'Vyama vya siasa vitoe fursa zaidi kwa wagombea wanawake'

NA MATHEW KWEMBE

TANGU ufanyike Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi nchini mwaka 1995, idadi ya wanawake wanaowania uongozi kupitia vyama vya siasa katika nafasi za ubunge na udiwani imekuwa ikiongezeka kutoka uchaguzi mmoja kwenda mwingine.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika WILDAF, Anna Kulaya akizungumza kwenye mojawapo ya mikutano yao ya kuhamasisha wanawake kugombea kwenye nafasi mbalimbali za uongozi nchini.

Kutokana na ongezeko hili, idadi ya wanawake katika Bunge la Jamhuri ya Muungano kufuatia uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 imefikia asilimia 37.

Hata hivyo, baadhi ya wadau wa siasa wanashauri kuwa ipo haja kwa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu kutenga nafasi zaidi kwa wanawake kugombea nafasi za ubunge na udiwani ili kuongeza ushiriki wao katika vyombo hivyo vya uamuzi.

Mmoja wa wadau hao ni Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) Dkt. Rose Reuben ambaye anabainisha kuwa vyama vya siasa vinavyopata nafasi ya kuteua wabunge na madiwani havina budi kuteua wagombea wengi wanawake ili waweze kushika nyadhifa hizo.

“Vyama vya siasa ndivyo vinavyopendekeza majina ya wagombea wa ubunge na udiwani kuwania nafasi za uongozi, kama vitaamua kutoa fursa zaidi kwa wagombea wanawake, uwakilishi wa wanawake utaongezeka katika vyombo vya kutoa maamuzi,” anaeleza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika WILDAF, Anna Kulaya anasisitiza kuwa kama vyama vya siasa vitazidi kuwaamini wagombea wanawake kuwania nafasi za uongozi katika chaguzi zijazo, upo uwezekano wa kufikia asilimia 50 kwa 50 nchini.

Hata hivyo, Kulaya anavitaka vyama vya siasa kutoa nafasi za ushiriki kwa wanawake wakati wa uteuzi wa kugombea nafasi za uongozi hasa ubunge na udiwani wakati zinapofanyika chaguzi hizo.

“Kuruhusu wanawake wengi zaidi kushiriki kugombea nafasi za uongozi katika chaguzi za vyama vya siasa ndiyo namna iliyo bora ya kuongeza idadi yao kuanzia ngazi za chini za uongozi hadi taifa,” anaeleza.

Kwa mujibu wa Kulaya mwamko wa wanawake katika kuwania nafasi za uongozi umekuwa mkubwa tangu uchaguzi mkuu wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi ulipofanyika mwaka 1995.

Mathalani, mwaka 2005 wakati uchaguzi mkuu wa vyama vingi unafanyika kwa mara ya tatu idadi ya wanawake walioteuliwa na vyama vyao vya siasa kuwania nafasi za ubunge ilikuwa ni 159 ambapo jumla ya wagombea 1,222 waliwania nafasi za ubunge.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 jumla ya wagombea 1,036 kutoka vyama vya siasa 18 vilivyokuwa na usajili wa kudumu waliteuliwa kugombea Ubunge katika majimbo 239 ya Uchaguzi, ambapo idadi ya wagombea wanawake ilikuwa 191 sawa na asilimia 18.4.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, idadi ya wanawake walioteuliwa kuwania nafasi ya ubunge ilikuwa 233 sawa na asilimia 19 ambapo jumla ya wagombea 1,209 waliteuliwa kuwania nafasi ya ubunge.
Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) Dkt. Rose Reuben akichangia umuhimu wa vyama vya siasa kuongeza idadi ya wagombea wanawake katika chaguzi zijazo za kidemokrasia nchini.

Kadhalika, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, jumla ya wagombea 1,257 waliteuliwa kugombea Ubunge katika majimbo 264.

Kati ya wagombea hao wanawake walikuwa ni 293 sawa na asilimia 23 na wanaume walikuwa 964 sawa na asilimia 77.

Kwa upande wa nafasi za udiwani katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, jumla ya vyama vya siasa 18 viliwateua wagombea 7,561 katika Kata 2,552 kushiriki uchaguzi huo.

Katika uchaguzi mkuu huo, wagombea wanaume 7,120 waliteuliwa na vyama vyao kuwania nafasi hizo huku idadi ya wagombea udiwani wanawake ilikuwa ni 441.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 jumla ya wagombea 7,934 waliteuliwa kugombea udiwani kwenye jumla ya Kata 3,335.

Idadi ya wagombea wanawake iliongezeka na kufikia 559 kati ya jumla ya wagombea 7,934 walioshiriki uchaguzi mkuu huo ambapo wagombea wanaume walikuwa 7,375.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, uteuzi wa nafasi za udiwani ulifanyika katika kata 3,946 ambapo jumla ya wagombea 10,716 waliteuliwa kuwania nafasi za viti vya udiwani.

Jumla ya wagombea wanawake 670 na wanaume 10,046 waliteuliwa na vyama vya siasa 22 kushiriki uchaguzi mkuu huo.

Kwa upande wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, jumla ya wagombea Udiwani 9,231 waliteuliwa katika kata 3,953. Kati ya hao, 8,563 walikuwa wanaume sawa na asilimia 92.76 na 668 walikuwa wanawake sawa na asilimia 7.24.

Ukiacha idadi hiyo ya wagombea ubunge na udiwani walioteuliwa na vyama vya siasa kuwania nafasi za uwakilishi kupitia majimbo yao ya uchaguzi, idadi ya wabunge na madiwani wanawake imekuwa ikipatikana kupitia Viti maalum.

Huu ni utaratibu unaopatikana katika nchi mbalimbali duniani unaolenga kuongeza idadi ya wanawake katika bunge na mabaraza katika siasa kwa jumla.

Kwa mujibu wa Mkataba wa uondoaji wa ubaguzi wowote wa wanawake (CEDAW) ulioanzishwa mwaka 1981 na kutiwa saini na mataifa 189 nchi nyingi duniani ikiwemo Tanzania zilichukua hatua za kuongeza nafasi za wanawake serikalini.

Aidha, taratibu za kisheria za kutenga sehemu ya viti vya bunge kwa wanawake pekee zilifuatwa na mwaka 2013 utaratibu huu ulitumiwa katika nchi 36, hasa za Afrika na Asia Kusini.

Kwa mujibu wa Ibara ya 66 (1) (b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Wabunge wanawake wa Viti Maalum ni asilimia thelathini ya Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watakaochaguliwa na vyama vya siasa kwa mujibu wa ibara ya 78, na kwa kuzingatia masharti ya uwiano wa kura.

Awali idadi ya Viti Maalum Wanawake ilikuwa asilimia 30 hata hivyo, Serikali iliongeza idadi hiyo hadi kufikia asilimia 40.

Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 wabunge wanawake wa viti maalum walikuwa 75, mwaka 2010 wabunge wa viti maalum walikuwa 102, mwaka 2015 idadi ya wabunge wa viti maalum ilikuwa 113.

Kwa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020, idadi ya Wabunge Wanawake wa Viti Maalum ilikuwa 113 na walipatikana kutoka kwenye vyama vilivyopata asilimia tano (5%) au zaidi ya kura zote halali za Ubunge kama ilivyoainishwa katika ibara ya 78(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Dkt. Wilson Mahera Charles anaeleza kuwa ingawa idadi ya asilimia 37 ya wabunge wanawake si haba lakini ipo haja kwa vyama vya siasa kushawishiwa zaidi kuongeza idadi ya wanawake katika teuzi zake za kuwania ubunge na udiwani.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Dkt. Wilson Mahera Charles akisisitiza jambo katika mkutano na wadau wa siasa hivi karibuni.

Anabainisha kuwa kama vyama vya siasa hasa vile vyenye uwakilishi mkubwa bungeni vitateua wagombea wengi wanawake kuwania nafasi za uongozi, uwezekano wa kufikia asilimia 50 ya wanawake katika viti vya ubunge na udiwani utakuwa mkubwa.

Kwa ujumla, vyama vya siasa vina fursa kubwa ya kuteua wagombea wanawake katika majimbo yao hasa vyama vya siasa ambavyo vina wabunge wengi ili kuongeza wigo wa wanawake katika kuwania nafasi za uongozi wa kisiasa na hii itasaidia kufikiwa kwa asilimia 50 kwa 50 kwenye uongozi kati ya wanawake na wanaume.

Mathew Kwembe ni Afisa Habari Mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi anapatikana kupitia simu 0656577945.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news