NA OR-TAMISEMI
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI),Mhe. Innocent Bashungwa amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga kuhakikisha wanajenga jengo la mionzi katika Kituo cha Afya Ngamiani kwa kutumia mapato ya ndani.Waziri Bashungwa ameagiza hayo wakati wa ziara yake jijini humo na kutembelea kituo hicho cha Afya kikongwe ambacho hapo awali kilishapata shilingi milioni 400 kwa ajili ya uboreshaji.
Akiwa katika kituo hicho, Mhe. Bashungwa amesema Kituo cha Afya Ngamiani ni kikongwe na kinahudumia watu wengi na kinasaidia kupunguza msongamano kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, "sasa kinapokua hakuna huduma ya mionzi hatuwatendei haki watu wa Tanga,"amesema Mheshimiwa Bashungwa.
"Wakati umefika sasa wananchi wanaopata huduma katika Kituo hiki wakaanza kupata huduma ya mionzi na kwa sababu Jiji hili lina mapato mengi, mnaweza kabisa kujenga jengo hilo, sasa niwaelekeze kuhakikisha jengo la utawala linajengwa haraka na linaaamza kutoa huduma,"amesema.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Adam Malima amesema eneo la Kituo cha Ngamiani ni dogo hivyo wataangalia namna ya kubomoa baada ya majengo ya zamani ili wapate eneo ambalo wanaweza kulitumia hata kwa kujenga kwenda juu ili kuzingatia matumizi bora ya ardhi.
Kituo cha Afya Ngamiani kilichopo katikati ya Jiji la Tanga huwa kinahudumia wagonjwa 200 hadi 250 kwa siku na idadi ya akinamama wanaojifungua kwa mwezi ni kati ya 150 hadi 200.