Waziri Bashungwa aeleza faida za uboreshaji miundombinu ya usafirishaji mkoani Kigoma

NA OR-TAMISEMI

JITIHADA za Serikali katika kuboresha miundombinu mbalimbali mkoani Kigoma zinalenga katika kuondoa changamoto ya miundombinu ya usafiri na usafirishaji kwa njia ya barabara na meli ili kuwezesha uwekezaji na biashara baina ya mkoa huo na nchi za Maziwa Makuu.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Innocent Bashungwa (Mb) wakati akifunga Kongamano la Uwekezaji na Biashara la nchi zinazozunguka Ziwa Tanganyika na Ukanda wa Maziwa Makuu ambapo amesema kuwa Serikali imewekeza fedha nyingi ili kuunga barabara za Mkoa wa Kigoma na mikoa mingine kwa kiwango cha lami.

Pia ameongeza kuwa, usafiri wa meli katika Ziwa Tanganyika, umeme wa kiwango cha Gridi ya Taifa pamoja na upanuzi wa uwanja wa ndege ni moja ya vipaumbele vya Serikali katika kuufungua Mkoa wa Kigoma ili kuvutia biashara na uwekezaji.h

"Dhamira ya Serikali ni kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya kufanya biashara na uwekezaji, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha tunaweka mazingira ya kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara kwa wawekezaji wetu nchini, na kuhakikisha kuwa maboresho yote tunafanya katika uwekezaji na ufanyaji biashara, yanakuwa endelevu,"amesema.

Amesema kuwa, mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita ni kuondoa kero za wawekezaji na wafanyabiashara wa nje na ndani ya nchi.

Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa kushirikiana na wadau wa uwekezaji na biashara nchini, imeweza kutatua kero mbalimbali kupitia majadiliano ya kusikiliza kero za uwekezaji wao, na kuzipatia ufumbuzi na majawabu kwa haraka.
Sambamba na hilo, ameongeza kuwa Serikali kwa sasa imeweka kipaumbele katika kuvutia miradi ya uwekezaji, kwenye sekta zenye matokeo makubwa kiuchumi kwa wananchi, kwa lengo la kuimarisha minyororo ya thamani kwenye mazao ya kilimo, uvuvi na mifugo (ASDP II), ambayo yanaajiri wananchi wengi.

Waziri Bashungwa amewaeleza wadau kuwekeza katika uzalishaji wa bidhaa zinazotokana na malighafi zinazopatikana Kigoma na mikoa ya jirani.

“Chukueni pia matokeo ya kongamano hili kama fursa mkitambua kuwa fursa, haziletwi bali zinatafutwa na kuzitumia. Kwa kufanya hivi mtakuwa mmeitikia wito wa Serikali, wa kujenga uchumi wa viwanda, ili kuchochea mageuzi ya uchumi na maendeleo ya watu,”amesisitiza.

Amesema,juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuufungua mkoa wa Kigoma zinaendelea ikiwa pamoja na ujenzi wa barabara kiwango cha lami Manyovu-Kasulu Kibondo-Kabingo yenye km. 260.6, barabara ya Uvinza-Malagarasi - km. 51, na barabara ya Kaliua-Malagarasi-Ilunde (156 km.).
Aidha, katika Ziwa Tanganika Serikali ya imeanza hatua za ujenzi na ukarabati wa meli ambapo zaidi ya shilingi Bilioni 10 zimetengwa kwa ajili ya Ujenzi wa Meli mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 400 za mizigo, na Mwili yenye uwezo wa kubeba tani 2800 za Mizigo, pia kukarabati Meli ya MV Liemba, MV Sangara.

Uimarishaji wa usafiri katika Ziwa Tanganyika unamaanisha kuifungua Kigoma kiuchumi ndani na nje ya mipaka ya Tanzania, hivyo itakuwa fursa kubwa kwa wafanyabiashara kusafirisha bidhaa mbalimbali.

Nishati ya umeme Umeme wa Gridi ya Taifa zimefanyika ikiwa pamoja na Ujenzi wa Kituo cha kupozea Umeme
Kilovoti 132 kutokaTabora – Kigoma kule Nguruka, umeme wa msongo wa Kilovolti 400 kutoka Nyakanazi-Kigoma ambapo hadi kufikia 2023 Mkoa wa Kigoma utakuwa umeunganishwa na Umeme wa Uhakika wa Gridi ya Taifa hivyo kuruhusu mazingira bora ya uwekezaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news