NA HAPPINESS SHAYO-WMU
SERIKALI kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeratibu maandalizi ya Mpango wa Kitaifa wa miaka 10 wa Kuenzi na Kutangaza Urithi wa Mwalimu Nyerere kwa lengo la kuibua, kuhifadhi na kutangaza vielelezo vinavyoonesha mambo ya msingi aliyoyaasisi Baba wa Taifa na kuyasimamia.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) katika Kongamano la Miaka 100 ya Mwalimu Nyerere na Uzinduzi wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere uliofanyika jijini Dodoma leo ukumbi wa Jakaya Kikwete.
“Mambo ya msingi aliyoyasimamia na kuyaasisi Baba wa Taifa ni pamoja na amani, heshima, utu, utulivu, umoja wa kitaifa, uhuru, kazi, demokrasia na maendeleo ya watu,” Mhe. Masanja amesisitiza.
Amefafanua kuwa utekelezaji wa mpango huo umejikita katika kuangalia uwepo wa mkakati wa kukusanya, kuhifadhi na kutangaza urithi wa dunia; kujengwa na kuboreshwa kwa miundombinu katika maeneo ya urithi wa Mwalimu Nyerere na Kuwepo kwa mfumo shirikishi wa kuratibu utekelezaji wa kazi za kumuenzi Mwalimu Nyerere.
Pia amesema, utekelezaji huo utagusa masuala ya kujengea uwezo na kuimarishwa uelewa wataalam na jamii kuhusu uhifadhi wa urithi wa Mwalimu Nyerere, tunu za Kitaifa zilizoasisiwa na Mwalimu Nyerere ikiwemo Lugha ya Kiswahili na kubuni vyanzo vipya vya mapato endelevu vya kuwezesha shughuli za kumuenzi Mwalimu Nyerere.
Mhe. Masanja ameweka bayana kuwa utekelezaji wa mpango huo utawezesha kujengwa kwa Makumbusho ya wapigania uhuru ya kwanza Afrika ambayo itaonesha mchango wa Tanzania katika ukombozi wa Bara la Afrika na pia urithi wa Hayati Mwalimu Nyerere utatambulika, kuhifadhiwa, kusherehekewa ndani na nje ya Tanzania.