Wasichana wanaohifadhiwa Hope Mugumu Nyumba Salama watunukiwa vyeti na Chuo cha Alison nchini Uingereza

NA FRESHA KINASA

CHUO cha Alison cha nchini Uingereza kimewatunuku vyeti wasichana 10 wanaohifadhiwa Kituo cha Hope Mugumu Nyumba Salama kinachomilikiwa na Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania linalojishughulisha na mapambano ya Ukatili wa Kijinsia mkoani Mara kufuatia wasichana hao kuhitimu mafunzo ya kompyuta ngazi ya cheti waliyokuwa wakiyasoma kwa njia ya mtandao katika chuo hicho.
Wasichana hao ambao wanapata hifadhi katika kituo hicho kufuatia kukimbia ukatili wa kijinsia (ukeketaji) kutoka katika familia zao wamekabidhiwa vyeti hivyo leo Mei 20, 2022 na Mike feerick kutoka chuo hicho alipofika katika kituo hicho kilichopo Mugumu Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara.

Mike amesema kuwa, elimu waliyoipata itawasaidia kuendana na ukuaji wa teknolojia katika ulimwengu wa sasa katika nyanja mbalimbali. Huku akiahidi kushirikiana na Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania ikiwemo kuweka maudhui ya elimu ya madhara ya Ukatili wa Kijinsia katika mtandao.
Pia, amepongeza juhudi za Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania pamoja na Serikali katika kuendelea na mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo kutoa elimu kwa jamii na kuwaendeleza kitaaluma na kifani wasichana ambao wamekuwa wakipata Hifadhi katika Kituo cha Hope Mugumu Nyumba Salama.
Akizungumza kwa niaba ya wahitimu wenzake mmoja wa wahitimu hao, Florida Johnson amesema kuwa elimu hiyo itakuwa na tija kwao katika kuwasaidia masuala mbalimbali muhimu.
Pia, Johnson amelishukuru Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania kwa kuwezesha mafunzo hayo kwao pamoja na kuendelea kuwapa huduma zote muhimu na kuwaendeleza kifani na kielimu wasichana waliopo Katika kituo hicho.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Shirika la (HGWT),Rhobi Samwelly Mkuu wa Kituo cha Hope Mugumu Nyumba Salama Daniel Misoji amesema shirika hilo kwa sasa kwa kushirikiana na Dawati la Jinsia na Watoto, Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii wanaendelea na utoaji wa elimu Katika shule za Msingi Wilayani Serengeti juu ya madhara ya vitendo vya ukatili wa Kinjinsia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news