NA MWANDISHI PSC
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mheshimiwa Jenista J. Mhagama (Mb) ameiagiza Tume ya Utumishi wa Umma kuhakikisha katika mipango iliyopanga kuitekeleza Ukaguzi wa Rasilimali Watu katika Taasisi za Umma uwe ni kipaumbele.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista J. Mhagama (Mb) aliyekaa katikati, akiwa na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji Mstaafu Mhe. Hamisa H. Kalombola (aliyekaa kushoto), Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma Bw. Mathew M. Kirama (aliyekaa kulia) katika picha ya pamoja na Waheshimiwa Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma, Mhe. Waziri Mhagama (Mb) alikutana na kuzungumza na Makamishna wa Tume wakati wa mafunzo elekezi yaliyofanyika Dodoma. (Picha na PSC).
Mheshimiwa Waziri Jenista J. Mhagama (Mb) amesema hayo Mei 25,2022 wakati alipokutana na kuzungumza na Mwenyekiti na Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma walioteuliwa na kuapishwa na Mheshimiwa Rais tarehe 21 Mei 2022 Ikulu Chamwino Dodoma. Mwenyekiti na Makamishna hao wanashiriki mafunzo elekezi yanayofanyika katika Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dodoma.
Mwenyekiti na Makamishna wa Tume kwa mujibu wa Sheria mnatakiwa kumsaidia Mheshimiwa Rais juu ya usimamizi na uendeshaji wa masuala ya rasilimali watu kuhakikisha Utumishi wa Umma unaendeshwa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali iliyopo.
“Tuisimamie vizuri Rasilimali Watu iliyopo ili tubadilishe tabia, tubadilishe mwenendo, tubadilishe fikra na mtizamo wa Rasilimali Watu tuliyonayo, ianze kuona ina jukumu kubwa la kuwajibika kwa Watanzania, kuwajibika kwa Taifa, kuvaa uzalendo, kuleta tija katika utendaji kazi wao wa kila siku,”alisema Mheshimiwa Waziri Mhagama.
“Mkienda kukagua huko mtakuta kuna kasoro nyingi masuala ya likizo za watumishi, watu hawatengi fedha za likizo na matokeo yake ni madai na malimbikizo. Hii inasababisha Serikali badala ya kufikiria miradi mikubwa kama ya ujenzi wa reli inafikiria kulipa madai ya malimbikizo watumishi”.
Tatizo jingine ni kuwepo kwa Waajiri wachache ambao wanathubutu kupandisha madaraja Watumishi wa umma bila kuzingatia sifa na vigezo vilivyopo, sasa wakishapandisha hiyo Rasilimali Watu inaweza kuleta tija? Na kuzingatia matokeo, haiwezekani bado huko kuna shida na kasoro. Wapo baadhi ya Watumishi wanakaimishwa vyeo bila kuwa na sifa, mnategemea nini hii nalo haiwezekani. Haya yote lazima muendelee kuyabainisha kwenye Kaguzi zenu na kuishauri Serikali hatua za kuchukua.
Mheshimiwa Waziri Mhagama (Mb) alisema mazingatio ya mienendo mizima ya nidhamu katika kusimamia nidhamu kuna Watumishi wanaonewa na kuna watumishi ni watovu wa nidhamu na wengine hata hatua hazichukuliwi, hawa wanaharibu kabisa taswira nzuri ya Utumishi wa umma na mwenendo mzima wa Utumishi wa Umma, Tume mkifanya Ukaguzi mtawakuta.
Kwa upande wa mashauri ya nidhamu kuchukua muda mrefu kuhitimishwa alisema unakuta mtumishi wa umma ana kesi, shauri la nidhamu limeshafika miaka miwili, huyu mtumishi hawezi kuwa na tija. Shauri halijafungwa linaendelea tu taratibu nzima za kushughulikia shauri hazijafuatwa na wakati mwingine amesimamishwa na anaendelea kulipwa mshahara wa Serikali na haendi kuzalisha hii si sawa kuwa na Rasilimali ya namna hii kwenye nchi hii, Rasilimali ambayo haitoi mchango wake kwa maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Waziri Jenista J. Mhagama (Mb) ameiagiza Tume ya Utumishi wa Umma kuhakikisha kuwa Ukaguzi wa Rasilimali Watu katika Taasisi za Umma kuangalia uzingatiaji wa Sera, Sheria, Kanuni, taratibu na Miongozo inayotolewa iwe ni kipaumbele cha Tume.