NA DIRAMAKINI
SIKU chache baada ya filamu ya Tanzania The Royal Tour kuzinduliwa, wadau mbalimbali duniani wamejitokeza kuja kutathimini misitu nchini kwa ajili ya biashara ya hewa ukaa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema hayo wakati akizindua filamu hiyo jijini Dar es Salaam juzi huku akisisitiza kuwa amefanya mazungumzo na wadau wakubwa wa utalii na wako tayari kuja pia.
“Nimefanya mikutano kadhaa na ‘giant’ wa sekta ya utalii nao pia baada ya kuona hii filamu, wameahidi kuja lakini filamu hii imeonyesha hali ya mazingira ya Tanzania, msitu wa Tanzania na tayari tushapokea maombi ya watu wa hewa ukaa kuja kufanya tathmini ya msitu wote waliouona, msitu wa Tanzania ili tuanze kuvuna fedha za hewa ukaa,” amesema Mhe.Rais.
Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi – TFS Prof. Dos Santos Silayo anasema anamshukuru Mhe. Rais kwa kuionyesha na kuizungumzia vizuri misitu kupitia filamu hiyo kiasi cha kuwavutia wawekezaji wengi kuja nchini kuwekeza hususan katika biashara ya hewa ukaa.
Prof. Dos Silayo anaongeza kuwa wadau hao wameamua kushirikiana na Tanzania ili kuweza kuimarisha misitu ili iweze kuwa sehemu ya chujio la hewa chafu duniani na kupunguza mrundikano wa gesi joto inayosababisha kuongezeka kwa joto duniani.
“Eneo la biashara ya hewa ukaa limeonekana kuwavutia wawekezaji wakubwa duniani katika bara la Asia na Marekani kuja kuwekeza na tayari kuna wawekezaji waliojitokeza tuko kwenye mazungumzo nao,” anasema Kamishna wa Uhifadhi wa TFS.
Aidha, Prof. Silayo anasema Wakala wa Huduma za Misitu nchini umejipanga katika maeneo matatu, kwanza kuhakikisha uhifadhi wa misitu unakuwa imara, pili kuhakikisha unatumia maeneo ya vitutio vya misitu kuvutia wawekezaji kwenye suala la utalii na mwisho ni kuhakikisha kunakuwa na uwekezaji katika viwanda vya misitu na nyuki.
Kamishna wa Uhifadhi huyo anasema kazi hiyo kubwa aliyofanya na Mhe. Rais itapelekea watu wengi kuifahamu Tanzania lakini kubwa ni kuona umuhimu wa kuwekeza katika sekta ya misitu hususan kilimo cha misitu ya kupanda na kuiacha misitu yetu ya asili ikiwa katika hali salama.