NA ANGELA MSIMBIRA, OR-TAMISEMI
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza mishahara ya watumishi wa umma kwa asilimia 23.3.
Akitoa salamu za Ofisi ya Rais-TAMISEMI leo Mei 18, 2022 kwenye uzinduzi wa barabara Tabora-Koga-Mpanda yenye urefu wa kilometa 342.9, uliofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, Mhe.Bashungwa amesema asilimia 75 ya watumishi wanatoka kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, hivyo amemuahidi Rais kufanyakazi kwa weledi katika kuwatumikia wananchi.
Waziri Bashungwa pia amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza bajeti ya Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini katika Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge hadi kufikia asilimia 193 na kubadilisha mandhari ya eneo hilo.
Amesema, kwa upande wa ujenzi wa kituo cha afya Serikali imetoa fedha kiasi cha shilingi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya cha Tutuo na kwa upande utatuzi wa changamoto za ujenzi wa nyumba za waalimu nchini katika bajeti ya mwaka 2022/2023 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 55.57 kwa ajili ya ujenzi huo
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu kwenye zoezi la anuani ya makazi na kujitokeza kuhesabiwa ili serikali iweze kuwatambua na kuweza kutoa huduma bora kulingana na takwimu zilizopo.