

TANZANIA The Royal Tour ikiwa ni filamu mahususi iliyotengenezwa kuonesha vivutio vya utalii vilivyopo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tayari imezinduliwa.

Uzinduzi wake ulianzia jijini New York,Marekani Aprili 18,2022 baadaye Los Angeles nchini Marekani, Arusha, Zanzibar na Dar es Saalam nchini Tanzania.

Filamu hiyo ya dakika 56 inaonesha vivutio vya utalii, uwekezaji, sanaa na utamaduni vilivyopo nchini ambapo Rais Samia Suluhu Hassan ndiye kiongozi wa kutoa maelezo kuhusu vivutio hivyo kwa Peter Grenberg, ambaye ni mwanahabari nguli na mtozi wa filamu kutoka runinga ya CNBC nchini Marekani.

The Royal Tour, iliyorekodiwa nchini Tanzania mwaka 2021 ambapo Mheshimiwa Rais aliigiza kama mhusika mkuu wa filamu itatumika kutangaza vivutio vya utalii vya nchi kwa kiwango cha kimataifa, ikiwa ni sehemu ya mkakati mpya wa serikali za kukuza utalii baada ya janga la kimataifa la UVIKO-19.

Sekta ya utalii ya Tanzania ambayo iliathiriwa vibaya na janga hilo, imekuwa katika hali ya ahueni, ambapo takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonesha kuwa, katika kipindi cha mwaka unaoishia Februari 2022, mapato ya fedha za kigeni kutoka sekta hiyo yaliongezeka hadi dola za kimarekani bilioni 1.457 kutoka dola za kimarekani bilioni 645.4 katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Ongezeko hilo lilitokana na ongezeko la asilimia 87.9 la watalii waliofika na kufikia wasafiri 958,173 katika kipindi kilichoishia Februari 2022.

Ungana na Mshairi wa Kisasa Bw.Lwaga Mwambande hatua kwa hatua kupitia shairi hili uweze kujifunza jambo muhimu kuhusu filamu hii muhimu katika sekta ya utalii na uwekezaji nchini;

1:Ukweli utabakia, uonekanavyo hasa,
Royal Tour fagilia, tendo la maana hasa,
Nchi kututangazia, watu wapate hamasa,
Muda wa kujiandaa, kuvuna ujio wao.

2:Rais wetu Samia, hapa amelenga hasa,
Fursa tuibulia, kafungua ukurasa,
Dola nyingi kutujia, na sisi tuweze tesa,
Muda wa kujiandaa, kuvuna ujio wao.

3:Wageni watatujia, kufanya zao anasa,
Si dhambi za Biblia, kuona simba na kasa,
Wao watafurahia, sisi Euro tutanasa,
Muda wa kujiandaa, kuvuna ujio wao.

4:Huduma kuwapatia, watalii bora hasa,
Pesa waweze tumia, nasi tukusanye hasa,
Vema kujiandalia, zisitupite fursa,
Muda wa kujiandaa, kuvuna ujio wao.

5:Toka wanapoingia, hiyo kwetu ni fursa,
Hadi watapoishia, tuwe tumevuna hasa,
Tusije tukatulia, tuzikose hizo pesa,
Muda wa kujiandaa, kuvuna ujio wao.

6:Mnyororo hudumia, bila kufanya makossa,
Wao wakifurahia, mwakani hawatakosa,
Vema kuchangamkia, hili twapewa darasa,
Muda wa kujiandaa, kuvuna ujio wao.

7:Filamu waangalia, vivutio vyetu hasa,
Kilimanjaro anzia, kaishie Ziwa Nyasa,
Zanzibar tafurahia, kila kitu wakigusa,
Muda wa kujiandaa, kuvuna ujio wao.

8:Ushauri katwambia, Dokta Rioba hasa,
Awezaye chungulia, kurasa hadi kurasa,
Vema kazi kufanyia, ushauri huu hasa,
Muda wa kujiandaa, kuvuna ujio wao.

9:Jicho chanya angalia, ni kubwa hii fursa,
Vema tukiitumia, huko mbele ni anasa,
Mshiko tajipatia, maisha yawe asusa,
Muda wa kujiandaa, kuvuna huu ujio.

10:Heko Rais Samia, kuzifungua fursa,
Ambazo twatazamia, kuwa mgodi wa pesa,
Vile hatujatumia, vile ipasavyo hasa,
Muda wa kujiandaa, kuvuna huu ujio.

Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news