NA DIRAMAKINI
KLABU ya Simba SC imetangaza kumfuta kazi Kocha Mkuu, Mhispania Pablo Franco Martin (41) ikiwa ni siku 207 toka aajiriwe na klabu Novemba 6, 2021.
Pablo amefutwa kazi pamoja na Kocha wa viungo Daniel De Castro Reyes ikiwa ni siku mbili zimepita toka Simba SC ivuliwe Ubingwa wa Kombe la ASFC kwa kufungwa 1-0 na Yanga katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza huku Kombe pekee alilotwaa ni Mapinduzi Cup 2022 pamoja na kufika robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Aidha, taarifa za ndani zinadai hajafutwa kazi tu kwa sababu ya kufungwa na Yanga ila viongozi hawajavutiwa na mwenendo mzima wa timu yao ambao chini ya Pablo umepoteza matumaini ya kutetea taji lao la Ligi Kuu walilotwaa miaka minne mfululizo.
Kuhusu Pablo Franco
Kocha Pablo Franco Martin, mzaliwa wa Madrid, nchini Hispania, ndiye kocha mwenye CV iliyosheheni kuwahi kutokea katika historia ya soka hapa nchini.
Pablo Franco, alizaliwa Juni 11, 1980 katika jiji la Madrid, na hadi “Anatangazwa kuja” kwa Wekundu wa Msimbazi Simba, kocha huyo ana leseni ya UEFA Pro Licence ambayo inaelezwa kuwa ndiyo leseni inayotolewa kwa muhitimu wa mafunzo ya juu kabisa ya Ufundishaji (Coaching) na Usimamizi (Managerial) wa wa soka barani Ulaya.
Kocha huyo kijana ni miaka mitano iliyopita alikuwa akifanya kazi na Kocha mwenye mafanikio makubwa Duniani kwenye mpira wa miguu akiwa kama mchezaji na kocha, Maestro Zinedine Zidane “Zizou” kwenye Klabu ya Real Madrid ya Uhispania kama kocha msaidizi.
Kocha Pablo mbali na kuiongoza Real Madrid kam Kocha Msaidizi, aliwahi pia kufundisha timu za Getafe CF na Getafe B zote za Hispania, pia timu za Club Deportivo Santa Eugenia, Club Deportivo Illescas, Club Deportivo Puertollano zote za huko huko Hispania na FC Saburtalo ya Georgia.
Kocha huyo ana shahada ya juu ya kufundisha mbinu za mpira wa miguu, utimamu wa mwili wa mwanasoka na jinsi ya kuusoma na kuuchambua mpira wa soka timu zinapokuwa uwanjani.
Kocha Pablo alikuja Simba SC ikiwa nafasi ya pili na alama 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara (NBC Premier League) msimu huu wa 2021-2022,ikiwa ndiyo timu pekee kwenye ligi ambayo ilikuwa haijafungwa bao hata moja.Kwa msimu huu klabu hiyo mwenendo wake upo ovyo.