NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe amezindua Bodi ya Wakurugenzi ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji leo tarehe 14 Mei, 2022 jijini Dodoma, na kuitaka kuainisha maeneo mbalimbali ambayo kwa ujumla wake ni hekari milioni 29 yanayofaa kwa umwagiliaji.
Waziri Bashe ameitaka bodi hiyo kuziweka hekari hizo katika mfumo wa kidigitali ili wizara ya Kilimo iuwasilishe mchoro huo katika Wizara ya Ardhi na maeneo husika yatakayokuwa yameahinishwa yatengwe kwa shughuli za kilimo.
Alisema, kutokana na shauku kubwa ya wananchi ya kutaka kuyaona mafanikio ya kilimo cha umwagiliaji, hivyo ni jukumu la Bodi hiyo kusimamia miradi ya maji kikamilifu na kuhakikisha inakuwa na tija.
“Mfano maeneo ya karibu na Mto Rufiji na Lubada, pia eneo la Ziwa Victoria, Tanganyika, Rukwa, Mto Ruvuma na maeneo mengine ambayo yanafaa kuanzishwa kwa miradi ya umwagiliaji ni lazima maeneo hayo ijengwe miradi mikubwa yenye tija, na ninaiagiza bodi kuhakikisha yanajengwa mabwawa yenye viwango stahiki yatakayosaidia upatikanaji wa maji ya uhakika hata kama mvua isiponyesha mabwawa hayo yatumike kumwagilia na kuzalisha,”amesema.
Aliitaka bodi kufanya kazi kibiashara hasa kwa kusimamia mapato yatokanayo na miradi ya umwagiliaji badala ya kuviachia jukumu hilo vyama vya ushirika na kuitaka bodi kutambua kuwa kwa kusimamia vema mapato inakuwa kwenye mazingira mazuri zaidi ya kukopeshwa fedha kutoka kwenye Taasisi za fedha mbalimbali kutokana na kuwa na rekodi nzuri ya mapato.
“Yani sheria inaruhusu Mfuko wa Maendeleo ya Umwagiliaji kupatiwa asilimia tano kutoka katika mapato yatokanayo ya miradi ya umwagiliaji, mapato haya yakikusanywa yataweka rekodi nzuri ya fedha itakayouwezesha mfuko kukopeshwa,” alisema Bashe.
Aidha,ameiagiza bodi hiyo kuhakikisha, serikali haipotezi fedha yoyote kutoka kwenye miradi ya umwagiliaji na kuanza kukusanya mapato hayo.
Pia ameongeza kuwa, bodi ifanikishe ujenzi wa mabwawa makubwa ya umwagiliaji kuanzia hekari 20 na kuendeea ili iwe na tija kubwa zaidi na kuepuka kutoa zabuni za ujenzi wa mabwawa kwa mitazamo ya kisiasa.
Katika kuhakikisha kuwa serikali inawezesha kilimo cha umwagiliaji, Bashe alibainisha kuwa ofisi zaidi 140 zitafunguliwa kwa ajili ya wahandisi wa umwagiliaji watakaokuwa na jukumu na kusimamia miradi pamoja na kukusanya mapato.
Bodi hiyo inaongozwa na Mwenyekiti Prof. Henry Mahoo huku wajumbe ni Mhandisi Anna Green Mwangamilo, Bw Nathael Nhonge Mathew,Mhandisi Athumani J Kilundunya, Bi Emelda Teikwa Adam, Dk Gift Joseph Kweka, Bw John John Nchimbi, Bw Stephen Mngodo Michael, Bw Revocatus Valery, Bw Kimario, Bw Joseph Lutago Dk Upendo Eliuze Msovu.