Utangulizi
Ofisi ya Rais – TAMISEMI, hutoa taarifa ya mapato na matumizi ya mapato ya Ndani ya Halmashauri, kwa kila robo mwaka, ili kuongeza uwazi na uwajibikaji katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri Nchini.
Hivyo, Ofisi ya Rais-TAMISEMI imeandaa taarifa ya Mapato na Matumizi ya mapato ya Ndani ya Halmashauri, kwa kipindi cha Julai, 2021 hadi Machi, 2022.
Katika kipindi hiki cha robo tatu ya mwaka wa fedha 2021/2021, uchambuzi na ulinganifu umefafanuliwa, si kwa makusanyo pekee, bali tumeongeza vigezo vingine sita (6). Vigezo hivi 6 ndio vitatumika kupima ufanisi wa Halmashauri, pamoja na Mikoa. Vigezo hivyo ni:
Ukusanyaji wa mapato ya ndani;
Ujibuji wa Hoja za Ukaguzi;
Matumizi ya mapato ya ndani katika miradi ya maendeleo;
Utoaji wa Mikopo kwa Vikundi ya asilimia kumi 10 ya mapato ya ndani;
Usimamizi wa urejeshaji wa Mikopo ya Vikundi; na Matumizi ya Fedha za Marejesho
Uchambuzi wa Ufanisi katika Ukusanyaji wa Mapato ya Ndani kwa Mwaka 2021/22
Mlinganisho wa Ukusanyaji wa mapato kati ya Mwaka wa Fedha 2020/21 na mwaka 2021/22
Katika mwaka wa fedha 2021/22, Halmashauri zimepanga kukusanya Shilingi Bilioni 863.9 kutoka kwenye vyanzo vya mapato ya ndani. Katika kipindi cha mwezi Julai, 2021 hadi Machi 2022, Halmashauri zimekusanya jumla ya Shilingi Bilioni 675.8, ambayo ni asilimia 78 ya makisio ya mwaka.
Makusanyo hayo ni sawa na asilimia 104 ya lengo la robo tatu ya mwaka. Itakumbukwa kwamba bajeti ya makusanyo ya mapato ya ndani, ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, iliongezeka kutoka Shilingi Bilioni 814.96 katika mwaka wa fedha 2020/21, hadi Shilingi Bilioni 863.9 katika mwaka wa fedha 2021/22.
Uchambuzi wa taarifa za mapato ya ndani ya Halmashauri, katika kipindi cha Julai, 2021 Machi 2022, umeonesha kuwepo kwa ongezeko la mapato halisi yaliyokusanywa kwa kiasi cha Shilingi bilioni 118.4, ikilinganishwa na kiasi kilichokusanywa katika kipindi kama hicho, cha Julai, 2021 - Machi 2022, sawa na ongezeko la asilimia 21.
Katika kipindi hiki, Julai 2021 Machi 2022, zipo Halmashauri ambazo zimeongeza jitihada katika ukusanyaji wa mapato, ikilinganishwa na kipindi kama hiki cha mwaka wa fedha 2020/21.
Halmashauri hizo ni Halmashauri za Wilaya za Ngorongoro (asilimia 34), Mtama (asilimia 36), na Kishapu (asilimia 36), Halmashauri ya Mji Bariadi (asilimia 36), na Halmshauri ya Manispaa ya Lindi (asilimia 36).
Katika kipindi hicho cha Julai, 2021 - Machi, 2022 Halmashauri hizo zilikuwa za mwisho. Pia zipo baadhi ya Halmashauri ambazo katika kipindi cha Julai, 2021 Machi 2022, zimeshuka katika ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ikilinganishwa na kipindi kama hiki cha Julai, 2020 Machi 2021.
Katika kundi hili Halmashauri ya Wilaya ya Msalala ambayo iliongoza kwa asilimia 117, imeshuka kwa asilimia 38, kutokana na makusanyo yaliyotokana na ushuru wa huduma katika migodi, ambayo hayakuwa yamewekwa kwenye Bajeti, na kuonekana wemekusanya fedha nyingi ikilinganishwa na Bajeti.
Hivyo, nazielekeza Halmashauri ziweke mazingira mazuri, ili kuwa na vyanzo ambavyo ni endelevu na vinavyoakisi uhalisia.
Mwenendo wa Ukusanyaji wa Mapato ya Ndani kwa Kipindi cha Julai Machi, 2022
Uchambuzi wa taarifa kuhusu ufanisi wa Halmashauri katika ukusanyaji wa mapato ya ndani, unaonesha kuwa Halmashauri 110 zimekusanya kwa asilimia 75, au zaidi ya lengo la mwaka.
Halmashauri 72 zimekusanya kati ya asilimia 50 hadi asilimia 75. Halmashauri 2 zimekusanya chini ya asilimia 50. Ulinganisho wa ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani, unaonesha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mlele, imeongoza katika Halmashauri zote 184, kwa kukusanya asilimia 139 ya makisio yake ya mwaka, ikifuatiwa na Halmashauri za Wilaya ya Rufiji asilimia 128, na Halmashauri ya Mji Mbulu kwa asilimia 126 ya makisio yake ya mwaka.
Hata hivyo, kuna uwezekano wa Halmashauri hizi kuwa na makisio yasiyoakisi uhalisia wa uwezo wake, wa ukusanyaji mapato ya ndani, hivyo kuhitaji kufanya mapitio ya bajeti, ili kuongeza bajeti ya makusanyo ya ndani.
Mfano mzuri ni Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji, ambayo imekuwa ikiweka makadirio ya chini kwa miaka 3 mfululizo.
Kwa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji nitataka kupata maelezo ya kina kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri na Katibu Tawala Mkoa kwa nini Halmashauri hii imeendelea kutoa makisio yasiyo akisi uhalisia wa vyanzo vya mapato yao ya ndani.
Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli imekuwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 43 ya makisio yake ya mwaka, ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, ambayo imekusanya asilimia 48 (Kiambatisho Na. 1A).
Katika kuzipima Halmashauri zote kwa kigezo cha wingi wa mapato (pato ghafi), Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imekusanya mapato mengi zaidi kuliko Halmashauri zote, kwa kukusanya Shilingi Bilioni 56.4, ikifuatiwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma Shilingi Bilioni 37.7, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Shilingi Bilioni 37.4, na Halmashauri 20 kati ya 184 zimekusanya kuanzia Shilingi Bilioni 5 na zaidi (Kiambatisho Na. 1B).
Uchambuzi kwa kuzingatia ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ikilinganishwa na bajeti ya mwaka kimkoa, umeonesha Mkoa wa Manyara, umeongoza kwa kukusanya asilimia 95 ya lengo la mwaka ikifuatiwa na Mkoa wa Pwani asilimia 91, Mkoa wa Njombe asilimia 88, na Ruvuma asilimia 87. Mkoa wa Singida umekua wa mwisho kwa kukusanya asilimia 63, ukifuatiwa na Mkoa wa Lindi asilimia 64, na Mkoa wa Rukwa asilimia 66 (Kiambatisho Na. 2A).
Katika kuipima Mikoa yote kwa kigezo cha wingi wa mapato (pato ghafi), Mkoa wa Dar es Salaam umekusanya mapato mengi zaidi kuliko Mikoa mingine, kwa kukusanya Shilingi Bilioni 146.7, ikifuatiwa na Mkoa wa Dodoma Shilingi Bilioni 48.9, na Mkoa wa Rukwa umekuwa wa mwisho kwa kukusanya Shilingi Bilioni 6.4, ukifuatiwa na Mkoa wa Katavi kwa kukusanya shilingi Bilioni 9.5. (Kiambatisho Na. 2B).
Taarifa ya Mapato ya Ndani ya Halmashauri kwa Kuzingatia aina (kundi) ya Halmashauri
Halmashauri za Majiji
Katika kipindi cha Julai hadi Machi kwa mwaka wa fedha 2021/22, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeongoza kwa kukusanya mapato kwa asilimia 81 ya makisio yake ya mwaka, ikifuatiwa na Halmashauri za Majiji ya Mwanza, na Arusha ambazo zimekusanya asilimia 80 ya makisio ya mwaka, na Halmashauri ya Jiji la Mbeya asilimia 78. Halmashauri za Majiji ya Dodoma na Tanga zimekuwa za mwisho, katika kundi hili kwa kukusanya asilimia 75 ya makisio ya mwaka (Kiambatisho Na. 3A).
Halmashauri za Manispaa
Katika kipindi cha Julai hadi Machi 2021/22, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, imeongoza kwa kukusanya mapato kwa asilimia 90 ya makisio ya mwaka, ikifuatiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Musoma asilimia 88, na Halmashauri ya Manispaa ya Kahama asilimia 85.
Katika kundi hili Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara imekuwa ya mwisho, kwa kukusanya asilimia 59 ya makisio ya mwaka, ikifuatiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Lindi asilimia 60, na Manispaa ya Kigoma asilimia 61 (Kiambatisho Na. 3B).
Halmashauri za Miji
Katika kipindi cha Julai hadi Machi 2021/22, Halmashauri ya Mji wa Mbulu imeongoza kwa kukusanya asilimia 126 ya makisio ya mwaka, ikifuatiwa na Halmashauri ya Mji wa Kibaha asilimia 105, na Mji wa Njombe asilimia 98.
Halmashauri za Miji ya Korogwe na Bariadi zimekuwa za mwisho kwa kukusanya asilimia 69 ya makisio ya mwaka, zikifuatiwa na Halmashauri za Miji ya Nanyamba na Handeni, ambazo zimekusanya kwa asilimia 70 (Kiambatisho Na. 3C).
Halmashauri za Wilaya
Katika kipindi cha Julai hadi Machi 2021/22, Halmashauri ya Wilaya ya Mlele imeongoza kwa kukusanya asilimia 139 ya makisio ya mwaka, ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji asilimia 128, na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro asilimia 122.
Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli imekuwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 43 ya makisio ya mwaka, ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni asilimia 48 ya makisio ya mwaka (Kiambatisho Na. 3D).
Matumizi ya Mapato ya Ndani
Halmashauri zenye mapato ya ndani chini ya shilingi bilioni 5, zimeelekezwa kutenga na kutumia asilimia 40 ya mapato yake kutekeleza miradi ya maendeleo, na Halmashauri zenye mapato zaidi ya shilingi bilioni 5, zimeelekezwa kutenga na kutumia asilimia 60 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Matumizi katika Miradi ya maendeleo
Uchambuzi wa taarifa za matumizi ya fedha za mapato ya ndani kwa kipindi cha kuanzia Julai 2021 hadi Machi 2022, unaonesha kuwa Halmashauri zimetumia Shilingi Bilioni 210.7, sawa na asilimia 63.52 ya makisio ya miradi ya maendeleo ya mwaka. Matumizi hayo ni asilimia 82.98 ya fedha zilizopaswa kutumika kwenye miradi ya maendeleo, kiasi cha Shilingi Bilioni 253.99.
Halmashauri 17 zimetumia asilimia 100 au zaidi ya kiasi kilichopaswa kutumika, Halmashauri 151 zimetumia asilimia 50 hadi 99, na Halmashauri 16 zimetumia chini ya asilimia 50.
Taarifa zinaonesha kuwa Halmashauri ya Mji wa Njombe imeongoza kwa kuchangia asilimia 138, ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya asilimia 124, na Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga asilimia 119.
Aidha, Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma imekuwa ya mwisho kwa kuchangia asilimia 26, ikifuatiwa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti asilimia 28, na Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli asilimia 31 (Kiambatisho Na. 4).
Mikopo ya Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu
Uchambuzi wa taarifa za matumizi ya fedha za mapato ya ndani kwa kipindi cha Julai 2021 hadi Machi 2022, unaonesha kuwa Halmashauri zimechangia Shilingi Bilioni 43.05 kwenye Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, ambayo ni asilimia 63.62 ya makisio ya mwaka. Matumizi haya ni asilimia 83.57 ya fedha zilizopaswa kupelekwa kwenye Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu kwa kipindi cha Julai 2021 hadi Machi 2022.
Kwa kipindi hiki kiasi kilichopaswa kupelekwa ni Shilingi Bilioni 51.51 ambazo ni asilimia 10 ya mapato yaliyokusanywa yasiyolindwa.
Halmashauri 22 zimechangia asilimia 100 au zaidi, Halmashauri 152 zimechangia asilimia 50 hadi 99, na Halmashauri 10 zimechangia chini ya asilimia 50 kwenye mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu. Taarifa zinaonesha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imeongoza kwa kuchangia asilimia 127, ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga asilimia 119, na Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa asilimia 114.
Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga imekuwa ya mwisho kwa kuchangia asilimia 30, ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi asilimia 34, na Halmashuri ya Wilaya ya Kalambo asilimia 35 (Kiambatisho Na.5).
Tathmini ya Jumla
Tathmini ya ujumla imezipima Halmashauri kwa kutoa alama kwenye vigezo vya mapato na matumizi ya mapato ya ndani, vilivyobainishwa hapo juu na kuongeza vigezo vingine vya ujibuji wa hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, pamoja na usimamizi na matumizi ya fedha za marejesho ya mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri.
Katika kipindi cha Julai 2021 hadi Machi 2022, tathmini ya ufanisi wa utendaji wa Halmashauri ni asilimia 70 (Kiambatisho Na. 6). Tathmini hii imezingatia vigezo 6 kama nilivyoeleza awali, ambavyo vimepewa uzito kulingana na umuhimu wake. Vigezo hivyo ni:
Ukusanyaji wa mapato ya ndani (Alama 20)
Kigezo hiki kimezingatia kiwango cha makusanyo halisi ya Mapato ya ndani ikilinganishwa na bajeti ya mwaka.
Ujibuji wa Hoja za Ukaguzi (Alama 20)
Kigezo hiki kimezingatia idadi ya hoja zote zilizojibiwa na kufungwa ikilinganishwa na Hoja zote za Halmashauri husika.
Matumizi ya mapato ya ndani katika miradi ya maendeleo (Alama 35)
Kigezo hiki kimezingatia jumla ya fedha za mapato ya ndani zilizotumika kwenye miradi ya maendeleo ikilinganishwa na fedha zilizopaswa kutumika kwenye miradi ya maendeleo kwa kipindi husika.
Utoaji wa Mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani (Alama 10),
Kigezo hiki kimezingatia fedha zilizopelekwa kwenye vikundi vya Wanawake, Vijana na watu wenye Ulemavu ikilinganishwa na fedha inayopaswa kupelekwa katika kipindi husika.
Usimamizi wa urejeshaji wa Mikopo ya asilimia 10 (Alama 10).
Kigezo hiki kimezingatia namna Halmashauri zilivyosimamia ukusanyaji wa marejesho yanayopaswa kurejeshwa katika kipindi husika (asilimia 75 ya marejesho yanayopaswa kurejeshwa kwenye mwaka 2021/22 ikilinganishwa na marejesho halisi).
Matumizi ya Fedha za Marejesho (alama 5)
Kigezo hiki kimezingatia namna Halmashauri zilivyotumia fedha za marejesho kwa kuzingatia kanuni ya 23 ya Utoaji na Usimamizi wa Mikopo kwa vikundi vya Wanawake, vijana na watu wenye Ulemavu (kukopesha vikundi pamoja na usimamizi na ufuatiliaji)
Matokeo ya Tathmini ya ujumla
Muhtasari wa Matokeo ya tathmini unaonesha Halmashauri 24 zimefanya vizuri kwa kupata alama kati ya 81-100, Halmashauri 38 zimepata alama kati ya 75 80, Halmashauri 90 zimepata alama 61 74, na Halmashauri 32 zimepata alama kati ya 21-60 kama inavyoonekana katika Jedwali Na. 1
Matokeo hayo yanaonesha Halmashauri ya Mji wa Mbulu imeongoza kwa kupata alama 89.63 ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Babati iliyopata alama 89.53. Halmashauri 5 zilizoongoza zimeoneshwa katika Jedwali Na.2.
Jedwali Na. 2: Halmashauri 5 zilizoongoza
Tathmini inaonesha Halmashauri ya Wilaya ya Bunda imekuwa na alama za chini zaidi, ikilinganishwa na Halmashauri nyingine ambapo imepata alama 37.53. Halmashauri 5 zilizopata alama za chini zaidi zimeoneshwa katika Jedwali Na. 3:
Jedwali Na. 3: Halmashauri 5 zilizopata alama za chini
MKutokana na tathmini hii, Ofisi ya Rais TAMISEMI imekwishaanza kuchukua hatua, ikiwemo kuwabadilisha vituo baadhi ya Wakuu wa Idara na Vitengo, kufanya msawazo kwa watumishi na kuwabadilishia majukumu baadhi ya Wakuu wa Idara na Vitengo, kwa lengo la kuimarisha utendaji kazi.
Katika kulitekeleza hili, nimekwishafanya mabadiliko kwa Wakuu wa Kitengo cha Manunuzi, na leo ninatoa mabadiliko kwa Wakuu wa Kitengo cha Fedha ambapo Wakuu wa Vitengo vya Fedha 109 wamebadilishiwa vituo, 72 wamebaki kwenye vituo vyao vya awali, 3 wamebaki kwenye vituo vya awali kwa matazamio na 16 wamebadilishiwa majukumu. Nitaendelea kufanya mabadiliko kila wakati inapobidi. Katika eneo hili napenda kutoa salamu kwa Wakurugenzi na Wakuu wa Kitengo cha Fedha kuwa, sitavumilia kabisa uzembe katika ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya Serikali mfano;
Marekebisho ya miamala kwenye mfumo wa makusanyo ya mapato ya ndani bila kuwa na ushahidi wa idhini pamoja na viambatisho vinayothibitisha uhalali wa marekebisho hayo, mfano Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imefanya marekebisho pasipo kuwa na vithibitisho ya shilingi bilioni 10.86 na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela iliyofanya marekebisho bila vithibitisho yenye thamani ya shilingi bilioni 8.72 kwa mujibu wa Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali yam waka 2020/21
Uwepo wa mapato yaliyokusanywa lakini hayakuwasilishwa Benki. Mfanop Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ambayo ina hoja hii yenye thamani ya shioilingi bilioni 1.27, Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji ina hoja hii yenye thamani ya shilingi bilioni 1.96,
Uwepo wa hoja ya vifaa vilivyolipiwa lakini havijapokelewa na Halmashauri.
Ili kuendelea kuimarisha uwajibikaji na utendaji kazi, tathmini ya mwisho wa mwaka pamoja na vigezo hivi, itajumuisha pia vigezo vya sekta ya afya, elimu, miundombinu, na utawala bora kwa lengo la kuzifanya Halmashauri ziongeze juhudi katika kuboresha huduma na kutatua kero za Wananchi. Matokeo ya tathmini hiyo yatatumika pia kufanya tathmini ya Wakurugenzi, Wakuu wa Idara na Vitengo, Makatibu Tawala wa Mikoa, na makatibu Tawala Wasaidizi.
Maelekezo Mahsusi
Wakuu wa Mikoa wanaelekezwa kutekeleza yafuatayo:-
Kuzingatia vigezo 6 vilivyobainishwa na OR TAMISEMI sambamba na kuweka mfumo wa upimaji wa utendaji kazi wa Wakurugenzi na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri.
Kuhakikisha Halmashauri zote ambazo zimekusanya chini ya asilimia 75 ya lengo, la mwaka la makusanyo ya Mapato ya ndani, zinasimamiwa na kuandaa mkakati wa kuhakikisha zinafikia malengo yao, ifikapo mwisho wa mwaka tarehe 30 Juni 2022.
Kuhakikisha Halmashauri ambazo zimetumia chini ya asilimia 100 ya fedha za maendeleo zilizokusanywa katika kipindi cha Julai 2021 hadi Machi 2022, zinapeleka fedha hizo kwenye miradi kwa mujibu wa bajeti.
Kuhakikisha Halmashauri ambazo zimepeleka chini ya asilimia 100 ya fedha zilipaswa kupelekwa kwenye mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, zinapeleka kwa mujibu wa sheria.
Kusimamia na kufanya uchambuzi wa mahitaji halisi ya mashine za kukusanyia mapato (POS), ili kubaini upungufu uliopo na kuchukua hatua. Ninasisitiza Mikoa iongeze usimamizi wa matumizi sahihi ya POS ili kudhiti upotevu wa mapato ya Serikali na kuondoa PoS zenye toleo la zamani.
Kuhakikisha ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo katika Halmashauri, inajumuisha ukaguzi wa Miradi inayotokana na mikopo ya asilimia 10, inayotolewa kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu. Mikoa ibainishe kiasi chote cha fedha za mikopo ya asilimia 10, ambacho hakijarejeshwa, na kusimamia urejeshaji na kuwasilisha taarifa Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Kusimamia na kuhakikisha hoja zote za ukaguzi zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinajibiwa kikamilifu na kufungwa.
Innocent L. Bashungwa (Mb.)
WAZIRI WA NCHI, OR TAMISEMI
05 Mei, 2022