NA SOPHIA FUNDI
HALMASHAURI ya Wilaya ya Karatu mkoani Arusha inatarajia kutoa chanjo ya matone ya Polio kwa watoto zaidi ya 41,000 chini ya miaka mitano kwa awamu ya pili.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa chanjo hiyo mganga mkuu wa wilaya,Dkt.Lucas Kazingo amesema kuwa, chanjo hiyo itatolewa kuanzia Mei 18 hadi Mei 21, 2022 katika vituo vyote vya afya vya wilaya pamoja na zahanati.
Amesema kuwa, pamoja na chanjo kutolewa katika vituo vya afya pia kutakuwa na timu ya wataalam itakayozunguka nyumba kwa nyumba itakayoongozwa na wenyeviti wa vitongoji ambao watatoa chanjo kwa watoto chini ya miaka mitano watakaokutwa katika nyumba hizo.


Naye mwakilishi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), Sally Emanuel aliwaomba wananchi kuepuka upotoshaji kuhusiana na chanjo ya polio inayotolewa kwani chanjo hiyo ni salama.
Amewasihi wananchi pale wanapomuona mtoto anadalili yoyote ya ugonjwa huo waripoti hospitali Ili apatiwe huduma ya afya kabla hajaambukiza wengine.
