Wawekezaji kutoka Uingereza, Norway wabisha hodi Tanzania, Waziri Nchemba awapa taarifa njema

NA BENNY MWAIPAJA-WFM

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amewahakikishia wawekezaji kutoka Uingereza na Norway kwamba Serikali itatoa ushirikiano mkubwa ili kufanikisha uwekezaji wao hapa nchini kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji pamoja na vivutio kadhaa.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), (aliyesimama) akiwahamasisha wawekezaji kutoka Uingereza na Norway waliomtembelea kwenye Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam, ambapo walijadili kuhusu fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana nchini Tanzania.

Dkt.Nchemba ametoa ahadi hiyo jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na kundi la wawekezaji kutoka nchini Uingereza na Norway, wanaotaka kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali hapa nchini.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (wa nne kulia) akiwa katika picha ya pamoja na kundi la wawekezaji kutoka Uingereza na Norway pamoja na baadhi ya viongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango, baada ya kumalizika kwa kikao cha majadiliano kuhusu fursa na vivutio vya uwekezaji vinavyopatikana nchini Tanzania, mkutano huo umefanyika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi Ndogo Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kulia) akisalimiana na Balozi wa Norway nchini Tanzania Mhe. Elisabeth Jacobsen, baada ya kumalizika kwa kikao cha majadiliano kati yake na ugeni wa wawekezaji kutoka Norway na Uingereza, kuhusu fursa na vivutio vya uwekezaji vinavyopatikana hapa nchini, mkutano huo umefanyika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi Ndogo, Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dar es Salaam.

Ujio wa wawekezaji hao wanaotaka kuwekeza kwenye sekta za kilimo, nishati, uchimbaji na uchakataji madini, ujenzi wa miundombinu mbalimbali, ni matunda ya ziara ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyoifanya katika nchi za Ubelgiji na Nchi za Kiarabu hivi karibuni

Dkt. Nchemba aliwahakikishia wawekezaji hao tarajiwa, kwamba Serikali itaendelea kuboresha sera za uwekezaji na kuwatoa hofu kwamba Serikali ina sera za uwekezaji za uhakika, za kuvutia na zinazotabirika ili iweze kushiriki kikamilifu katika biashara za kimataifa, kikanda na kukidhi soko la ndani.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji-Huduma za Fedha wa Africa Finance Corporation Bw. Sanjeev Gupta, anayetafuta fursa za uwekezaji nchini Tanzania, baada ya kumalizika kwa kikao cha majadiliano kuhusu uwekezaji, Katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi Ndogo, Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa amani na usalama vilivyopo nchini, upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya kuwekeza, uwepo wa idadi kubwa ya walaji likiwemo soko la ndani na soko la ukanda, ni fursa nyingine itakayowawezesha wawekezaji hao kupata faida katika uwekezaji wao.

Wakizungumza katika kikao hicho, wawekezaji hao walipongeza jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kuhamasisha uwekezaji pamoja na kuweka mazingira mazuri na rafiki ya uwekezaji na ufanyaji biashara.

Walisema kuwa wamekuja nchini kukutana na wadau zikiwemo Wizara na Taasisi mbalimbali ili kujifunza zaidi namna watakavyowekeza mitaji na teknolojia kwenye sekta za kilimo, uzalishaji wa umeme, uchakataji madini, mafuta na gesi.
Kiongozi wa ujumbe wa wawekezaji kutoka Norway na Uingereza walioko katika ziara ya kuangalia maeneo ya kuwekeza nchini Tanzania, Bw. Lanre Akinola, akizungumza jambo kwenye mkutano kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na wawekezaji hao, Ofisi Ndogo za Wizara, Jijini Dar es Salaam. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango).

Mwenyekiti wa wawekezaji hao Bw. Lanre Akinola, alisema kuwa katika miaka michache ijayo, Tanzania inatabiriwa kuwa itakuwa na uchumi imara na wenye nguvu zaidi kutokana na kutarajia kupata wawekezaji wengi kutoka Uingereza na Norway, hatua itakayo kuza uchumi pamoja na kuzalisha ajira kwa wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news