NA DIRAMAKINI
WAUGUZI mkoani Pwani wametakiwa kufanya kazi kama alivyokuwa mwasisi wa uuguzi Florence Naitngel ili kumuenzi na kunusuru vifo vya mama wajawazito na watoto na wagonjwa wengine.
Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Shangwe Twamala ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa huo wakati sherehe ya siku ya Wauguzi Mkoani Pwani iliyoandaliwa na Chama Cha Wauguzi Tanzania (TANNA) Mkoa wa Pwani.
Twamala alisema kuwa, mwasisi huyo wa uuguzi alikuwa ni wa mfano kwa kutoa huduma nzuri kwa wagonjwa akizingatia maadili ya kazi yake.
Alisema, moja ya changamoto iliyopo ni vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga hivyo maarifa yao watumie maarifa kukabiliana na vifo vya mama wajawazito ambapo kwa mwaka jana vilikuwa 51 na watoto 390.
Alisema kuwa, hali hiyo siyo nzuri lazima jitihada zifanyike kuzuia vifo hivyo ambapo hiyo ni changamoto kubwa sana ambayo inapaswa kufanyiwa kazi ili kupunguza tatizo hilo ambalo linasababisha kupoteza watu wengi.
"Tunajua kuna changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja ikama, vifaa, nyumba, usafiri na mengine lakini serikali inafanyia kazi changamoto zinazojitokeza lakini wasikate tamaa kwani ya afanyiwa maboresho,"alisema Twamala.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama Cha Wauguzi Tanzania (TANNA) Veronica Makange alisema kuwa siku hiyo waliadhimisha kwa kufanya mazoezi ya kutembea kisha kutoa zawadi mbalimbali kwa wagonjwa waliolazwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Tumbi.
Makange alisema kuwa malengo yao ni kujenga majengo kwa ajili ya kutolea mafunzo ya uuguzi ili kuzalisha wauguzi wengi ambapo mkoa huo kupitia chama hicho kuwa wa kwanza kumiliki chuo cha uuguzi.
Awali akisoma risala ya chama hicho, Katibu wa TANNA mkoa wa Pwani Dafroza Mzava alisema kuwa wanaomba kupewa kipaumbele kwenye kupata elimu ya kutosha, vifaa vya kisasa, mazingira mazuri ya kazi na motisha kwani wao muda mwingi wako na wagonjwa.
Mzava alisema kuwa, changamoto kubwa waliyonayo ni upungufu wa wauguzi ambapo mkoa una wauguzi 2,591 kukiwa na upungufu wa wauguzi 1,312.