NA DIRAMAKINI
MAAFISA Utumishi na wananchi wametahadharishwa kuchukua tahadhari dhidi ya baadhi ya watu wanaojitambulisha kwa majina na vyeo tofauti kuwa ni wafanyakazi katika Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Umma na wamekuwa wakiomba kupatiwa taarifa mbalimbali za masuala ya Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma na wengine kuomba kupatiwa fedha.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Richard Cheyo ametoa tahadhari hiyo kupitia taarifa kwa umma aliyoitoa leo Mei 31, 2022 Jijini Dodoma.
“Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Umma kwa nyakati tofauti imepokea taarifa za kuwepo kwa baadhi ya Watu ambao pasipo Tume kujua wamekuwa wakiwapigia simu, kutuma ujumbe “SMS” kwa baadhi ya Maafisa Utumishi na baadhi ya Watu waliowasilisha mashauri na malalamiko yao Tume. Watu hao wamekuwa wakijitambulisha majina na vyeo tofauti kuwa ni Wafanyakazi wa Tume ya Utumishi wa Umma na wamekuwa wakiomba kupatiwa taarifa mbalimbali za masuala ya Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma na wengine kuomba kupatiwa fedha,” amesema Bw. Cheyo kupitia taarifa hiyo.
“Ili kutimiza azma yao mbaya ya kuonekana ni Watumishi wa Umma, watu hawa matapeli wamekuwa wakiudanganya Umma na Wananchi kwa kujitambulisha kuwa ni Watumishi wa Serikali kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Umma, Watu hawa ni Matapeli na wapuuzwe. Tume inapenda kuufahamisha Umma kuwa tayari hatua stahiki zimechukuliwa na zinaendelea kuchukuliwa dhidi ya Watu hawa” amesema Bw. Cheyo.
Taarifa imefafanua kuwa Tume ya Utumishi wa Umma inazo taarifa kwamba matukio haya yametokea katika Mikoa mbalimbali ikiwemo Kigoma, Morogoro, Dar es Salaam, Tabora na Mtwara.
Tume kupitia taarifa hiyo imeufahamisha umma kuwa mawasiliano mahsusi yanaweza kufanyika kupitia simu namba 0738166 703 na 0733 005 974, barua pepe kwa anuani ya secretary@psc.go.tz au kufika katika Ofisi za Tume zilizopo Jengo la Chimwaga, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dodoma.
Mkuu wa Kitengo cha mawasiliano wa Tume hiyo Bw. Richard Cheyo ametoa rai kwa watumishi wa umma na wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya watu hawa na yeyote atakayepigiwa simu yenye viashiria vya utapeli na udanganyifu amesisitiza ni muhimu kutoa taarifa kwa Tume ya Utumishi wa Umma au kuripoti kwenye vyombo vya kiusalama mara moja ili hatua stahiki dhidi ya Watu hawa ziweze kuchukuliwa.