NA LILIAN LUNDO-MAELEZO
SERIKALI imesema kuwa, itaruhusu wenye uwezo wa kuleta mafuta kwa bei nafuu waweze kuleta mafuta ili kupunguza upandaji wa bei za mafuta hapa nchini.
Waziri wa Nishati, January Makamba amesema hayo leo Mei 10, 2022 bungeni jijini Dodoma, alipokuwa akitoa kauli ya kupanda kwa bei za mafuta na hatua zinazochukuliwa na serikali kushughulikia suala hilo.
“Wizara imekamilisha kufanya tathimini ya kampuni zote zilionesha nia ya kuleta mafuta kwa bei nafuu kwa lengo la kujiridhisha na uwezo wao wa kuleta mafuta hayo ili kuhakikisha uwepo wa mafuta nchini (security of supply),” alifafanua Makamba.
Aliendelea kusema kuwa, hatua hiyo ni moja ya hatua zisizo za kifedha zinazochukuliwa na serikali, mipango hii ikileta matokeo yanayotarajiwa basi bei za mafuta zitapungua zaidi kuanzia mwezi Agosti, 2022.
Makamba ametaja hatua nyingine zisizo za kifedha ambazo serikali imechukua, kuwa ni pamoja na kuanzisha mfuko wa kuhimili ukali wa bei za mafuta (Fuel Price Stabilization Fund), ambapo serikali imeandaa utaratibu wa kuanzisha mfuko maalum utakaotumika kupunguza makali ya bei ya mafuta kipindi ambacho bei hizo zinaongezeka kwa kiasi kikubwa.
“Mpango wa kuanzisha mfuko huu uko katika hatua za mwisho za maandalizi na utakapokamilika, utawasilishwa katika Baraza la Mawaziri,” alifafanua Makamba.
Aidha hatua nyingine ni kuanzisha Hifadhi ya Mafuta ya Kimkakati (National Strategic Petroleum Reserve), ambapo serikali inakamilisha marekebisho ya kanuni za kuanzisha na kuendesha hifadhi ya mafuta ya kimkakati ili nchi ijihakikishie usalama wa upatikanaji wa mafuta na unafuu wa bei katika vipindi kama hivi ambavyo bei ya mafuta inakuwa imepanda.
Vilevile serikali imechukua hatua ya kuanzisha kituo kikubwa cha mafuta (Petroleum Hub), ambapo ipo kwenye hatua ya kukamilisha makubaliano ya kujenga maghala makubwa ya kuhifadhi mafuta kwa ajili ya kuuzwa ndani na nje ya nchi kulingana na uhitaji. Uwepo wa kituo hicho utawezesha nchi kupata mafuta yenye bei nafuu pale bei zinapopanda kupita kiasi. Mpango huu na utekelezaji wake unaweza kukamilika katika kipindi cha miaka mitatu.
Hatua nyingine ni kuanzisha upokeaji wa mafuta katika ghala moja (Single Receiving Terminal – SRT) kupitia maghala ya TIPER ili kupunguza au kuondoa gharama za meli kusubiri au kuchukua muda mrefu katika upakuaji wa mafuta katika maghala mengi, ambapo gharama hizo pia zina mchango katika bei ya mafuta (dermurrage charges).
“Hatua hii itaondoa changamoto za udanganyifu na kuongeza ufanisi katika biashara ya mafuta hapa nchini. Hatua hii inaendana na kuyafanya maghala haya kuwa Customs Bonded Warehouse ili kushamirisha biashara ya mafuta yanayokuja nchini na kwenda kwenye nchi nyingine,” alifafanua Makamba.
Pia serikali inaongezea uwezo TPDC kuagiza mafuta nje ya nchi, ambapo mara ya mwisho ilifanya shughuli hiyo miaka 20 iliyopita, pamoja na kuimarisha utendaji na weledi wa taasisi za serikali zinazoshughulika na biashara ya mafuta nchini, ikiwemo EWURA na PBPA (Wakala wa Uagizaji wa Mafuta Pwani).
Makamba amesema kuwa, hatua hizo zitafafanuliwa kwa kirefu na wabunge watapewa fursa ya kutoa maoni na ushauri wakati wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati wiki tatu zijazo.