Tufanye mazoezi kwa afya na tujiandae kwa Sensa asema Mke wa Rais wa Zanzibar

NA DIRAMAKINI

MKE wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi amesema kuwa mazoezi ni umoja, mshikamano na upendo ambao utaendelea kuleta amani ya kudumu hapa Zanzibar.
Mke wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation Mama Mariam Mwinyi akijumuika na Wananchi na Vikundi vya mazoezi ya viungo vya Wilaya ya Kaskazini “B” Unguja katika mazoezi ya pamoja yaliyofanyika katika viwanja vya mpira Bumbwini Makoba na (kushoto kwake) Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mhe.Ayoub Mohammed Mahmoud na (kulia kwake), Mama Asha Shamsi wakijumuika katika mazoezi hayo baada ya kumaliza matembezi ya Kilomita Tano yaliyoazia katika makutano ya barabara ya Mangapwani. (Picha na Ikulu).

Mama Mariam Mwinyi ameyasema hayo Mei 28, 2022 huko katika viwanja vya Skuli ya Sekondari Bumbwini Makoba, Wilaya ya Kaskazini ‘B’, Mkoa wa Kaskazinii Unguja mara baada ya kumaliza mazoezi ya kilomita tano aliyoyaongoza ambayo yalianzia njia ya panda ya kuelekea Mangapwani Mkoani humo mnamo majira ya 12 za asubuhi.

Amesema kuwa, matembezi hayo ni ahadi yake aliyoitoa mnamo Febuari 19 mwaka huu wakati akizindua taasisi yake ya ‘Zanzibar Maisha Bora Foundation’ (ZMBF),ambapo aliahidi kuwa yeye atakuwa championi na kinara katika kuhamasisha ufanyaji wa mazoezi.

Amesema kuwa, mazoezi yana umuhimu hasa katika kuimarisha afya, kwani kufanya mazoezi kunauweka mwili salama, kunazuia magonjwa mengi ambayo si ya kuambukiza, kufanya kazi vizuri, kutokuwa mtu wa kwenda hospitali mara kwa mara na kuwaacha wale ambao wana maradhi ya kwedna hospitali tu.
Mke wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation, Mama Mariam Mwinyi akiwasalimia wananchi wa Kijiji cha Bumbwini wakati akiwa katika matembezi ya Kilimita Tano yalioazia katika makutano ya barabara ya Mangapwani na kumalizia kwa mazoezi ya viungo yaliyofanyika katika viwanja vya mpira Bumbwini Makoba Wilaya ya Kaskazini “B” Unguja na kushoto kwake) Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud. (Picha na Ikulu).

Mama Mariam Mwinyi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya ‘Zanzibar Maisha Bora Foundation’ (ZMBF), alisema kuwa kufanya mazoezi kutapunguza msogamano katika hospitali hapa nchini sambamba na kuipunguzia mzigo mkubwa katika Bajeti ya sekta ya Afya.

Alisisitiza kwamba mazoezi ni maendeleo na kuahidi kuwa hatochoka katika kutekeleza juhudi zake hizo na kusema kwamba utamaduni huo atauendeleza.
Mama Mariam Mwinyi alisisitiza umuhimu wa sensa ya watu na makazi na kuwahimiza wananchi kujitokeza siku itakapofika kwa azma ya kupata kujua idadi ya watu ili kupata takwimu na hatimae kuisaidia Serikali kupanga maendeleo.

Mama Mariam Mwinyi alitumia fursa hiyo kupongeza na kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuwa mstari wa mbele kwa kuhamasisha sensa ya watu na makazi kwa ajili ya maendeleo.

Aliwasihi akina mama kuhakikisha wanatumia fusra hiyo kuhamasisha zoezi la sensa ya watu na makaazi kwa watu wa rika zote wakiwemo wazee, watoto, vijana wa kike na kiume, wagonjwa, walemavu ili kujua idadi yao na kuiwezesha Serikali kuongeza huduma mijini na vijijini.
Alitumia fursa hiyo kueleza kwamba Mei 28, ni siku ya hedhi salama duniani ambalo ni suala muhimu sana kwa ustawi wa wanawake na vijana wa kike na kusisitiza kuitumia siku hii kwa kuelimishana juu ya masuala ya makuzi na afya ikiwa ni pamoja na kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana mashuleni.

Alisema kuwa, mazoezi hayo yatakuwa endelevu na yataendelea katika Wilaya na Mikoa mengine yote ya Unguja na Pemba ili Wazanzibari wote wawe na afya njema na kuleta maendeleo ya haraka.
Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Leila Mohamed Mussa kwa niaba ya Waziri wa Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo alieleza umuhimu wa mazoezi na kusema kwamba mazoezi ni tiba na afya huku akiwaasa wananchi kutosubiri kuambiwa na madaktari kufanya mazoezi.

Alisema kwamba lengo la Mama Mariam Mwinyi ni kutaka Wazanzibari wote kujua umuhimu wa kufanya mazoezi na kusisitiza kuwa kinga ni bora kuliko tiba.

Alimpongeza Mama Mariam Mwinyi kwa kuwaamsha na kuwahamasisha Wazanzibari umuhimu wa kutumia fursa ya uzima kabla ya maradhi huku akimpongeza kwa ukakamavu wake wa kufanya mazoezi.
Waziri Leila, kwa niaba ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo aliompongeza Mama Mariam Mwinyi kwa wazo lake hilo na kueleza kwamba wataendelea kumuunga mkono pamoja na taasisi yake ili iweze kutekeleza vyema majukumu iliyojipangia.

Alimpongeza Mama Mariam Mwinyi kwa kuwa ni sehemu ya kutekeleza majukumu yao na kuahidi kufanikisha yale yote aliyopanga katika taasisi yake likiwemo ufanyaji wa mazoezi.

Mapema Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Ayoub Mohammed Mahmoud alitoa shukrani kwa Mama Mariam Mwinyi kwa uwamuzi wake wa kuamua kufanya mazoezi kupitia taasisi yake ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF),” ambapo kwa mwezi huu ameamua kuungana na wananchi wa Mkoa huo.

Mkuu wa Mkoa huyo alitumia fursa hiyo kumpongeza na kumshukuru Rais Dk. Mwinyi kwa kuendelea na kazi kubwa anayoifanya ambapo wananchi wa Mkoa huo wanaridhika sana.

Alisema kuwa wananchi wa Mkoa huo wameridhishwa na yanayoendelea na yanayopangwa kwa ajili ya maendeleo yao na Taifa lao ambapo katika kipindi kifupi cha uongozi wake wamefaidika katika maeneo mengi.
Akiyataja miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana katika uongozi wa Rais Dk. Mwinyi, kwamba kwa upande wa sekta ya elimu wamepatiwa madarasa 188 na karibu yote yanakaribia kukamilika.

Aidha, alisema kuwa katika sekta hiyo hiyo ya elimu kutokana na hali ya afya na kuzingatia mazingira ya watoto walio shuleni wamepatiwa vyoo 338 na vyote vinakaribia kukalimika pamoja na nyumba mbili za walimu pamoja na kupatiwa hospitali mbili za Wilaya ikiwemo Kivunge Wilaya ya Kaskazini ‘A’, na Pangatupu iliyopo Wilaya ya Kaskazini ‘B’, Unguja.

Aliongeza kwamba kwa upande wa barabara Mkoa huo umepatiwa kilomita 46 katika maeneo mbali mbali ikiwemo barabara ya kuelekea Kiongwe, Bumbwini kuelekea Pangatupu Mahonda na barabara ya Zingwezingwe, ambazo zote hizo mikataba imeshasainiwa na wakandarasi wako katika maeneo ya ujenzi wanaendelea na upembuzi yakinifu.
Na kwa upande wa sekta ya maji, Mkoa huo umepatiwa matangi mawili ya maji yatakayokuwa na ujazo wa lita milioni moja kila moja ambapo moja litakuwa Tumbatu na jengine Bumbwini na kuendeleza visima 16 katika Mkoa huo.

Mkuu wa Mkoa huo alisisitiza kwamba juhudi hizo zinazochukuliwa na Serikali pia, zitachangia kwa kiasi kikubwa kufanya mazoezi na kupelekea wananchi kuwa na afya na kueleza kwamba mazoezi hayo yatawasaidia kwa kiasi kikubwa wananchi wa Mkoa huo huku akisisitiza suala zima la sensa ya watu na makaazi.

Viongozi mbalimbali walishiriki mazoezi hayo wakiwemo wake wa viongozi wastaafu akiwemo Mke wa Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mstaafu Mama Asha Balozi, Mke wa Waziri Kiongozi Mstaafu Mama Asha Shamsi Vuai Nahodha, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said, pamoja na viongozi wengine wa vyama vya siasa na serikali, wananchi pamoja na vikundi mbali mbali vya mazoezi kikiwemo Chama Cha Mazoezi ya Viungo Zanzibar (ZABESA) kupitia zoni C ya Mkoa huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news