NA ANGELA MSIMBIRA, OR-TAMISEMI
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa amebariki mapendekezo ya Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Moshi ya kujengwa kwa Hospitali ya Wilaya katika Kijiji cha Chekereni Kata ya Mabogini mkoani Kilimanjaro.

Waziri Bashungwa ameendelea kufafanua kuwa, lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za afya hivyo kamati hiyo ipo sahihi kulingana na miongozo iliyowekwa na Serikali.
Amesema, vigezo vilivyotumika kuchagua eneo hilo ni uwepo wa eneo ambalo halina mgogoro, wingi wa watu, jografia ya eneo, umbali wa eneo ambao ni kilomita 35 kutoka Moshi Mjini na uduni wa taasisi zilizopo katika Kata ya Mabogini tofauti na Kata ya Kilua Vyunjo Kusini ambapo mchakato wa kukabidhi ardhi kwa Mkurugenzi bado unaendelea kwa kuwa bado wananchi hawajavuna mazao yao.

Waziri Bashungwa amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Mhandisi Daniel Kileo kuhakikisha anaanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya mara moja katika Kata ya Mabogini na kumuagiza Meneja wa TARURA Mkoa kuhakikisha wanajenga barabara katika eneo linalojengwa hospitali hiyo.

Aidha, mgogoro wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya umedumu kwa takribani miezi tisa ambapo tayari kiasi cha shilingi milioni 500 zilishatengwa kwa ajili ya ujenzi huo katika bajeti ya mwaka 2021/2022.